Na Dominic Allen
Mkutano wa pamoja kati ya Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliyohusu kutafuta suluhisho juu ya mgogoro nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) umehitimishwa hii leo jijini Dar es Salaam, ambapo mambo kadhaa yameafikiwa katika mkutano huo.
Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya kumalizika kwa mkutano huo uliyofanyika kwa siku mbili, EAC na SADC zimesema kuwa zimewaagiza Wakuu wa Ulinzi kutoka nchi wanachama kukutana ndani ya siku tano na kuja na mwelekeo juu ya namna kusitisha mapigano mara moja na kumaliza uhasama unaoendelea Mashariki mwa DRC kati ya kundi la waasi wa M23 na serikali ya nchi hiyo.
EAC na SADC pia imewataka Wakuu wa Ulinzi kuangalia jinsi ya kutoa msaada wa kibinadamu ikiwemo kuwazika waliopoteza maisha na kuwaondoa waliyojeruhiwa.
Jumuiya hizo zimekubaliana kuimarishwa kwa hali ya usalama katika mji wa Goma, ambapo hadi sasa bado unashikiliwa na kundi la waasi wa M23.
Mbali na hayo, zimetaka kufunguliwa kwa njia kuu, ikiwemo njia ya Goma – Sake – Bukavu; Goma – Kibumba – Rumangabo pamoja na njia nyingine.
Wakuu wa Ulinzi pia wametakiwa kuhakikisha uwanja wa ndege Goma unafaunguliwa tena, baada ya kufungwa kufuatia uvamizi wa M23.
Hata hivyo, hali ya kiutu na usalama nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) bado ni tete, huku taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Umoja wa Mataifa (UN) ikisema kuwa takriban watu 3,000 wameuawa katika mji wa Goma tangu kundi la waasi wa M23 liudhibiti mji huo.
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


