Na Dominic Allen
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa hii leo amesema kuwa serikali imeendelea kujenga vyuo vya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) katika maeneo mbalimbali nchini ili kuimarisha utoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi.
“Katika kufikia dhamira ya kuwawezesha Watanzania kiujuzi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameongeza vyuo 65 ambavyo vitaendelea kujengwa katika mikoa na wilaya hapa nchini” amesema Majaliwa.
Waziri Mkuu Majaliwa ameeleza hayo katika hafla ya Maadhimisho ya Miaka 30 ya VETA ambayo yamefanyika katika ukumbi wa JNICC, jijini Dar es Salaam, ambapo viongozi mbalimbali wamehudhuria akiwemo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda.
Majaliwa amebainisha kuwa hadi sasa kuna vyuo 80 vya VETA ambayo vinafanya kazi, na vyuo 25 kati ya hivyo vina hadhi ya ngazi ya mkoa, huku vyuo 55 vikiwa na hadhi ya wilaya, ambapo baada ya vyuo hivyo vipya kukamilika, kutakuwa na jumla ya vyuo vya VETA 145.

Ameongeza kuwa katika kutambua umuhimu wa mafunzo ya ufundi stadi nchini, serikali ya Tanzania imeongeza bajeti ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kutoka Tsh. Bilioni 54 mwaka 2021 hadi Tsh. Bilioni 85 kwa mwaka wa fedha wa 2024/25, akisema kuwa hilo ni ongezeko la asilimia 57.4.
Hata hivyo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wadau wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini kutoka mafunzo yanayoendana na soko la ajira.
“Wadau wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini hakikisheni kwamba mafunzo yanayotolewa yanazingatia mahitaji halisi ya soko la ajira. Mahitaji ya soko la ajira tunayajua kwa kufanya tafiti za mara kwa mara kwa ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na taasisi za kimataifa” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


