Wakazi wanne wa Ngorongoro, wakiwemo wafanyakazi watatu wa Shirika la Pastoral Women’s Council (PWC), wameachiwa jana usiku baada ya kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa zaidi ya saa 24 katika Kituo Kikuu cha Polisi Arusha, ambapo walioachiwa ni Thadeus Clamian, Nangei Meitaya, Ezekiel Kishau pamoja na Salangat Makko.
Wakili John Lairumbe, amesema wateja wake wameachiwa majira ya saa tatu usiku bila kufunguliwa mashtaka, huku akieleza kuwa katika ufuatiliaji wa suala hilo hawakuweza kubaini kosa mahususi walilokuwa wakituhumiwa nalo. Amesema awali polisi walieleza kuwa walikuwa wakimtafuta mtu anayetajwa kwa jina la Naishorwa na waliomba ushirikiano katika kumpata, lakini juhudi hizo hazikufanikiwa.
Lairumbe amesema baada ya kuendelea kufuatilia suala hilo, mawakili walifika kituoni na kuonana na mpelelezi wa shauri hilo, ambaye awali hakutoa majibu ya kina na kuwaelekeza katika ofisi nyingine. Baadaye walipewa maelezo kuhusu kumtafuta Naishorwa, huku ikidaiwa kuwa Lobulu Tome, aliyekuwa pamoja na waliokamatwa katika Hospitali ya Selian, alikuwa na mawasiliano na mtu huyo.
Akizungumzia hali ya wateja wake baada ya kuachiwa, Lairumbe amesema kwa mujibu wa maelezo yao hakukuwa na tukio la uvunjifu wa haki za binadamu wakati wote waliokuwa wakishikiliwa. Hata hivyo, amesema changamoto kubwa ilikuwa kutopata fursa ya kuwasiliana na wakili wao kwa wakati, huku yeye mwenyewe akisema alikumbana na ugumu wa kuonana na kuzungumza na wateja wake wakati akifuatilia suala hilo kituoni.
Lairumbe amesema suala lililoibua changamoto kubwa zaidi katika tukio hilo ni kuzuiwa kwa mawasiliano kati ya mawakili na wateja wao, jambo alilodai liliathiri utoaji wa huduma ya kisheria. Hadi walipoachiwa jana usiku, amesema mawakili walikuwa bado hawajafahamishwa kwa uwazi kosa mahususi ambalo wateja wao walikuwa wanatuhumiwa nalo.
Wakazi hao walikamatwa na Jeshi la Polisi tarehe 6 Oktoba 2026 katika eneo la Hospitali ya Selian jijini Arusha, baada ya kufika hospitalini hapo kwa lengo la kumtembelea na kumsalimia Siwuo Tome.
Picha: Global Publishers


