Na Dominic Allen
Tunapozungumzia wanasiasa watata na wenye kucheza na maneno, huwezi kumuweka kando Rais Mstaafu wa Marekani, Donald Trump.
Kwa mara nyingine anakisaka kiti cha Urais wa Marekani alichokipoteza katika uchaguzi wa Urais mwaka 2020.
Maisha yake binafsi
Mnamo mwezi Juni 14, 1946 jijini New York alizaliwa mwanasiasa Donald Trump ambaye pia ni mfanyabiasha maarufu nchini Marekani.
Trump mwenye umri wa miaka 78, ni mtoto wa nne kati ya watoto 5 wa bwana Frederick Trump na Mary MacLeod.
Alifanikiwa kujiunga na Shule ya Kijeshi ya New York kutoka mwaka 1959 hadi 1964, kabla ya kuhitimu Shahada ya kwanza Uchumi katika Chuo Kikuu cha University of Pennsylvania mwaka 1968.
Mwaka 1968 wakati wa vita vya Vietnam, Trump alikuwa na changamoto ya kiafya, hivyo akaondolewa kwenye orodha ya kuandikishwa kwenda kupigana vita hivyo.
Donald Trump ni baba wa watoto 5 na wajukuu 10. Kwa sasa Trump yupo kwenye ndoa na mwanamama Melania Trump. Kabla ya kuwa kwenye ndoa na Melanie, Trump alishawahi kufunga ndoa na Ivana Trump mwenye asili ya Czech aliyezaa nae watoto watatu ambao ni Donald Jr., Ivanka and Eric Trump.
Ivana Trump alitoa mchango mkubwa kwa Donald Trump kwani alijihusisha kwa karibu sana na miradi mingi ya kibiashara ya mume wake, ikiwa ni pamoja na Trump Tower na Grand Hyatt katika Jiji la New York, na miradi mingine.
Ndoa ya wawili hawa alidumu kwa miaka 15 kutokea mwaka 1977 na kuachana mwaka 1992.
Miongoni mwa watoto wenye mchango mkubwa kwa Donald Trump ni Ivanka Trump.
Mwezi Machi 2017, Ivanka alijiunga rasmi katika ofisi ya baba yake katika Ikulu ya White House na kuhudumu kama Msaidizi wa Rais.
Mwezi Julai mwaka huo huo Ivanka, alimwakilisha baba yake katika mkutano wa nchi tajiri wa G20.
Chombo cha habari cha Bloomberg, kinasema kuwa Trump ana utajiri wa Dola za Marekani bilioni 6.5 huku akimiliki Trump Media & Technology Group Corp na sehemu ya ghorofa maarufu kama Trump Tower, Manhattan, New York City.
Maisha yake ya Siasa
Donald Trump ambaye anagombea nafasi ya Urais kupitia chama cha Republican ameandika vitabu kadhaa, kitabu chake cha hivi karibuni amekipatia jina la ‘Save America’ akiamaanisha ‘Okoa Amerika’.
Miaka ya 1980, Donald Trump hakuwa muumini sana wa siasa, lakini mwaka 2015 alibadili mitazamo yake na kusema kuwa angegombea nafasi ya urais.
Mwaka 2016 aligombea nafasi ya Urais kupitia chama cha Republican, akiwa na kauli mbiu ya ‘Make America Great Again’, akimaanisha ‘Kulifanya Taifa la Amerika kuwa na Nguvu Tena’ na alifanikiwa kushinda uchaguzi huo na akawa ni Rais wa 45 kuiongoza Marekani.
Mwaka 2020, Trump aligombea tena nafasi ya Urais kupitia Chama cha Republican, lakini hakufua dafu dhidi ya mpinzani wake Joe Biden kutoka chama cha Democratic.
Donald Trump amerejea tena kwa kishindo. Iwe mvua, iwe jua anakitaka kiti Urais kilichomponyoka miaka 4 iliyopita. Katika kampeni zinazoendelea mgombe huyu amekumbana na kadhia kadhaa, ikiwemo jaribio la kumuua lililotokea July 13, 2024 na la Septemba 16 mwaka huu.
Licha ya hayo yote Trump hajakata tamaa katika safari yake hii ambayo ana imani kubwa ataishinda, huku baadhi ya watu maarufu kama bilionea Elon Musk na Ben Carson ambaye ni Mwanasiasa na Daktari bingwa mstaafu wa upasuaji wa ubongo kutoka Marekani, wakimuunga mkono mwanasiasa huyu.
Miongoni mwa mambo ambayo Trump ameahidi kufanya endapo ataingia madarakani ni kuvimaliza vita vya Ukrain na Urusi, mara kadhaa amenukuliwa katika kampeni zake kuwa kama angelikuwa Rais basi vita hivyo visingetokea. Je, ataweza kutekeleza hilo analolisema? Jibu litapatikana kama atashinda uchaguzi huu.
Lakini haitakuwa kazi rahisi kuingia madarakani, kwani mgombea kutoka chama cha Democratic, Kamala Harris anaonesha ushindani mkubwa dhidi yake. Trump katika safari yake ya kuelekea katika Ikulu ya White House amemchagua JD Vance ambaye ni Seneta kutoka jimbo la Ohio, kuwa mgombea mwenza.
Katika uchaguzi wa mwaka 2016, katika moja ya mahojiano, Vance hakuonekana kabisa kuvutiwa na Donald Trump, lakini sasa amekuwa mshirika wa karibu na ndiye mgombea mwenza wa Trump katika uchaguzi utakaofanyika Novemba 05 mwaka huu.
Endapo Donald Trump ataingia madarakani, anakabiliwa na kibarua kizito ndani ya marekani na nje ya Marekani. Vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati na Ukraine, macho yameelekezwa kwa taifa la Marekani kufanya lolote lile lililo jema kumaliza vita hivi.
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


