Salaam kwako Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni matumaini yangu kuwa ni buheri wa afya njema.
Ninaomba muda wako mchache kusoma barua yangu ya wazi kwako kwa manufaa ya jamii yangu na ustawi wao, ikiwa wewe ni kiongozi wao wa nchi na kwamba unaweza kuamuru kutenda haki kwa manufaa ya watu wa jamii ya watanzania unaowaongoza au unaweza kuamuru kuondosha ustawi wao kwa kuwawekea vikwazo vya maendeleo kwa malengo yenye maslahi na watu wachache wenye nguvu na wanaotumia dhamana walizonazo kujilimbikizia mali na utajiri mkubwa na kuwaacha wananchi wakiwa maskini wa kutupwa.
UTANGULIZI
Mhe Rais, utakumbuka vyema jamii ya watu wa Ngorongoro na Loliondo wanapitia kipindi kigumu sana kutokana na serikali kuchukua maeneo yao. Takriban siku 16 tokea umeapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia kifo cha Hayati John Pombe Magufuli, ulisema hadharani kwamba Arusha ni Utalii, na Utalii ni Ngorongoro na kisha baadaye ukaenda mbali zaidi kwamba watu wanaoishi Ngorongoro hasa eneo la Ardhi Mseto ya Mamlaka ya Ngorongoro siyo lazima watu waishi mahali hapo na kwamba wanaweza kutafuta maeneo mengine nje ya hifadhi, watu wakaenda kuishi huko ili wapishe uhifadhi.
Mhe. Rais mara baada ya kauli yako uliyoitoa Arusha , Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) ilitoa Notisi ya siku 90 kuvunjwa kwa makanisa, ofisi za vijiji, shule, vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na majengo mengine ya kudumu.
Hata hivyo baadae serikali ilianzisha zoezi la kuwahamisha wakazi wanaoishi kwenye hifadhi ya Ngorongoro kuwapeleka Msomera, Tanga (uhamisho uliyokuwa na kiini macho cha uhiyari kwenda Msomera).
Mara baada ya kuanza zoezi hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Ngorongoro aliandika barua kwenda kwa walimu wakuu shule za msingi na sekondari, vituo vya afya, watendaji wa vijiji na kata kuwataka wahamishe fedha za miradi ya maendeleo zilizokuwa katika akaunti zao na zitumwe kwenda akaunti ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Tanga ambapo kazi hiyo ilifanyika ndani ya wiki moja.
Mhe. Rais vikwazo vya kimaendeleo vimewekwa kwa jamii yetu ili kutengeneza mazingira magumu yatakayofanya jamii yetu kuhama kwenda Msomera, Tanga.
Mhe. Rais, kwa tarafa za Sale na Loliondo watu wetu waliporwa maeneo yao kwa mabavu na kwamba hata maeneo kidogo waliyobakiwa nayo kuna hati hati yakachukuliwa.
MAONI YETU NA MAPENDEKEZO YETU
- Mhe. Rais ikiwa unayo nia thabiti ya kutafuta ufumbuzi wa kudumu katika mgogoro huu uliyosababishwa na serikali basi ufanye kikao cha wazi na wananchi wote wa Ngorongoro huko Ngorongoro na siyo watu wachache ambao ni wanasiasa na hasa wa chama chako.
- Zoezi la uhamisho wa Msomera halina uhiyari wowote, ni pia mnaongeza mgorogoro mwingine kwa kuchukua ardhi ya wazawa wa Msomera na hili litathibitika ukitoa vikosi vya ulinzi huko, wananchi watadai haki zao.
- Tunaomba urejeshe huduma za jamii kwa vitendo, kwa sababu hadi sasa hakuna huduma iliyorejeshwa, na ili kuthibitisha nia thabiti, fedha za miradi ya maendeleo zilizohamishwa zirejeshwe na uwafukuze waliyoratibu zoezi hilo.
- Mhe. Rais tunaomba urejeshe ukarabati kwa vitendo wa miundombinu yote ya shule, vituo vya kutolea huduma za afya, ofisi za vijiji na barabara.
- Mhe. Rais, tunaomba urejesha Baraza la Wafugaji na wapatiwe Gawio toshelezi kulingana na mapato makubwa wanayopata NCAA, warejeshewe ofisi yao Ngorongoro na siyo Halmashauri na vitendea kazi vyote muhimu kwa ajili ya kazi zao.
- Tunaomba suala uboreshaji wa mifugo kwa kurejesha Ranchi ya Ngairish.
- Mhe. Rais, uwekezaji unaoendelea Ngorongoro wa ujenzi wa hoteli zenye hadhi za kimataifa ni uchafuzi mwingine kwa ikolojia na uhifadhi, ni kujidanganya kuwaondoa wamasai kwa kujinasibu kuendeleza uhifadhi ambao kwao ni utamaduni wao.
- Bodi ya Mamlaka ya Ngorongoro ivunjwe na nusu ya wajumbe wote iwe ni wanajamii wazawa na isiwe Wakuu wa vyombo vya majeshi wanaostaafu.
- Wenyeji wapewe kipaumbele kutegemeana na nafasi za ajira zitakazotangazwa na NCAA.
- Mhe. Rais, uhifadhi, utalii na ikolojia usiendeshwe kwa mfumo wa kijeshi na kwamba mfumo huu hauna kesho iliyo bora zaidi ni uporaji kwa maslahi ya watu wachache.
- Mh Rais mfumo wa uendeshwaji na usimamizi wa uhifadhi, utalii uwe baina ya jamii na serikali. Kwa maana hiyo jamii iwepo katika nafasi za maamuzi na si kama ilivyo sasa.
- Tunaomba sana turuhusiwe kwenda majumbani mwetu muda wowote, pia vyombo vya wenyeji wasilipishwe kiingilio kila siku.
- Tunaomba eneo la kilomita za mraba 1,500 kwa tarafa ya Sale na Loliondo lirejeshwe kwa wananchi, na mpango wowote wa kutaka kuchukua maeneo yao machache waliyobakiwa nayo usitishwe.
- Ikiwa Mhe Rais Samia Suluhu Hassan, kama unafanya hili kwa manufaa ya kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 pasipo kuwa na nia dhati ya kumaliza mgogoro ni bora usifanye hivyo, tunatambua ni kwa kiasi gani tumeumizwa na sasa hatuko tena tayari kuumizwa.
- Mhe. Rais, Wana-CCM ambao unatarajia kukutana nao hawatakuambia ukweli kwa sababu ya nafasi zao za kisiasa, tunaomba sana uende kwa wananchi.
Ukifanikiwa kusuluhisha hili kwa kuzingatia maslahi ya wananchi unaowaongoza, utakua umejijengea sifa na heshima kubwa.
Tunaomba Taasisi za Kimataifa ziwe macho kufuatilia mgogoro huu.
Natanguliza shukrani zangu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Baba Loma
Mkazi wa Ngorongoro


