Na Dr. Bravious Kahyoza
Tanzania imejitokeza na kuwa kielelezo cha kupambana na rushwa barani Afrika, ikipata mafanikio ya kipekee yanayostahili kupewa kongole. Katika ripoti ya hivi karibuni iliyotolewa na Shirika la Transparency International ya Corruption Perceptions Index (CPI) ya mwaka 2024, Tanzania imepanda katika orodha katika udhibiti wa rushwa, ambapo imeshika nafasi ya pili katika nchi za Afrika Mashariki na ya 14 barani Afrika.

Mafanikio katika suala la udhibiti wa rushwa hapa nchini hayakuja bila juhudi za makusudi na mikakati madhubuti ambayo Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa ikitekeleza chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Maendeleo haya ni matunda ya juhudi za pamoja za taasisi mbalimbali za Serikali, ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na sekta nyingine za umma. Mapambano haya hayakuwa rahisi, lakini kwa uthabiti na nia ya kweli ya kubadilisha mazingira ya kisiasa na kiuchumi, Tanzania imeweza kuonyesha mwelekeo mzuri.
Nafasi ya Tanzania katika ripoti za Transparency International
Katika ripoti hiyo ya Shirika la Transparency International, Tanzania imepata alama 40 kati ya 100, ikiwekwa katika nafasi ya 87 kati ya nchi 180 duniani zilizohusishwa katika ripoti.
Haya ni maendeleo makubwa ikilinganishwa na alama ya 38 iliyopatikana mwaka 2023, ambapo Tanzania ilikuwa katika nafasi ya 94 duniani, ambapo katika ripoti ya mwaka 2024, imeongeza alama mbili na kupanda kwa nafasi saba katika kipindi cha mwaka mwaka mmoja tu.
Katika ukanda wa Afrika Mashariki, Tanzania inashika nafasi ya pili baada ya Rwanda, ambayo ilipata alama 53 na kushika nafasi ya 49 duniani. Hii inamaanisha kuwa Tanzania imepiga hatua za maana katika kuboresha uwazi na utawala bora, na kuwa kielelezo kwa nchi nyingine za kanda.
Ikilinganishwa na nchi kama Uganda ikiwa na alama 26 na kushika nafasi ya 141, huku Kenya ikipata alama 31 na kushika nafasi ya 126).
Maendeleo ya Tanzania katika kupambana na rushwa yamezidi kupiga hatua chanya, mnamo mwaka 2020, Tanzania ilikuwa na alama 38 katika ripoti ya CPI, na mwaka 2021 alama ziliongezeka hadi 39, huku miaka ya 2022 na 2023 alama zilishuka hadi 38, lakini mwaka 2024 imepanda hadi kufikia alama 40.

Maendeleo haya yanaonesha kuwa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani ipo kwenye mwelekeo sahihi katika kupambana na rushwa, na juhudi zake zimeendelea kuzaa matunda.
Juhudi za kimkakati za Serikali katika kupambana na rushwa
Katika Ripoti ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ya mwaka 2020, baadhi ya Taasisi za Serikali zilitajwa kuwa vinara kwa vitendo vya rushwa, ambapo Jeshi la Polisi Tanzania lilishika nafasi ya kwanza kwa kuwa na asilimia 45.6, Taasisi za Afya zikishika nafasi ya pili kwa rushwa kwa kuwa na asilimia 17.9, Mahakama ikishika nafasi ya tatu kwa asilimia 11.9, huku nafasi ya nne ikishikwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuwa na asilimia 6.1.
Mara baada ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani, Tanzania imeonekana kupiga hatua katika udhibiti wa rushwa, hatua hizi zimetokana na mikakati ambayo Serikali imekuwa ikitekeleza.
Moja ya mafanikio makubwa ni kurejesha fedha zilizoporwa ambazo zinafikia Shilingi bilioni 211.95, jambo ambalo linaonyesha uthabiti wa taasisi za kisheria katika kufuatilia na kurejesha mali za umma.
Huu ni ushahidi wa uwezo wa mifumo ya kisheria ya nchi katika kupambana na rushwa. Zaidi ya hilo, Serikali imetaifisha mali zenye thamani ya Shilingi za Kitanzania bilioni 35.688, ikiwa ni pamoja na nyumba, magari na fedha taslimu.
Hatua hizi zilizochukuliwa na Serikali zinaonyesha kuwa hakuna aliye juu ya sheria, ambapo Taasisi za Serikali zimezidi kuimarisha mifumo ya uwajibikaji na uwazi.
Ushirikiano wa kimataifa na utawala bora
Tanzania imeendelea kuimarisha ushirikiano wake kimataifa katika kupambana na rushwa, kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa (UN) na Umoja wa Afrika (AU) katika kuboresha utawala bora, ambapo ushirikiano huu umehusisha kubadilishana uzoefu, mafunzo na kuweka mifumo ya kimataifa ya kufuatilia na kupambana na rushwa.
Kwa kushirikiana na mashirika ya kimataifa, Tanzania imeweza kupata msaada wa kiufundi na kifedha ambao umechangia kuimarisha uwezo wa taasisi za kupambana na rushwa, na kusaidia katika kuboresha sheria za kimataifa za kupambana na rushwa pamoja na kuweka mazingira ya kushirikiana na nchi nyingine katika kufuatilia mali zilizoporwa.
Changamoto katika mapambano dhidi ya Rushwa
Rushwa katika sekta za umma, kama vile afya, elimu na miundombinu, bado inasalia kuwa tatizo linaloathiri huduma za msingi kwa wananchi nchini Tanzania. Baadhi ya watu ambao wanaojihusisha na rushwa hawawajishwi kutokana na mapungufu katika mifumo ya kisheria na utekelezaji wa sheria.
Uwajibikaji wa maafisa wa umma na uwazi katika michakato ya manunuzi ya umma bado unahitaji kuimarishwa. Kunahitajika mifumo imara ambayo itaweza kuhakikisha kuwa michakato yote ya Serikali inafanywa kwa uwazi na uwajibikaji. Aidha, kujenga uwezo kwa taasisi za kufuatilia na kuhakikisha kuwa sheria zinatekelezwa kwa ufanisi.
Tanzania bila rushwa inawezekana
Ni ndoto ya kila mwananchi anaelitakia heri Tanzania, kuwa na Taifa lisilo na chembe ya rushwa ndani yake, ambapo ili kufikia malengo hayo, ni muhimu kuendelea kuimarisha mifumo ya utawala bora, kukuza uwazi katika sekta za umma na kujenga uwezo wa taasisi za kisheria.
Kwa kuendeleza juhudi hizi za makusudi na kukuza ushirikiano wa kimataifa, Tanzania ina nafasi ya kufikia viwango vya juu zaidi vya uwazi na kuwa kielelezo kwa nchi nyingine Afrika na duniani kwa ujumla.
Mapambano dhidi ya rushwa ni safari ndefu ambayo inahitaji uthabiti, ushirikiano pamoja na kujitolea kwa malengo ya muda mrefu. Lakini kwa misingi imara iliyopo sasa chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Tanzania ina nafasi kubwa ya kutokomeza rushwa.
Mwandishi: Dr. Bravious Kahyoza
Mhariri: Dominic Allen


