Amani: Nguzo ya Maendeleo Endelevu

Na Dominic Allen.

Amani ni nguzo ya maendeleo endelevu katika nchini yoyote duniani. Amani ni kichochezi kimojawapo kinacholeta mabadiliko chanya katika nchi.

Ni karne na miongo sasa tangu ulimwengu kushuhudia Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia vilivyotokea kuanzia mwaka 1914 hadi 1918. Vita hivi vilileta hasara za kijamii, kiuchumi na kisiasa bila kusahau Vita Vikuu Vya Pili Vya Dunia vilivyopiganwa kuanzia mwaka 1939 hadi 1945. Vita vyote hivi viliitikisa dunia.

Kwa mujibu wa Shirika la Sensa Marekani, Vita Vikuu vya Vikuu vya Kwanza vya Dunia viliteketeza maisha ya takribani watu Milioni 20 na wengine Milioni 21 walijeruhiwa.

Kama ilivyokuwa katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia, kwenye Vita Vikuu vya Pili vya Dunia hali ilikuwa ni mbaya zaidi kwani Umoja wa Mataifa (UN) unatueleza kuwa inakadiriwa watu Milioni 60 walipoteza maisha kutokana na vita hii, raia wakiwa ni Milioni 40 na wanajeshi Milioni 20. Nguvu kazi kubwa ilipotea na uchumi duniani uliporomoka kutokana na kushindwa kuitunza amani.

Amani inamaanisha heshima, ustawi kwa wote, na si tu kukosekana kwa vita. Jamii yenye amani huwa na usawa, uvumilivu, maelewano, usalama na utulivu bila kusahau ushirikiano wa kijamii na utawala bora.

Kutokana na Vita Vikuu vya Kwanza, Shirikisho la Mataifa (League of Nations) lilianzishwa Januari 10, 1920, likiwa na wananchama 63 likiwa na malengo ya kudumisha na kutunza amani ili kuepukana na vita. Je, lilifanikiwa?

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Hamduny Marcel anatoa maoni yake juu ya hili.

“Lilikufa kutokana na kuwa na malengo yasiyofikika. Shirika likafa kutokana na kutokuwa na uthabiti wa mitazamo ya kisiasa na kiitikadi katika mataifa mengi ya Ulaya. Na ikaonekana ni shirika ambalo lilikuwa haliwezi kukidhi matakwa ya kuanzishwa kwake.” Amesema Hamduny.

Baada ya Shirikisho la Mataifa (League of Nations) kushindwa kutimiza lengo kuu la kudumisha na kutunza amani ulimwenguni kutokana na kuibuka kwa Vita Vikuu vya Pili, wawakilishi kutoka nchi 50 walikutana jijini San Fransisco, California na kufanya kikao kilichochukua miezi miwili yaani kutokea tarehe 25 Aprili hadi 26 Juni 1945.

Miezi minne tangu kikao hicho kufanyika, mnamo Oktoba 24, 1945 Umoja wa Mataifa (United Nations – UN) ulianza kufanya kazi rasmi na Makao makuu yakiwa jijini New York, Marekani.

Umoja wa Mataifa (UN) una malengo kadhaa ikiwemo kuratibu mahusiano ya kimataifa kupitia sheria na mikataba ya kimataifa kwenye nyanja za usalama, amani, maendeleo ya jamii na ya uchumi, haki za binadamu, uhuru, demokrasia na kadhalika.

Katika kuhakikisha lengo la kutunza amani linasimamiwa ipasavyo mikataba mbalimbali ilianzishwa. Mkataba wa Umoja wa Mataifa na Sheria ya Mahakama ya Kimataifa ulipitishwa mnamo Juni 26, 1945 na kuanza kutumika Oktoba 24, 1945.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) lilitambua umuhimu wa amani ulimwenguni, hivyo lilipitisha siku maalumu ya kuadhimisha amani mnamo mwaka 1981 na kuadhimishwa kwa mara ya kwanza Septemba 21, 1982.

Maadhimisho ya mwaka huu yakiwa na kauli mbiu ya “Kukuza utamaduni wa amani” tunaangazia ni kwa namna gani uwepo wa amani ni msingi wa maendeleo katika nchi.

Tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa (UN), kumekuwa na operesheni mbalimbali za kulinda amani kwenye nchi ambazo zina mgogoro kama vile Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, Ukraine kipindi cha hivi karibuni na nchi nyingine.

Lakini mchambuzi Hamduny anapata shaka na utendaji kazi wa Umoja wa Mataifa (UN) ya kwamba hakuna usawa katika utendaji kazi wake.

“Kinachoufanya Umoja wa Mataifa ukose nguvu zaidi ni ile kura ya turufu. Kura ya turufu ambayo inaonekana kuwa ni chombo kingine, nyenzo ya unyonyaji na ukandamizaji, ambapo wanaweza kuamua ukileta jambo ambalo mataifa mengine makubwa ya kibepari hayakubaliani nalo, yatasimamisha kwa kura turufu.” Ameeleza Hamduny.


Kutokuwepo kwa baadhi ya mataifa makubwa kama Marekani katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kunaufanya Umoja Mataifa kukosa nguvu ya kuyawajibisha mataifa hayo.

“Changamoto inakuja ni pale baadhi ya mataifa kutokuwepo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Mataifa kama Marekani ambalo limekuwa ni mtuhumiwa mkubwa wa uvunjifu wa amani katika baadhi ya maeneo duniani, baadhi ya viongozi wake wanapokosea wanashindwa kuwajibishwa.” Mtazamo wa Juma Mudimi, mchambuzi wa masuala ya siasa.

Licha ya uwepo wa Umoja wa Mataifa (UN) lakini bado hali ya amani ni kitendawili ulimwenguni, kwani uzalishaji wa silaha za kivita kwa nchi kama Korea Kaskazini unatupa mashaka na maswali kuwa silaha hizi ni kwa ajili ya kumuangamiza nani?

Hamduny Marcel anasema kuwa hakuna usawa namna Umoja wa Mataifa (UN) unashughulikia suala la udhibiti wa silaha hizo ambazo ni tishio kwa amani na maendeleo endelevu ulimwenguni.

“Baada ya Azimio la Umoja wa Mataifa, tuliona Iraq ina mitambo ya nyukila ya kutengeneza silaha na Umoja wa Mataifa ukatoa maamuzi na maelekezo mengi. Lakini bado tunaweza kuona Marekani, Uingereza, Ufaransa na hata Warusi na Wachina wakijaribu makombora haya na bila kuulizwa na mtu yeyote.” Maoni ya Hamduny.

Uhusiano wa amani na maendeleo

Amani hutengeza mazingira kwa nchi husika kuwa huru kufanya shughuli za kimaendeleo pasipo kuwa na bugudha.

Nchi ya Iceland ndiyo inaongoza kwa kuwa na kiwango kikubwa cha amani duniani, hii ni kwa mujibu wa ripoti ya Hali ya Amani Ulimwenguni ya mwaka 2024 iliyotolewa na Taasisi ya Amani na Uchumi (Institute for Economics and Peace).

Kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia, Pato la Taifa la Iceland kwa mwaka 2023 lilikuwa na Bilioni 31.02 za Kimarekani huku likitarajiwa kupanda kufikia Bilioni 33.36 za Kimarekani mwishoni mwaka 2024.

Nchi ya Yemen ambayo inashika mkia duniani kwenye suala la amani, Pato la Taifa kwa mwaka 2023 lilikuwa ni Bilioni 18.42 za Kimarekani na kwa mwaka 2024 limeshuka hadi Bilioni 16.94 za Kimarekani.

Uwepo wa amani huchangia utawala bora, ulinzi na usimamiaji wa haki za binadamu, kuvutia wawekezaji ndani na nje ya nchi, mazingira bora ya kufanya kazi kwa wananchi na mengine mengi.

Dokta Lenny Kasoga, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya uchumi anaitazama amani kama mbolea ya kuchochea maendeleo kwenye nchi.

“Amani ndiyo msingi mkubwa wa maendeleo katika nchi. Ukiangalia nchi ambazo zimevurugukiwa ambazo hazina amani kama vile Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Sudan Kusini…Ukishakosa amani unafikiria kuua, kubomoa au kumuumiza mwenzako.” Amesema Dokta Lenny.

Bila amani, maendeleo ya kiuchumi, kijamii, kisiasa, na kiutamaduni yanakuwa ni ndoto za Abunuasi.

Ni ukweli usiyopingika kuwa amani hufungua milango kwa wawekezaji kuwekeza katika sekta mbalimbali, jambo la heri kwa maendeleo ya nchi. Lakini tusisahau kuwa uwekezaji huo unapaswa pia kuwafaa wananchi wa nchi husika.

“Ukiwa na asilimia kubwa ya watu halafu ukawa haungalii kwamba wao wataishije, na ukaachia rasilimali za nchi zikaporwa na wageni na ukasema huo ni uwekezaji, basi unaweza ukawa unakaribisha matatizo.” Mtazamo  wa Dokta Lenny.

Hali ya amani Duniani kwa sasa

Tukiwa tunaadhimisha Siku ya Amani Dunia, jicho letu tulipeleke kuangazia hali ya amani katika mataifa mbalimbali ulimwenguni.

Katika baadhi ya mataifa kumekuwa na vita baina ya nchi na nchi, vita vya wenyewe kwa wenyewe, migogoro na mivutano ambayo imekuwa na athari kubwa kwa maisha ya watu na ulimwengu kwa ujumla.

Tukiimwulika Mashariki ya Kati, tunakutana na vita iliyodumu kwa miongo, ni vita vya Israel na Palestina. Vita hivi vimetafuna maelfu ya roho za wananchi kutoka pande zote mbili. Katika eneo la Ukanda wa Gaza miundombinu imeharibiwa vibaya kufuatia kutokuwepo kwa amani katika eneo hilo.

Mfululizo wa mvutano na mapigano kati ya Israel na baadhi ya mataifa kama vile Iran yameshika kasi siku za karibuni. Tangu uvamizi uliofanywa na Kikundi cha Hamas nchini Israel mnamo Septemba 7, 2023 umeipa hasira Israel, hasira ambayo imewaacha maelfu ya watu kwenye maumivu huku wengine wakipoteza maisha.

Nchi kama vile Syria imekuwa na mgogoro wa wenyewe kwa wenyewe tangu mwaka 2011, huku mataifa makubwa ikiwemo Urusi na Marekani yakichagiza migogoro nchini Syria kwa kuunga mkono pande zilizo kwenye migogoro badala ya kuzisuluhisha.

Urusi imekuwa ikumuunga mkono Rais wa Syria, Bashar al-Assad huku Marekani ikiunga mkono makundi ya waasi nchini humo. Ni zaidi ya miaka 10 sasa vita bado vimepamba moto na Syria imebaki kuwa gofu, hakuna usalama, shughuli za kimaendeleo zimekwama na raia wake wamegeuka kuwa wakimbizi.

Nchini Iraq hali nayo siyo shwari tangu uvamizi wa Marekani nchini humo mwaka 2003 uliomuondoa madarakani aliyekuwa Rais wa Iraq Saddam Hussein, aliyehukumiwa hukumu ya kunyongwa hadi kufa. Uwepo wa vita na migogoro nchini Iraq umepelekea kuzorota kwa uchumi wa taifa hilo na maisha ya watu yameharibika, taifa la Marekani linanyooshewa kidole juu ya hili kutokana na uvamizi wake nchini Iraq miaka 21 iliyopita.

Hivi sasa jumuiya za kimataifa na ulimwengu kwa ujumla umeelekeza macho yao kwa taifa la Ukraine na Urusi ambao wamekuwa kwenye mvutano wa muda mrefu, na sasa wapo kwenye vita.

Vita kati ya Ukraine na Urusi vilianza mnamo Februari 24, 2022, pindi Urusi ilipoanzisha uvamizi wa kijeshi dhidi ya Ukraine.

Vita Ukraine na Urusi vimeleta madhara makubwa, ikiwa ni pamoja na vifo vya maelfu ya watu, uharibifu mkubwa wa miundombinu, na mamilioni ya raia kutoka pande zote mbili kulazimika kukimbia makazi yao.

Uchumi wa dunia pia umeathirika kutokana na vita hivi. Mfano, kuongezeka kwa bei ya nishati na chakula ukizingatia Ukraine ilikuwa inategemewa kwa sehemu kubwa na nchi za Afrika kwa ngano.

Madhara makubwa ya kibinadamu yameikumba Ukraine, huku pia ikisababisha vikwazo vya kimataifa dhidi ya Urusi, jambo linalochochea mgawanyiko wa kisiasa duniani.

Tukiwa tunazungumzia masuala ya mivutano baina ya mataifa makubwa ulimwenguni ni vigumu kuacha kutaja taifa la Marekani na Korea Kaskazini. Mataifa haya yamekuwa na mvutano hasa wakati wa utawala wa aliyekuwa Rais wa Marekani, Donald Trump.

Mvutano ulishika kasi zaidi kutokana na masuala ya uzalishaji na majaribio ya silaha za nyuklia yaliyokuwa yakifanywa na Korea Kaskazini chini ya Rais Kim Jong-Un. Marekani kupitia Umoja wa Mataifa (UN) ulifanikiwa kuiwekea vikwazo Korea Kaskazini ili kusitisha mpango wake wa silaha za nyuklia ambao ulikuwa unatishia amani ulimwenguni.

Hali ya amani barani Afrika

Nchi za Afrika kama zilivyo nchi zingine kwenye mabara mengine, kuna nchi zina amani na nyingine ipo lakini ya kusuasua huku baadhi ikiwa haipo kabisa.

Barani Afrika tuna Umoja wa Africa (AU) ambao umelenga kuimarisha mshikamano na ushirikiano baina ya nchi za Afrika, bila kusahau suala la amani.

Licha ya juhudi za Baraza la Usalama na Amani la Umoja wa Afrika lenye malengo ya kuzuia, kudhibiti na kutatua migogoro barani Afrika lakini bado hali ya amani katika mataifa ya Afrika ni kitendawili, mfano hai kuhusu hilo ni Somalia ambapo sehemu kuwa ya viongozi wa nchi hiyo hawaishi Somalia.

Migogoro ya kisiasa, vita vya wenyewe kwa wenyewe, rushwa na mengine mengi yameathiri hali ya amani na kuwaacha wananchi kuteseka, kuwa wakimbizi na baya zaidi ni maendeleo katika nchi hizo yanasonga kwa mwendo wa kinyonga.

Katika taifa la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tunashuhudia migogoro kila kukicha, watu wamepoteza maisha huku wengine wakilazimika kuyakimbia makazi yao. Ni miongo sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo suala la amani bado ni kitendawili.

Katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kumekuwa na mvutano na vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo pia vimechochewa na udini. Mfano, waasi wa kundi la kikristo la Anti Balaka katika taifa hilo walishutumiwa kusababisha mauaji ya watu wa dini nyingine.

Mchambuzi Hamduny Marcel, anasema ulegevu wa Umoja wa Afrika ndiyo chanzo cha umoja huu kushindwa kufikia malengo ya kuleta amani kwenye nchi zenye migogoro Afrika.

“Umoja wa Afrika unazo nguvu ila zisizokidhi haja na matakwa halisi ya nguvu zinazotakiwa ili kujenga amani ya Afrika.” Ameeleza Hamduny.

Juhudi mbalimbali zimekuwa zikifanywa na mataifa ya Afrika katika suala zima la utunzaji wa amani. Operesheni za kurejesha na kuimarisha amani zinazoendeshwa na Umoja wa Afrika nchini Somalia zinaonekana kudorora, kundi la Al Shabab likibaki kuwa jinamizi kwa nchi hiyo. Je, Umoja wa Afrika unafanya kazi yake ipasavyo katika kuimarisha amani?

Mchambuzi wa siasa Juma Mudimi, anautazama Umoja wa Afrika kama umbwa asiyeng’ata kutokana na kushindwa kufanya kazi zake ipasavyo.

“Umoja wa Afrika ni mbwa asiyeuma kwa sababu imekosa vyombo vya ambavyo vingeweza kusimamia vizuri, lakini pia kumekuwa na uingilio mkubwa wa shughuli za Umoja wa Afrika na mataifa kadhaa ya magharibi.” Amedokeza Mudimi.

Hali ya amani nchini Tanzania

Kwa mujibu wa ripoti ya Taasisi ya Amani na Uchumi duniani ya mwaka 2024, Tanzania inashika nafasi ya 65 kwa amani duniani huku katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara Afrika, ikishikilia nafasi ya 7.

Picha: Imesanifiwa na Dominic Allen kwa msaada wa ChatGPT.

Hali hii ya amani imechagiza kwa wawekezaji kuja kuwekeza nchini, kwa mujibu wa ripoti ya Kituo cha Uwekezaji (TIC) nchini kwa mwaka wa fedha 2023/24, TIC ilisajili miradi 707, ikiwa ni ongezeko kubwa la asilimia 91.60 ikilinganishwa na miradi 369 ya mwaka wa fedha 2022/23.

Kwetu kama taifa ni neema, swali ni: Je, ni kwa namna gani tumepanga kuimarisha na kuitunza amani tuliyonayo?

Juhudi za kulinda amani nchini Tanzania zilionekana baada ya kusaini na kupitisha Mikataba ya Kimataifa yenye lengo la kulinda amani.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoridhia Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupinga Matumizi ya Silaha za Nyuklia wa mwaka 1968. Mkataba huu unalenga kuzuia usambazaji wa silaha za nyuklia na kusaidia juhudi za kimataifa za kulinda amani kwa kuondoa tishio la silaha hizo.

Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupiga Vita Biashara Haramu ya Silaha Ndogo na Nyepesi wa mwaka 2001, pia Tanzania imeupitisha. Lengo kuu la mkataba huu ni kudhibiti biashara haramu ya silaha ndogo na nyepesi ambazo mara nyingi hutumika katika migogoro na kuleta machafuko.

“Tanzania imekuwa ikijinasibu kuwa ni kisiwa cha amani lakini hali iliyopo kwa sasa kidogo inatishia siwezi kusema ni amani bali inatishia uhuru. Hali ilyopo kwa sasa haitishii sana amani bali inatishia uhuru wa mtu mmoja mmoja” Ameeleza Mudimi.

Kama ilivyoainishwa awali ya kuwa amani huandaa mazingira ya maendeleo katika nchi, na amani huonekana kwa vitendo namna ambavyo uongozi wa nchi husika na mamlaka zake unavyoongoza watu wao pamoja na ushirikiano na mataifa ya nje.

Ijapokuwa ripoti ya Taasisi ya Amani na Uchumi duniani imeonesha kuwa tupo nafasi ya 7 kwa kuwa na amani kwa upande wa nchi zilizopo Kusini wa Jangwa Sahara, lakini tunapaswa kujiuliza kwa haya yanayoendelea ya mauaji na utekaji wa raia hapa nchini yanaathiri vipi tunu yetu ya amani.

Katika makala zilizowahi kuchapishwa na Land Dwellers, kuna makala yenye kichwa cha “Utekaji: Fumbo linalotushinda?” ambayo ilizungumzia kwa kina suala la kushamiri kwa matukio ya utekaji na mauaji yanayoendelea nchini Tanzania.

Katika baadhi ya matukio haya kwa namna moja au nyingine vyombo vya usalama hasa Jeshi la Polisi limeonekana kunyooshewa kidole.

Mauaji ya hivi karibuni ya Mjumbe wa Sekretarieti ya CHADEMA Taifa na Msaidizi wa Katibu Mkuu, Mzee Ally Kibao yamezua hisia kali kwa wale wote wanaopenda haki na kuthamini utu wa mtu.

Leonce Sarwat ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu CHADEMA (CHASO) Dar es Salaam, anasema kuwa hali ya amani nchini ni tete kutokana na kushamiri kwa matukio haya.

“Kwa namna moja au nyingine hali ya hewa (amani) kwa sasa ni mbaya sana, ndiyo maana hata polisi hatuwaamini tunatembea watu wawili wawili.” Amesema Leonce.

Leonce anaeleza ni vigumu kwa wananchi kuwa na maendeleo kama sakata hili la mauaji na utekaji halitatatuliwa.

“Hakuna maendeleo kama hakuna amani. Kama mtu wangu wa karibu ametekwa au amepotezwa akili yangu itawaza kumtafuta huyo mtu, nitafanyaje vitu vya maendeleo? Sidhani kama kutakuwa na maendeleo.” Maoni ya Leonce.

Juma Mudimi anaiona hatari kama suala la utekaji na mauaji ya raia lisipopatiwa dawa ya kudumu.

“Kuchelewa kuonekana kwa majibu au kuonekana kwa watu ambao wamefanya vitendo hivyo, kwa kiasi kikubwa kunatishia amani ya taifa.” Ameeleza Mudimi.

Ni zaidi ya mwezi sasa tangu kutekwa kwa mwanaharakati na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA), Jimbo la Temeke, Deusdedith Soka na wenzake wawili na hadi leo hawajulikani ni wapi walipo.

Soka na wenzake waliotekwa siku moja ni miongoni mwa wengine wengi waliokumbwa na madhila haya, jambo lililowafanya viongozi na wanachama kwa ujumla kuitisha maandamano ya amani Septemba 23, 2024, endapo Soka na wengine waliotekwa hawatapatikana.

Kufanya maandamano ni haki ambayo ipo kikatiba chini ya ibara ya 20 ya Katiba ya Tanzania. Kila mwananchi ana haki ya kufanya maandamano pasipo kuvunja sheria za nchi.

Katika hali iliyowashtua watu wengi hasa wanaharakati na wanasiasa wa vyama vya upinzani, ni pale Jeshi la Polisi lilipofanya onesho la maigizo ya askari wa kutuliza ghasia (FFU) na wananchi. Igizo hili lilifanyika mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Miaka 60 ya Jeshi la Polisi Tanzania.

Hii iliibua hisia tofauti ikizingatiwa kuwa CHADEMA ilishatangaza kufanya maandamano ambayo Jeshi la Polisi iliyapiga marufuku kwa kigezo kuwa yanaingilia uchunguzi ambao unaendelea kuhusiana na matukio ya mauaji na utekaji nchini Tanzania.

Licha ya katazo hilo kutoka kwa Jeshi la Polisi Tanzania, viongozi na wanachama wa CHADEMA wameonesha dhamira ya kuwa ni lazima wafanye maandamano hayo.

Tanzania imeridhia Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa mwaka 1966 ambao unalinda haki za kiraia na kisiasa za watu wote, pamoja na haki ya kuishi kwa amani, usalama na haki za msingi. Vyombo vya ulinzi na usalama vinapaswa kupitia upya juu ya utendaji wao wa kazi kwa maslahi ya umma.

Aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na Jaji Mstaafu Tanzania, Joseph Warioba anaona kuwa kukosekana kwa kuongea lugha moja kati vyombo vya ulinzi na usalama na vyama vya siasa hasa upinzani ndiyo chanzo cha mvutano ambao kwa namna moja au nyingine una matokeo hasi.

“Chama kinasema kitakuwa na maandamano, Polisi wanasema hakuna maandamano. Unajiuliza, utaratibu upo (haki ya kuandamana). Lakini kila mmoja anatoa uamuzi wake, kwa nini wasingeshauriana?” Amesema Mzee Joseph Warioba.

Tanzania inapaswa kujifunza kutoka mataifa kama Somalia, ambayo walilivunja bakuli la amani na hadi leo wanaunganisha vipande kuirejesha amani.

Ni wazi kuwa kuvurugika kwa amani kunaathiri moja kwa moja maisha ya kila mwananchi hasa wazee, wamama na watoto.

Amani ikivurugika utendaji kazi utashuka, wengine wataishia ukimbizini huku mazingira ya uwekezaji ya kudorora. Ni hakika hakuna anayetaka taifa letu lifikie hatua hiyo.

Litupasalo kufanya ili kuilinda tunu ya amani

Kulinda amani ni jukumu la kila mmoja wetu, na ili kufanikisha hili kuna hatua na mikakati mbalimbali inayoweza kuchukuliwa.

Kwanza, serikali inapaswa kuhakikisha kuna haki na usawa kwa raia wote bila kujali kabila, dini, jinsia au hali ya kiuchumi.

Pili, serikali inapaswa kufanya shughuli zake kwa uwazi na uwajibikaji ikiwa ni pamoja na kudhibiti rushwa na upendeleo.

Tatu, serikali na wadau wa maendeleo wanapaswa kuweka mikakati ya kupunguza umasikini, kama vile kutoa fursa za ajira kwa wananchi, kwa sababu kukosekana kwa ajira kumekuwa ni moja ya vyanzo vya machafuko.

Nne, wananchi wanapaswa kujifunza kuhusu haki zao na jinsi ya kuzilinda, pamoja na kuhamasisha utatuzi wa migogoro kwa njia za kisheria badala ya kutumia ghasia au kulipiza kisasi.

Nne, kujenga mahusiano bora katika jamii, ikiwa ni pamoja na kuelimisha jamii kuhusu tofauti za kidini, kikabila, na kitamaduni. Hii itasaidia watu kukubali tofauti zao na kuheshimu maoni ya wengine.

Tunapaswa kutambua kuwa bila amani juhudi za maendeleo zitakwama, kwani migogoro, ghasia, na uvunjifu wa sheria huwa ni kikwazo kufikia malengo ambayo kama taifa mmejiwekea.

Amani inatoa mazingira salama na thabiti kwa serikali, wananchi, na mashirika mbalimbali kushirikiana katika kuleta mabadiliko chanya na maendeleo endelevu.

Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway

Hot this week

CHADEMA kutoa msimamo wake kuhusu maridhiano

By Veronica Mlyatu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa...

Mnyonge, mnyongeni ila haki yake mpeni

By Dorlingson Edward Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), leo...

Popular Articles

Safari ya Mashimba katika kutetea jamii ya Wahadzabe

Nchini Tanzania  kuna jumla ya makabila zaidi ya 120...

Polisi waendelea kuwashikilia viongozi wa CHADEMA

Ni siku ya kwanza tangu kukamatwa kwa viongozi wa...

Siku ya Vijana Duniani.

Kwa sasa ni kijana wa miaka 25 ambaye amejiajiri...

BWAWA LA ARBA’AT  LASABABISHA MAAFA NCHINI SUDAN

Watu 30 mashariki mwa Sudan na na wengine 60...

Sand Mining in Tanzania: Trails of Destruction in Lake Victoria and its Environs

By Dominic Allen On November 14th, 2021 in the Geita...

 Utekaji: Fumbo linalotushinda?

Na Yohani Gwangway Taifa la Tanzania kwa miaka mingi limekuwa...

Abduction: Is it a riddle we can’t solve?

By Yohani Gwangway For many years Tanzania has been an...

Mustakabali wa Hewa Safi kwa kila kiumbe

Na Dominic Allen Msingi wa maisha ya viumbe hai yaani...
LAND DWELLERS FACT CHECK HUB VERIFY FACTS STOP MISINFORMATION Trusted Fact-Checking in Tanzania Beyond What You Know VERIFY NOW

Related Articles

Popular Categories

DWELLERS CHECK-HUB Verify Facts. Stop Misinformation Trusted Fact-Checking in Tanzania • Beyond What You Know VERIFY NOW