Na Dominic Allen
Mtalamu wa uchumi, Dkt. Bravious Kahyoza hii leo amesema sababu ya noti ya Tanzania ya Sh. 10,000 kutumika zaidi ni kutokana na matumizi makubwa ya watu kwenye chakula, vinywaji visivyo na kilevi pamoja na nguo, ambapo kwa sehemu kubwa manunuzi yake hutumia noti hiyo na mara nyingi huwa ni kwa njia ya fedha taslimu.
Ameeleza kuwa kwa wastani kwa mwaka mtu hutumia kiasi cha Tsh. Milioni 2.4 kwa ajili ya matumizi ya chakula, Tsh. Milioni 1.26 kwa vinywaji visivyo na kilevi na Tsh. 237,799 kwenye manunuzi ya mavazi.
Dkt. Kahyoza amebainisha hayo kufuatia ripoti mpya ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inayoeleza kuwa nchini Tanzania noti ya Sh. 10,000 ndiyo hutumika zaidi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya BoT, noti ya Sh. 10,000 pia inachangia zaidi ya asilimia 85 ya fedha zote zinazozunguka nje ya mfumo wa benki.
Ripoti hiyo pia imeeleza kuwa zaidi ya Tsh. Trilioni 7.1 za noti za Sh. 10,000 zipo kwenye mzunguko kwa ajili ya matumizi ya kila siku kote nchini, ikilinganishwa na noti za Sh. 5,000 ambapo zilizopo kwenye mzunguko zina thamani ya Tsh. Bilioni 674, noti za Sh. 2,000 zikiwa Tsh. Bilioni 279, noti za Sh. 1,000 zikiwa Tsh. Bilioni 199, huku noti za Sh. 500 zikiwa Tsh. Bilioni 60 pekee.
Chanzo: Clouds Media
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


