Na Dominic Allen
Wataalamu kutoka Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC) wakiongozwa na Bw. Dakawa Msoleni Mratibu wa Miradi ya PPP katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa PPP, akiambatana na Bw. David Mushi kutoka Idara ya Miradi, pamoja na wawekezaji wa Kampuni ya ANHUI HUAFEI INTERNATIONAL TRADES CO. LTD ya China, wamehudhuria kikao maalum kilichofanyika katika ukumbi wa Mkuu wa mkoa wa Morogoro, kujadili fursa za uwekezaji katika kilimo biashara.

Kikao hicho kiliongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Mussa Ally Mussa, akiwa ameambatana na Dkt. Rozalia Rwegasira ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi (Uchumi na Uzalishaji Mali), Bi. Beatrice Njawa ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi (Biashara, Viwanda na Uwekezaji), pamoja na viongozi wa Halmashauri za Wilaya ya Mlimba na Malinyi, akiwemo Bw. Filbert Mbwilo na Bw. Geofrey Kamwava.

Mjadala mkuu katika kikao hicho ulilenga kuibua na kujadili fursa za uwekezaji katika kilimo biashara ndani ya halmashauri hizo mbili, ambapo washiriki walisisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi katika kuendeleza miradi ya kilimo, kwa lengo la kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa mkoa wa Morogoro.

Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


