Na Dominic Allen
“Hawa ni sehemu ya watoto wa jamii, na ulemavu siyo kikwazo, ulemavu ni sehemu ya aina ya uwezo tofauti, na jamii yetu lazima itambue uwezo wa aina tofauti,”
Ni sauti ya msisitizo ya Makumba Mwemezi, Mkuu wa idara ya utafiti, ubunifu na uchambuzi wa sera kutoka shirika la HakiElimu, akieleza jinsi watoto wenye ulemavu ambavyo wanapaswa kupata haki ya elimu bora nchini Tanzania.
Baada ya kubainisha mizizi ya tatizo na mianya ya uwajibikaji iliyosababisha miundombinu isiyo rafiki kwa watoto wenye ulemavu kuendelea kuwepo mashuleni, swali halibaki tena nani ana wajibu, bali nini kifanyike ili kubadili hali halisi. Katika sehemu tatu, makala hii inaelekeza mjadala juu ya suluhisho, ikitazama hatua za kisera, kiutawala na kijamii zinazoweza kuchukuliwa ili kuhakikisha haki ya elimu jumuishi kwa watoto wenye ulemavu kwenye shule za msingi na sekondari katika mkoa wa Mwanza, ambapo makala itamulika namna ambavyo serikali, kamati za shule na jamii kwa ujumla pamoja na wadau wa elimu nchini Tanzania wanavyoweza kuwajibika katika nafasi zao.
Miongoni mwa mambo yaliyoibuliwa ni pamoja fedha zinazotumia kurekebisha miundombinu ikiwemo madawati, kutowazingatia inavyotakiwa wanafunzi wenye ulemavu, “Serikali ikitoa pesa inabidi iangalie pande zote, watu wenye mahitaji maalum na wengine. Mfano, wakitoa pesa za madawati, inatakiwa waangalie je, lile dawati litamfaa mwenye ulemavu?” Joasen Julius, mkazi wa Bulale, kata ya Buhongwa jijini Mwanza, mwenye ulemavu wa miguu na kuzungumza akishauri serikali juu ya hilo.
Suala la uwazi na uwajibikaji limesisitizwa na baadhi ya wananchi, ili kuhakikisha fedha zinazotengwa kwa ajili ukarabati wa miundombinu katika shule za msingi na sekondari na masuala mengine zinatumika ipasavyo na kuwanufaisha walengwa wote.
Magege Hailala Magege, mkazi wa kata ya Nyamanoro, Ilemela, ambaye pia ni Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ametilia mkazo suala la uwazi kwenye matumizi ya fedha hizo zinazotengwa.
“Fedha zinazotengwa kwa ajili ya watoto wenye ulemavu ziwe kwenye uwazi, kwa sababu kwa sasa hatujui ni kiasi gani, hatujui wanamuhudumia nani, kwa sababu hata kwenye kata niliyopo hatujui kuna idadi ya watoto wenye uhitaji wangapi,” amezungumza Magege.
Hata hivyo, Magege ameeleza kuwa katika mkoa wa Mwanza, suala la kutoa elimu kwa jamii kuhusu mahitaji ya watoto wenye ulemavu, halikwepeki, kwani baadhi ya wananchi wamekuwa na ushiriki duni katika kuhakikisha watoto wenye ulemavu nao wanapata haki sawa ya elimu kama ilivyo kwa watoto wengine.
“Jamii yetu inahitaji elimu, kitu cha kwanza ni elimu kwenye kila mkutano wa mtaa papatikane elimu… Hawa ambao wapo kwenye kundi maalum bila kujua haki zao au mahitaji yao au haki zao ni zipi, mtu anashindwa aanzie wapi kuwasaidia,” ameshauri Magege.
Prisca Mbise, mwalimu wa Shule ya sekondari Kabuhororo ameishauri serikali kuendelea kuboresha miundombinu ili kuwapa fursa watoto wenye ulemavu kupata elimu bora sawa na watoto wengine.
“Serikali iendelee kuboresha mazingira, miundombinu, madarasa wazingatie ili wale wenye mahitaji maalum pia waweze kuyatumia yale madarasa. Kama ni vyoo, yaani waguse kila eneo, waajiri pia zaidi watu wenye taaluma za watu wenye mahitaji maalum,” ameshauri Mbise.
Kwa upande wake, Julius ameiomba serikali iwaangalie kwa jicho la tofauti wanafunzi wenye mahitaji maalum katika shule za msingi na sekondari mkoani Mwanza, kwani wengi wenye ulemavu hukumbana na changamoto zaidi za kimaisha pindi wanapokosa elimu.
“Kwa niaba ya wenzangu wenye ulemavu waliopo shuleni naomba serikali iwaangalie sana, kwa sababu mtu mwenye ulemavu akishindwa kusoma akirudi mtaani ni changamoto,” amesema Julius, mwenye ulemavu wa miguu na kuzungumza.
Robert Kahema, Mwenyekiti wa kitongoji cha Mwasonge A, wilaya ya Misungungwi mkoani Mwanza, ameiomba serikali kuongeza juhudi za kuboresha miundombinu katika shule za msingi na sekondari, ili ziweze kutoa elimu juimuishi iliyo bora.
“Serikali izidi kutanua wigo wake na kuendelea kuboresha zaidi miundombinu ya madarasa. Kwa mfano Shule ya sekondari Mwasonge bado mapungufu yapo, japo ni madogo” ameleeza Kahema.

Diwani wa kata ya Nyamanoro kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kange, ametoa wito kwa wazazi wenye watoto wenye ulemavu kuwa mstari wa mbele kuwapeleka watoto wao shuleni ili wapatiwe elimu itakayowasaidia katika maisha yao ya sasa na baadae.
“Mimi niwatie moyo huo huo walionao (wazazi) waweze kujitoa au kuwatoa watoto kwenda kupata elimu, kwa sababu faida na msingi wa maisha ya mtoto ni elimu. Kwa maana hiyo usipompa mtoto elimu maana yake umefungia kwenye boksi, unapomfungulia mtoto na akapata elimu, umefungulia kuona mwanga ambao unaweza kuwa ni msaada wake katika maisha yake,” wito wa Diwani Kange kwa wazazi wenye watoto wenye ulemavu.
Mbarala Maharagande, Katibu wa Idara ya Haki za Binadamu na Vyombo vya Uwakilishi wa Wananchi, ACT Wazalendo Taifa, amesema katika kutatua changamoto hii, ni wajibu wa wazazi pamoja na wadau katika eneo husika kuweka mikakati ya muda mfupi na mrefu.
“Kuweka mikakati ya muda mfupi na mrefu katika maeneo yao, kwa sababu wakati mwingine shule hizo zinakuwa na mapato, ruzuku kutoka serikalini na halmashauri, kwa hiyo ni vizuri kuweza kufanya au kubuni mikakati ya muda mfupi ya kutatua changamoto hizo, mfano kama shule inakuwa haina ngazi ya kusukuma baiskeli za watoto wenye ulemavu, haihitaji mabilioni, ni jambo tu la wadau wa eneo husika kupitia kipato ambacho kipo katika shule yao wakalitekeleza hilo,” maoni ya Maharagande.
Maharagande, pia ameishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuweka mikakati ya muda mrefu, kama vile kutazama upya suala la bajeti kwa watu wenye ulemavu, ikiwemo wanafunzi katika shule za msingi na sekondari.
“Moja, serikali kuweka bajeti inayotosheleza. Pili, katika kila miundombinu mpya inayojengwa katika shule mpya na zinazokarabatiwa, ni kuhakikisha kwamba kunakuwa na miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu,” ushauri wa Maharagande.
Abdulrahman Lugone, Mweka Hazina mstaafu wa Shirikisho la Vyama vya Walemavu Tanzania (SHIVYAWATA), amesisitiza kuwa ili kuondoka na tatizo hilo la miundombinu isiyo rafiki kwenye shule kwa watoto wenye ulemavu, ni wakati sahihi sasa kusukuma utekelezaji wa sera na sheria husika zinazowagusa watu wenye ulemavu.
“Ni utekelezaji wa sheria, sheria inasema hivi kwamba halmashauri zote ziwe na bodi za huduma kwa watu wenye ulemavu. Sasa, mpaka sasa utakuta ni halmashauri za miji mikuu kama Majiji ndiyo ambayo yana hizo bodi. Hazijaundwa hizo bodi kwenye ngazi za halmashauri au sehemu za vijiji za kata…Kwa hiyo cha msingi ni turudi kwenye sheria na sera, kusukuma ziweze kutekelezwa ili huduma kwa watoto wenye ulemavu ziweze kupatikana,” amesisitiza Lugone.
Ili kuwanusuru watoto wenye ulemavu na magonjwa yanayosabishwa na kutumia vyoo visivyo rafiki kwao, Joyce Lukumay, mtaalam wa masuala ya afya, ameshauri watoto hawa kujengewa vyoo maalum shuleni, ambavyo vinakidhi mahitaji yao.
“Waandaliwe hivi vyoo vya kukaa, hivi vyoo vya kukaa inakuwa ni rahisi, kwa sababu anapokwenda na zile baiskeli zao (Wheelchair), akifika pale (chooni), ananyanyuliwa anakalishwa kwenye choo cha kukaa,” ameshauri Lukumay.
Shirika la HakiElimu linaona kuwa kama jamii tunapaswa kukumbushana wajibu wetu pamoja na kushirikishana, ili kuondokana na jinamizi na miundombinu mibovu linalozikumba shule za msingi na sekondari hapa nchini.
“Hatua za haraka ni kukumbushana wajibu wetu na kushirikishana, serikali kuwashirikisha wadau, wananchi, kuhakikisha wale watoto mahususi wanapatiwa mahitaji ambayo wanayahitaji,” amezungumza Makumba Mwemezi, Mkuu wa idara ya utafiti, ubunifu na uchambuzi wa sera kutoka shirika la HakiElimu.
“Hatua ya muda mrefu, ni kuwekeza, hatuna njia fupi ni lazima watu wawekeze. Kuhakisha kwamba bajeti zinazotengwa zinaweza kutoka kuhakikisha kwamba miundombinu inakuwepo na inakidhi vigezo. Lakini vilevile kuwa na uendelevu, kuhakikisha kwamba miundombinu hiyo ambayo imejengwa inaweza kuwahudumia wote na inakuwa ni ya muda mrefu,” maoni ya Mwemezi.
Kwa ujumla, changamoto ya miundombinu isiyo rafiki kwa watoto wenye ulemavu katika shule za msingi na sekondari mkoani Mwanza ni pengo kubwa kati ya sera, sheria na utekelezaji wake. Wakati haki ya elimu jumuishi ikitamkwa wazi katika katiba, sera na sheria mbalimbali za nchi, hali halisi shuleni inaonesha kuwa uwajibikaji bado ni dhaifu katika ngazi za maamuzi, utekelezaji pamoja na ufuatiliaji, matokeo yake watoto wenye ulemavu wanakosa haki ya kupata elimu bora.
Hata hivyo, mabadiliko yanawezekana endapo uwajibikaji utawekwa mbele kama nguzo ya maendeleo ya elimu nchini Tanzania. Serikali, halmashauri, viongozi wa serikali za mitaa, kamati za shule, wadau wa elimu pamoja na jamii kwa ujumla wanapaswa kuona elimu jumuishi si hisani, bali ni haki inayodai utekelezaji wa makusudi.
Kila darasa linalojengwa, kila choo kinachokarabatiwa na kila shilingi ya umma inayotumika, vinapaswa kuzingatia mahitaji ya watoto wenye ulemavu. Bila kufanya hivyo, mfumo wa elimu utaendelea kuwatenga, badala ya kuwaandaa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii.
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


