
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuondoka leo, Novemba 10, 2026, nchini Tanzania kuelekea mjini Antalya, Uturuki, kushiriki Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP31).

Mkutano huo ulianza jana, Novemba 9, 2026, ukiwa na ajenda mbalimbali zinazohusu mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo afya, usalama wa chakula na kilimo.
Katika ziara hiyo, Rais Samia pia anatarajiwa kufanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdoğan, kuhusu masuala mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano kati ya mataifa hayo.
Mkutano huo, unawakutanisha viongozi mbalimbali wa serikali, wanadiplomasia, wataalamu wa mazingira, wanasayansi na mashirika ya kiraia ili kujadili changamoto mbalimbali zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi duniani, pamoja na kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana na athari zake.
COP ni mkutano wa kila mwaka unaofanyika chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC), ulioanzishwa mwaka 1992. Huu ni mkutano wa 31 tangu kuanzishwa kwa jukwaa hilo, ambalo limekuwa sehemu muhimu ya majadiliano ya kimataifa kuhusu kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi, kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuweka mikakati ya ufadhili wa miradi ya kukabiliana na changamoto hizo.

