Na Dominic Allen
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron amesema kuzuka kwa vita kati ya Marekani, Israel na Iran kuna madhara makubwa kwa amani na usalama wa kimataifa, ambapo Ufaransa inachukua kila hatua kuhakikisha usalama wa mipaka yake, raia wake pamoja na maslahi yake Mashariki ya Kati.
Macron kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X, ameonya kuwa kuongezeka kwa mivutano kunahatarisha usalama wa kila upande na kwamba hali hiyo lazima isitishwe mara moja, huku akiitaka Iran kushiriki kwa nia njema katika mazungumzo ya kumaliza programu zake za nyuklia na makombora ya balistiki, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu kwa usalama wa Mashariki ya Kati.
Aidha, amesema wananchi wa Iran wanapaswa kuruhusiwa kwa uhuru kujenga mustakabali wao, akidai kuwa vitendo vya ukandamizaji vinapunguza uhalali wa utawala wa sasa. Kutokana na hali hiyo, Ufaransa imetangaza kuitisha mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, huku Macron akieleza kuwa yuko katika mawasiliano ya karibu na washirika wa Ulaya na Mashariki ya Kati kutafuta suluhisho la kidiplomasia.
Mapema hii leo baada ya mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel dhidi ya maeneo mbalimbali ndani ya Iran, ikiwemo mji mkuu wa Tehran, Iran pia imeripotiwa kufyatua makombora kuelekea kambi za kijeshi za Marekani zilizoko katika mataifa kadhaa kama Qatar, Kuwait, Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


