Na Yohani Gwangway.
Kushika kasi kwa matumizi ya mifuko ya plastiki jijini Mwanza imekuwa ni kidonda kinachohitaji tabibu wa haraka ili kiweze kupona. Kama tulivyoona katika sehemu ya kwanza na ya pili kuna sababu kadhaa zinazosababisha kuendelea kwa matumizi ya mifuko hii licha ya uwepo wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 pamoja na Kanuni za Usimamizi wa Mazingira za kupiga Marufuku Mifuko ya Plastiki za mwaka 2019.
Katika sehemu hii ya tatu, tunaenda kuangazia juu ya nini kifanyike ili kuondokana na tatizo la uwepo wa matumizi ya mifuko ya plastiki yenye madhara makubwa kwenye mazingira, viumbe wa ardhini na majini, uchumi na afya kwa binadamu.
Kutokana na madhara makubwa ambayo yalianishwa katika sehemu ya kwanza ya makala hii kwenye mazingira, viumbe, uchumi na kwa binadamu, baadhi ya wakazi wa jiji la Mwanza wanasema ili kutokomeza matumizi ya mifuko ya plastiki, serikali inapaswa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara yanayotokana na matumizi ya mifuko hiyo.
“Hapa suala kubwa ni wenyewe (maafisa mazingira) wakitoka mbele wakaanza kuongelea, wakapita hapa mtaani kutoa elimu ili watu waelewe madhara ya hii mifuko ya plastiki, nadhani itasaidia sana. Itakuwa ni chachu ya watu kuacha matumizi ya mifuko hii”. Anasema Rajabu ambaye ni mkazi wa Mwanza.
Kitendo cha serikali kutoa elimu kutawafungua macho wananchi maana wao ndiyo watumiaji wa mwisho wa mifuko ya plastiki, ambapo madhara kama ya kiafya kwa namna moja au nyingine yanawalenga moja kwa moja.
Baadhi wa wananchi wanaona kuwa elimu peke yake haitoshi. Wananchi wanaona kuwa serikali na mamlaka zinazohusika zinatakiwa kuzuia mifuko isiendelee kuzalishwa. Hoja hii ni kuwa wananchi wanatumia mifuko hii kwa sababu tayari iko mitaani, lakini kama ikizuiwa kuanzia kwenye chanzo basi ni rahisi kuzuia tatizo.
“Mimi ushauri wangu kwanza, naomba serikali ianzie kuzuia kule mifuko inapoingilia kwa maana ya mipakani. Wakishazuia kule mifuko haiwezi kuingia nchini kwetu. Na kama haiingii nchini maana yake ni kuwa haiwezi kutumika. Kwa hiyo kitu kikubwa ni kuzuia sehemu inapoingilia”. Maoni ya Lilian John kuhusu kuzuia mifuko ya plastiki.
Kukosekana kwa uwajibikaji kwa baadhi ya maofisa wa usimamizi wa mazingira kuanzia ngazi ya Jiji, Kata, Mtaa/Kijiji hadi Kitongoji kumetajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazopelekea uwepo wa matumizi ya mifuko ya plastiki hapa jijini Mwanza, hivyo maofisa hawa wanapaswa kujifunga mkanda na kutekeleza majukumu yao kikamilifu kama Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 inavyoelekeza.
“Ushauri ni kwamba wanatakiwa watutembelee hasa huku vijijini na pia wanatakiwa wawepo maafisa ili kuweza kuhimiza kuhusu hii mifuko kama ina changamoto, maana hata mimi mwenyewe sijui kama ina changamoto. Kwa hiyo ninashauri watutembelee na watoe elimu ili tujue kama hii mifuko ina changamoto”. Anashauri Sarah Wilson William, mkazi wa Nyamagana jijini Mwanza.
Katika mnyororo wa hatua za uzalishaji wa mifuko ya plastiki kwenye sehemu ya kwanza ya makala tumeona kuwa hatua ya kwanza huanzia viwandani ambapo mifuko ya plastiki huzalishwa, baadhi ya wataalamu wanashauri kuwa serikali inatakiwa ichukue hatua mahususi za kufanya msako kuvibaini na kuvifunga viwanda vyote vya mifuko ya plastiki nchini na kuhakikisha kuwa hakuna uzalishaji, vilevile kuzuia mifuko inayoingia nchini Tanzania kutoka nchi jirani kama vile Uganda.
“Kwanza kinachotakiwa ni kudhibiti kwenye chanzo. Kwa sisi wataalamu wa afya huwezi tu kutibu ugonjwa bila kuangalia chanzo cha ugonjwa. Ili kudhibiti ugonjwa unatakiwa ujue chanzo. Hivyo basi niombe serikali, hii mifuko tunaiona ipo kwenye jamii, lakini kuna wazalishaji, kwa sababu kuna mianya ambayo hii mifuko inapita. Kwa hiyo ikidhibitiwa isiingie na vile viwanda vya nje vinavyotengeneza hii mifuko vikazuiwa, tutakuwa tumedhibiti.” Ushauri wa Audiphace Sabbo, Afisa Afya Jiji la Mwanza.
Ripoti ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), yenye jina, ‘Kufunga Bomba: Jinsi ulimwengu unavyoweza kukomesha uchafuzi utokanao na plastiki na kuunda uchumi wa mzunguko’ iliyotolewa Mei 16, 2023 imesema kuwa ili kupamba na tatizo la uchafuzi wa plastiki ikiwemo mifuko ya plastiki, tunapaswa kuwekeza katika uchumi wa mzunguko.
Ripoti hii inasisitiza kutengeneza soko la bidhaa ambazo zinaweza kutumika zaidi ya mara moja na kuondokana na uchumi wa uzalishaji wa bidhaa za plastiki ambazo zinatumika mara moja na kisha kutupwa.
Kwa mujibu wa ripoti hii, kitendo cha kuwa mifumo ya kutumia bidhaa zinazotumika zaidi ya mara moja itachangia pakubwa zaidi katika kupunguza uchafuzi utokanao na plastiki kwa asilimia 30 ifikapo mwaka 2040, kwani itachukua nafasi ya baadhi ya bidhaa za plastiki zinazotumika mara moja.
Eneo jingine ambalo ripoti hii ya UNEP imetilia mkazo ni kutengeza soko imara la urejelezaji wa plastiki kwa kuhakikisha kuwa shughuli/kazi ya urejelezaji inakuwa ni yenye faida. Kwa kufanya hivyo kunaweza kupunguza uchafuzi wa plastiki kwa asilimia 20 zaidi ifikapo mwaka 2040. UNEP inasema katika kufanikisha hili kunahitajika upatikanaji wa kutosha wa malighafi inayoweza kurejelezwa na kuhakikisha kuwa bidhaa zilizorejelezwa zinaweza kushindana kwa usawa na bidhaa zilizotokana na malighafi mpya.

Katika jarida la Umoja wa Mataifa (UN), la Septemba, 2019 lenye jina ‘Teknolojia za Kisasa kwa Kukabiliana na Uchafuzi wa Plastiki’ linasema kuwa miongoni mwa njia za kupambana na uchafuzi utokanao na plastiki ni kutafuta mbadala wa bidhaa zote za plastiki, na kutukumbusha kuwa kabla ya enzi ya plastiki, bidhaa za asili zilitumika kukidhi mahitaji mengi ambayo kwa sasa yanatimizwa na plastiki hivyo basi kutafuta mbadala wa plastiki ni jambo linalowezekana kwa kugeukia mbadala ambao ni bidhaa za asili.
UN imesema kuwa mbadala huu ni rahisi kutekelezeka na hauhitaji teknolojia mpya, kwa mfano; inawezekana kurudi kwenye matumizi ya mifuko ya vitambaa kwa ajili ya kubebea bidhaa dukani, sokoni n.k, au matumizi ya majani ya migomba kufunga na kusafirisha chakula, bila kuwa na hitaji kubwa la ubunifu wa kiteknolojia.
Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, Kifungu cha 39, kinasema kuwa Halmashauri ya Wilaya itamteua Ofisa wa umma kwa ajili usimamizi wa mazingira wa mji, kata, kijiji, mtaa na kitongoji.
Licha ya kuwepo maofisa hawa wenye jukumu la kuratibu kazi zote na shughuli zinazolenga kuhifadhi mazingira kwenye maeneo yao husika, bado matumizi ya mifuko ya plastiki ni tatizo jijini Mwanza na Tanzania kwa ujumla.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mazingira lisilo la Kiserikali, Lawyers’ Environmental Action Team (LEAT), Wakili Dkt. Rugemeleza Nshala anasema kuwa mbali na maofisa hawa kuwajibishwa na viongozi wa ngazi za juu kama vile wakuu wa mikoa na wilaya, pia wananchi wanao wajibu wa kuwawajibisha maofisa hawa pindi wanaposhindwa kutekeleza majukumu yao.
“Kwa sehemu kubwa wananchi wanajukumu kubwa la kuwawajibisha maafisa watendaji wa serikali, kwa sababu serikali inawajibika kwa wananchi kwa hiyo kuna jukumu kwa kila mwananchi kuwawajibisha hawa watu (viongozi)”. Amesema Dkt. Nshala.
Kifungu namba 41 cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, kinazungumzia juu ya madaraka ya jumla ya Kamati za usimamizi wa mazingira za jiji, manispaa, wilaya, mji, kata, kijiji, mtaa na kitongoji.
Miongoni mwa madaraka ya Kamati hizi ni kuanzisha uchunguzi na upelelezi kuhusu tuhuma yoyote inayohusu mazingira, lakini licha ya jukumu hilo bado kuna matumizi ya mifuko ya plastiki ambayo tayari ilishapigwa marufuku.
Dkt. Nshala anaona kutotengwa kwa fedha za kutosha kwa Kamati za Usimamizi wa Mazingira hupelekea kupwaya katika utendaji wao wa kazi.
“Kutokuwepo kwa rasilimali fedha na kutokuwepo na mfumo ambao unahakikisha hizo Kamati zinakuwa na rasilimali ambazo wamepewa, kufanya kazi kwao kunakuwa ni kama kufanya kazi ya ziada au nyongeza”. Dkt. Nshala.
Mbobezi huyu kwenye masuala yanayohusu mazingira amesema kuwa kwa mataifa ambayo yamefanikiwa katika upigaji marufuku wa matumizi ya mifuko ya plastiki inayotumika kwa mara moja na kutupwa, kama vile Canada na baadhi ya nchi za Afrika kama Rwanda huwa yanaweka fedha za kutosha ili kuhakikisha sheria na kanuni zinazotungwa zinasimamiwa ipasavyo.
“Wanatenga rasilimali fedha za kuhahakikisha sheria inapotungwa, siyo inatungwa tu lakini na fedha ya kuhakikisha kuwa sheria hizo zinafuatwa na kutekelezwa zinatengwa. Kwa hiyo lazima kuwe na fedha za kutosha, ni makosa kwa Bunge kupitisha sheria bila kuweka fedha ambazo zitaweza kuhahakikisha hizo sheria zinatekelezwa.” Amesema Dkt. Nshala.
Dkt. Nshala amesema ili kutoka hapa tulipo tunapaswa kupitia upya sheria zetu lakini pia kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu masuala yahusuyo mazingira ili kudai uwajibikaji kwa viongozi wao.
“Kwa sehemu kubwa tunatakiwa tubadilishe sheria zetu ili watu wanaohusika (viongozi wa usimamizi wa mazingira) wawe ni watu ambao wameajiriwa moja kwa moja kufanya hizo kazi, kuongeza uelewa wa wananchi pamoja na uwepo wa Kamati hizo na viongozi mbalimbali wa mazingira lazima ufahamike, na wananchi waweze kudai kuwajibika kwao.” Ameshauri Dkt. Nshala.
Tunaona kuwa ili kukomesha matumizi ya mifuko ya plastiki, suala la uwajibikaji halipo tu kwa viongozi bali linaanzia chini kabisa katika ngazi ya mtu binafsi kwa kuelewa madhara ya mifuko hiyo, kuelewa na kuitekeleza sheria na kanuni za usimamizi wa mazingira na pia kuwa balozi wa mazingira kwa kila mwananchi.
“Hapa suala ni uwajibikaji wa mtu mmoja mmoja, yaani mimi pale nyumbani kwangu natunzaje mazingira, yule nyumbani kwake anatunzaje mazingira na yule nyumbani kwake anatunzaje mazingira. Na hakuna kitu kigumu kufanyia usafi kama mifuko ya plastiki. Suala hapa ni wajibikaji, huko masokoni sisi tulishapita tumetoa semina , hakuna mkuu wa soko ambaye hajui kinachotokea. Lakini je, mkuu wa soko akifika sokoni kazi yake ya kwanza muhimu anayohimiza ni ipi? Maokoto au utunzaji wa mazingira?” Meneja wa NEMC Kanda ya Ziwa Victoria.
Pia kwa maoni ya wananchi, viongozi wa usimamizi wa mazingira kuanzia ngazi ya viongozi wa vitongoji hadi Waziri mwenye dhamana wanapaswa kusimamia ipasavyo majukumu yao kama sheria na kanuni za usimamizi wa mazingira zinavyoelekeza.
Ili kulinda mazingira, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Usafi wa Mazingira Jiji la Mwanza, Desderius Polle anahimiza wananchi kuacha kuchafua mazingira kwani madhara ya matendo haya yanarudi kwao kwa sababu watahitaji kuishi katika mazingira hayo hayo yaliyochafuka.
“Kutupa taka ya mifuko, kutupa taka ya aina yoyote ndani ya vyanzo vya maji au popote, hiyo ni dhambi na ni kosa. Kwa hiyo wananchi wajue kuwa wanafanya hivyo lakini haya madhara hayaendi kwenye maji. Yanarudi kwetu, kwa sababu unapochafua chanzo cha maji au chakula, baadaye tunatumia sisi wenyewe. Hivyo wajue kuwa kila tunachofanya kina madhara kwetu wenyewe.” Anashauri Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Usafi wa Mazingira Jiji la Mwanza, Desderius Polle.
Jiji la Mwanza ni miongoni mwa majiji yenye idadi kubwa ya watu. Sensa ya mwisho ya mwaka 2022 ilionesha Mkoa wa Mwanza ambapo jiji hili linapatikana una zaidi ya watu milioni 5. Upekee mwingine ni kuwa Jiji hili limepakana na Ziwa Victoria ambalo linategemewa kwa upatikanaji wa samaki. Jambo hili linamaanisha uchafuzi wa mazingira ukiwemo utupaji wa mifuko unaenda kuathiri mamilioni ya watu na mazalia ya samaki.
Suala hili linamfanya Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Usafi wa Mazingira Jiji la Mwanza, Desderius Polle kuomba wananchi wote washirikiane na mamalaka za mazingira ikiwemo ofisi ya Jiji kutoa taarifa za watu wanaozalisha, wanaohifadhi ya kutumia mifuko ya plastiki.
“Mifuko hii imekuwa ikionekana katika baadhi ya maeneo hasa katika maeneo ya kukusanyia taka, kwenye mifereji. Hivyo tunaendelea kudhibiti. Inaonekana inaingia kwa njia ambayo siyo rasmi. Hivyo ni wajibu tu kwa sisi watenda kazi, lakini ni wajibu wa kila mwananchi mmoja mmoja kuhakikisha wanatoa ushirikiano wa kutoa taarifa ya wapi mifuko inaingilia, wapi inapatikana, na ni nani anauza ili tuweze kuipata na kuikamata na kuiteketeza. Na ikiwezekana kumjua nani mzalishaji na nani mwingizaji wa mifuko hii”. Polle akiomba ushirikiano wa wananchi.
Kwa sasa dunia inapambana na uzalishaji wa hewa ambazo zinaharibu Ozoni ambapo uzalishaji wa hewa hizo unatokana pia na matumizi ya plastiki hasa wakati wa kuchoma. Mwaka 2015 katika Mkutano wa Mabadiliko ya Tabia ya Nchi yaani COP21 uliofanyika Paris, Ufaransa, Tanzania iliwasilisha “Michango iliyopangwa kitaifa“ yaani Intended Nationally Determined Contributions (INDCs) ikiwa na ahadi ya kupunguza uzalishaji wa hewa chafu (greenhouse gas emission). Mkutano huu ulitoka na azimio la Paris, yaani Paris Agreement ambapo wakuu wa nchi walikubaliana mambo mbalimbali katika kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi.
“Tanzania itapunguza uzalishaji wa hewa chafu zinazotokana na shughuli za uchumi kwa asilimia 10 hadi 20 ifikapo mwaka 2030 kuendana na Ripoti ya kila baada ya miaka 2 (Bennial Update Report-BUR), kulinagana na uboreshaji wa ufanisi wa msingi, sambamba na ajenda yake ya maendeleo endelevu. Upunguzaji wa hewa chafu utakaguliwa baada ya ripoti ya kwanza ya kila baada ya miaka miwili yaani Biennial Update Report (BUR).
Hali inayooenekana katika Jiji la Mwanza na baadhi ya maeneo mengine nchini Tanzania hasa katika matumizi ya mifuko ya plastiki, inaenda kinyume na kusudio hili na kuleta maswali mengi. Je, kama Taifa tuko makini katika kusukuma ajenda ya mabadiliko ya tabia ya nchi? Na kwa kiasi gani tunawajibika kufikia malengo yaliyowekwa katika ajenda hii? Maswali haya na mengine mengi yanahitaji majibu ya kiuwajibikaji kwa viongozi, mamlaka, taasisi na idara zinazohusika kulinda mazingira na kutekeleza sheria zilizopo.

Mwandishi: Yohani Gwangway
Mhariri: Dominic Allen


