Kama nitakutana na Rais Samia leo.

Na Julius Laitayok

Nikiwa ni Mtanzania na mzawa wa Ngorongoro, kwa niaba ya wananchi wa Ngorongoro, mkoani Arusha, huu ni Waraka wangu kwako Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

1. Baraza la Wafugaji lirudishwe mikononi mwa jamii na liachwe liwe la jamii kwa sababu chombo hicho kiliundwa kwa lengo la kuhudumia jamii ya kifugaji.

2. Miradi ya jamii itekelezwe na huduma za kijamii zirudishwe na zitekelezwe na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa kushirikiana na Halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro na Serikali za vijiji ndani ya tarafa ya Ngorongoro.

3. Uhuru wa matumizi ya ardhi Ngorongoro urudishwe kama ilivyokuwa awali (maeneo ya malisho). Nyanda za malisho zinapaswa ziwe huru kwa sababu wanyama wote ni sawa.

4. Jukumu la tatu la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) litekelezwe kama Sheria za Mamlaka zinavyoelekeza, ‘Uendelezaji wa wenyeji kupitia Baraza La Wafugaji na ufadhili wa miradi ya maendeleo’. NCAA kwa miaka hivi ya karibu wamejikita kuendeleza jamii za jirani na kuacha kutoa huduma kwa wenyeji kama takwa la kisheria linavyoelekeza.

5. Serikali na jamii zishirikiane kwa pamoja tuwe na ufugaji wenye tija kwa kubadilisha mfumo wetu wa ufugaji kwa kufufua Ranchi ya Ngairish.

6. Mahusiano mazuri ya jamii na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) ndiyo njia pekee ya kuhakikisha maendeleo endelevu katika Hifadhi ya Ngorongoro.

7. Kuwe na ushirikishwaji wa jamii katika Uhifadhi na Utalii kama ilivyokuwa awali.

8. Vibali vya miradi ya maendeleo ya jamii visitumiwe tena na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kama fimbo ya kuumiza jamii wakati mahoteli na kempu za watalii zinajengwa kwa mamia ndani ya eneo la hifadhi asubuhi na jioni.

9. Serikali na jamii kumtafuta Afisa mmoja (Community Relation Officer), ambaye ni mwenyeji atakayesaidia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Jamii kuishi pamoja kwa kuendeleza mahusiano bora.

10. Idara za Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) za Mahusiano ya Umma, Intelijensia na Maendeleo ya jamii zote zifumuliwe, kwa sababu zimechangia kwa kiasi kikubwa kuharibika kwa uhusiano na jamii, kutesa, kunyanyasa, na kupotosha Umma juu ya hali halisi na kutengeneza propaganda kupitia vyombo vya Umma, Habari na Mitandao ya kijamii kwa lengo la kufanikisha nia yao ovu ya kuwaondoa wenyeji ndani ya eneo la Ngorongoro.

11. Bodi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Menejimenti zote zivunjwe kisha ziundwe upya na nafasi 3 zipewe wenyeji kama ilivyokuwa mwanzo wa uanzishwaji wa hii hifadhi. Bodi imekuwa ikiamua nini kifanyike kwa mamlaka bila kupata maoni na ushauri kutoka kwa wenyeji ambao maamuzi hayo yanaathiri sana maisha yao.

12. Uwekezaji wa kila kitu uwe shirikishi. Kumekuwepo na uwekezaji usioshirikishi kwenye maeneo ya vijiji hasa kwenye maeneo ya malisho, mapito ya wanyama na vyanzo vya maji ambao unafanywa na NCAA bila kuwashirikisha na kupata baraka kwenye ngazi za vijiji jambo ambalo linaleta migogoro na athari kubwa kwa wananchi na wanyama wafugwao pamoja na wanyama pori hasa kwenye ikolojia.

13. Viongozi na wafanyakazi wa NCAA waliyoipotosha serikali na kuipitisha jamii kwenye mwavuli wa mauti watafutwe na wawajibishwe ikiwa ni pamoja na kufikishwa Mahakamani kwa matumizi mabaya ya madaraka.

14. Dhana ya Ardhi Mseto (Multiple Land Use Model) kuwa imeshindikana siyo kweli, ni kwa sababu imekuwa ikiendeshwa na wale wenye nia mbaya na jamii, wenye maslahi binafsi ili kupotosha Umma na Jumuiya za Kimataifa pamoja na Mashirika ya Uhifadhi. Dhana ya Ardhi Mseto haijashindikana japo inahitaji maboresho iweze kuongeza tija kwa kushirikiana pande zote ikiwemo jamii na NCAA pamoja na serikali.

15. Pia nafasi zote za ajira hasa kwenye Usimamizi, Ukurugenzi hadi ya Mhifadhi mkuu zote zipewe kipaumbale kwa wenyeji.

16. Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa sasa inaendeshwa bila kuwa na Mpango wa Uendeshaji na Usimamizi (GENERAL MANAGEMENT PLAN – GMP) ya kusimamia eneo lote la hifadhi. Hivyo wadau wote washirikishwe, hasa kwa kuzingatia mawazo na ushauri wa wenyeji.

17. Idara ya Uwekezaji na Mipango iondolewe kabisa kwenye muundo wa NCAA kwa sababu imeshindwa kushauri Bodi kuhusu dhana ya uwekezaji.

18. Nyanda za malisho zinapaswa ziwe huru kwa sababu wanyama wote ni sawa.

19. Kuingia na kutoka kwa wazawa katika Lango la Oloduare imekuwa changamoto kubwa hadi kwa watu/wagonjwa mahututi.

20. Katika suala la uhamisho wa wananchi kuelekea Msomera mkoani Tanga, kipaumbele kimewekwa zaidi wale wanaohama kuliko wanaoendelea kubaki. Siyo kila mtu atahama Ngorongoro, kwa hiyo utaratibu wa kuhamisha wanaohama uwe rafiki ili kunusuru maslahi ya wananchi wanaobaki katika Hifadhi ya Ngorongoro.

21. Uboreshaji wa miundombinu umekuwa hafifu sana, hii imechangia umaskini kuenea kwa kasi kwa jamii katika kipindi hiki cha miaka minne (4). Hivyo uboreshaji na ujenzi ufanyike kwenye miundombinu kama vile barabara kwenye ngazi za vitongoji na sehemu za huduma muhimu kama shule na hospitali.

22. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan afanye ziara katika eneo la Ngorongoro na kukutana na jamii moja kwa moja na siyo wawakilishi.

23. Tathmini ifanyike kubaini mafanikio na madhara yaliyotokana na uhamisho wa watu Msomera, mkoani Tanga.

24. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan unapaswa kuheshimu Jamii za Asili, mawazo na ushauri wetu kama wadau muhimu na wa kwanza kabisa kwenye uhifadhi Ngorongoro.

25. Kuondokana na aina ya uhifadhi unaotumia mabavu (Fortress Conservation) na kuwa na uhifadhi wa jamii jumuishi katika maamuzi yenye kuheshimu haki za binadamu na utu.

26. Sheria za nchi kutambua watu wa Jamii za Asili na kuheshimu tamaduni zao na haki za binadamu. Serikali ikubali uasili wa wenyeji wa watu wa Ngorongoro kwa utamaduni wao na mtindo wa maisha ili kuondoa dhana mbaya ambayo imejijengea kwenye sura wa kimataifa ya kukana uwepo wa watu wa Jamii za Asili Tanzania.

27. Wenyeji wa Ngorongoro wapewe gawio la mapato yatokanayo na uhifadhi kama malipo yao kwa kushiriki kwenye uhifadhi kwa kujinyima mengi (Ecosystem payments), moja kwa moja na iwe ni 30% ya makusanyo yote ya fedha za utalii.

28. Watu wawe huru katika maeneo ya huduma (shopping centres) na wawe na haki ya kujenga makazi ya kudumu isipokuwa katika maeneo ya malisho yaani mifugo na wanyama, lakini maboma ya muda yaruhusiwe huko kwenye malisho kipindi cha kiangazi (Ronjoi).

29. Maeneo yote ya kiimani/ hija (Alamal), shughuli za kitamaduni (Engipaata), dawa (Irpuli) na madini joto yawe huru kwa jamii na mifugo, kwa mfano; Crater, Empakaai, Olmoti na mengine.

30. Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), ijenge miundombinu ya maji katika maeneo yenye ukame ya malisho hasa sehemu ambayo wafugaji wanachimba visima vya asili vya chini (Iltilal/Ilchororoi) na mabwawa ili kupunguza msongamano wa mifugo kwenye maeneo machache, pia kama sehemu ya utunzaji wa mazingira.

31. NCAA ijikite kwenye uhifadhi wenye tija na endelevu kwa;

i. Kutatua changamoto ya mimea vamizi.

ii. Kutoa elimu ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira kwa wenyeji badala ya matumizi ya nguvu.

iii. Kupunguza msongamano wa magari kwenye maeneo ya vivutio kama vile Crater na Ndutu.

iv. Kuanzisha miradi ya kijamii yenye lengo la kupambana na mabadiliko ya Tabia nchi, kwa mfano upandaji wa miti ya asili kupitia wenyeji kwenye maeneo ya mbugani.

v. Kuwa na Mabalozi wa uhifadhi katika ngazi za vitongoji ili jamii ishiriki kikamilifu kwenye masuala ya ulinzi.

Hitimisho: Ifahamike kuwa sisi wana Ngorongoro hatupingi kabisa umuhimu wa utalii na mapato yake, shida yetu ni kama kutuondoa Ngorongoro ndiyo njia pekee ya kuongeza pato la nchi, basi ni kinyume na haki za binadamu na hatuamini kama huu ni msimamo wa serikali yako.

Mtoa maoni: Julius Laitayok, kwa niaba ya wananchi wa Ngorongoro.

Mhariri: Yohani Gwangway & Dominic Allen

Hot this week

CHADEMA kutoa msimamo wake kuhusu maridhiano

By Veronica Mlyatu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa...

Mnyonge, mnyongeni ila haki yake mpeni

By Dorlingson Edward Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), leo...

Popular Articles

Safari ya Mashimba katika kutetea jamii ya Wahadzabe

Nchini Tanzania  kuna jumla ya makabila zaidi ya 120...

Polisi waendelea kuwashikilia viongozi wa CHADEMA

Ni siku ya kwanza tangu kukamatwa kwa viongozi wa...

Siku ya Vijana Duniani.

Kwa sasa ni kijana wa miaka 25 ambaye amejiajiri...

BWAWA LA ARBA’AT  LASABABISHA MAAFA NCHINI SUDAN

Watu 30 mashariki mwa Sudan na na wengine 60...

Sand Mining in Tanzania: Trails of Destruction in Lake Victoria and its Environs

By Dominic Allen On November 14th, 2021 in the Geita...

 Utekaji: Fumbo linalotushinda?

Na Yohani Gwangway Taifa la Tanzania kwa miaka mingi limekuwa...

Abduction: Is it a riddle we can’t solve?

By Yohani Gwangway For many years Tanzania has been an...

Mustakabali wa Hewa Safi kwa kila kiumbe

Na Dominic Allen Msingi wa maisha ya viumbe hai yaani...
LAND DWELLERS FACT CHECK HUB VERIFY FACTS STOP MISINFORMATION Trusted Fact-Checking in Tanzania Beyond What You Know VERIFY NOW

Related Articles

Popular Categories

DWELLERS CHECK-HUB Verify Facts. Stop Misinformation Trusted Fact-Checking in Tanzania • Beyond What You Know VERIFY NOW