Zoezi la uwekaji alama za mipaka eneo la UDOM, Njombe lakamilika

Na Amiri Kilagalila

Uongozi wa Kata ya Utalingolo kwa kushirikiana na wataalamu wa Idara ya Ardhi Halmashauri ya Mji Njombe jana Mei 13, 2025 wamekamilisha zoezi la uwekaji wa alama za mipaka (bikoni) kwenye eneo la Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Tawi la Njombe lenye ukubwa wa takribani ekari 300 lililopo katika kijiji cha Ihalula, ambalo litatumiwa na wanafunzi wa chuo hicho kwa ajili ya mazoezi ya vitendo.

Hapo jana akiongoza zoezi la uwekaji wa alama za mipaka, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Njombe ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Utalingolo, Erasto Mpete amewataka wananchi wa kijiji hicho kuendelea kuimarisha ulinzi wa eneo hilo kwa maslahi ya Watanzania.

“Niwaombe wananchi waendelee kulinda hili eneo kwa maslahi ya kizazi chetu na vizazi vijavyo, lakini pia wananchi muwe na subira kwa sababu ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya chuo hiki unaenda kwa awamu. Na kwa hatua ya kwanza ujenzi umeanza ofisi kuu pale Njombe mjini na huku ni eneo la mazoezi kwa vitendo kwa hiyo wananchi wanaozunguka hili eneo huko mbeleni watanufaika kiuchumi” amesema Mpete.

Baadhi ya wananchi wakishiriki katika zoezi la uwekaji wa alama za mipaka katika eneo la Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Tawi la Njombe katika kijiji cha Ihalula. Picha na Amiri Kilagalila.

Mpete pia ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha fedha za ujenzi wa Chuo Kikuu mkoani Njombe ambapo ametoa pongezi kwa Mkuu wa mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, Mbunge wa Njombe Mjini, Deodatus Mwanyika pamoja na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kuendelea kushikamana ili kukuza uchumi na miradi ya maendeleo mkoani humo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Njombe ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Utalingolo, Erasto Mpete wakati akizungumza na wananchi wakati wa uwekaji wa alama za mipaka. Picha na Amiri Kilagalila.

Stanley Nyangachi ambaye ni mkazi wa Utalingolo ameishukuru serikali kwa kukubali kujenga Chuo Kikuu mkoani Njombe kwa kuwa nao pia wanakwenda kunufaika na uwepo wa chuo hicho.

“Kimsingi hata sisi wananchi wa Utalingolo tunakwenda kunufaika na chuo hiki lakini na sisi tunawakaribisha wawekezaji kwa sababu fursa zitafunguliwa kwenye maeneo yetu” ameeleza Nyangachi.

Zoezi hilo la uwekaji wa alama za mipaka limefuatia baada ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Tawi la Njombe na kampuni ya Dimetoclasa Real Hope Limited kusaini mkataba wa ujenzi wa miundombinu ya chuo hicho siku ya Jumatatu Mei 12, 2025 unaotarajia kufanyika katika mtaa wa Kihesa uliopo Halmashauri ya Mji wa Njombe.

Baadhi ya wananchi wakitoa ushirikiano wakati wa zoezi la uwekaji wa alama za mipaka.

Kwa mujibu wa Naibu Mratibu wa Mradi wa HEET kutoka Chuo kikuu cha Dodoma Dkt. Happiness Nnko alipozungumza mkoani Njombe wakati wa kusaini mkataba wa ujenzi wa miundombinu ya chuo hicho, alisema kuwa kiasi cha Tsh. Bilioni 17.17 kimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu sita ya msingi katika chuo hicho, ambapo ujenzi unafanyika katika mtaa wa Kihesa mjini Njombe.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni inayokwenda kutekeleza mradi huo ya Dimetoclasa Real Hope Limited, Bwana Dickson Mwipopo aliahidi kufikisha mitambo eneo la ujenzi katika mtaa wa Kihesa ili kazi ianze mapema, ambapo utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa chuo kikuu hicho unatarajia kugharimu kiasi cha Tsh. Bilioni 20.

Aidha, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Prof. Rwekaza Mukandala alisema kutokana na ongezeko kubwa la wanafunzi kwenye vyuo vikuu nchini, Rais Samia Suluhu Hassan aliamua kuongezwa kwa matawi ya vyuo likiwemo tawi la Njombe.

Hata hivyo Mkuu wa mkoa wa Njombe, Antony Mtaka alisema suala la elimu kwa wakazi mkoani humo ni muhimu, ambapo wazazi wanahamasa kubwa ya kusomesha watoto wao.

Mwandishi: Amiri Kilagalila

Mhariri: Dominic Allen

Hot this week

CHADEMA kutoa msimamo wake kuhusu maridhiano

By Veronica Mlyatu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa...

Mnyonge, mnyongeni ila haki yake mpeni

By Dorlingson Edward Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), leo...

Popular Articles

Safari ya Mashimba katika kutetea jamii ya Wahadzabe

Nchini Tanzania  kuna jumla ya makabila zaidi ya 120...

Polisi waendelea kuwashikilia viongozi wa CHADEMA

Ni siku ya kwanza tangu kukamatwa kwa viongozi wa...

Siku ya Vijana Duniani.

Kwa sasa ni kijana wa miaka 25 ambaye amejiajiri...

BWAWA LA ARBA’AT  LASABABISHA MAAFA NCHINI SUDAN

Watu 30 mashariki mwa Sudan na na wengine 60...

Sand Mining in Tanzania: Trails of Destruction in Lake Victoria and its Environs

By Dominic Allen On November 14th, 2021 in the Geita...

 Utekaji: Fumbo linalotushinda?

Na Yohani Gwangway Taifa la Tanzania kwa miaka mingi limekuwa...

Abduction: Is it a riddle we can’t solve?

By Yohani Gwangway For many years Tanzania has been an...

Mustakabali wa Hewa Safi kwa kila kiumbe

Na Dominic Allen Msingi wa maisha ya viumbe hai yaani...
LAND DWELLERS FACT CHECK HUB VERIFY FACTS STOP MISINFORMATION Trusted Fact-Checking in Tanzania Beyond What You Know VERIFY NOW

Related Articles

Popular Categories

DWELLERS CHECK-HUB Verify Facts. Stop Misinformation Trusted Fact-Checking in Tanzania • Beyond What You Know VERIFY NOW