Na Dr. Bravious Kahyoza
Tanzania sasa imepiga hatua za kihistoria katika kuimarisha miundombinu ya mawasiliano hasa kupitia ujenzi wa minara ya mawasiliano, chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Rais Samia wakati akihitimisha Shughuli za Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Juni 27, 2025 alibainisha kuwa katika kipindi cha uongozi wake, minara 8,524 ya mawasiliano imejengwa, ikiongeza jumla ya minara nchini kutoka 754 mwaka 2020 hadi 9,278 kufikia Juni 2025.
Mafanikio haya yamewezesha upatikanaji wa mawasiliano katika maeneo yenye changamoto na kukuza uchumi wa kidijitali kupitia biashara mtandao na mawasiliano bora.

Changamoto za miundombinu ya mawasiliano kabla ya 2021
Tangu uhuru wa Tanzania mwaka 1961 hadi 2020, nchi ilikuwa imejenga minara ya mawasiliano 754 tu katika kipindi cha miaka 59. Idadi hii ndogo ilizua changamoto kubwa za upatikanaji wa mawasiliano, hasa katika maeneo ya vijijini na yenye changamoto za kijiografia.
Hali hiyo ilizuia maendeleo ya biashara za mtandao, huduma za simu na upatikanaji wa habari, hasa kwa jamii za vijijini ambazo hazikuwa na huduma za mtandao wa simu au intaneti. Pengo hili la kidijitali lilizuia fursa za kiuchumi na kuongeza tofauti kati ya jamii za mijini na vijijini katika upatikanaji wa huduma za kisasa.
Mapinduzi ya miundombinu ya mawasiliano chini ya Rais Samia
Ujenzi wa minara 8,524 ya mawasiliano na kufanya jumla ya minara nchini kufikia 9,278 mwaka 2025, inadhihirisha wazi juhudi za kimkakati za Serikali ya Awamu ya Sita za kuhakikisha Tanzania inakuwa sehemu ya uchumi wa kidijitali wa kimataifa.
Minara hiyo imewezesha upanuzi wa huduma za mawasiliano ya simu na intaneti hadi maeneo ya mbali, ikiwa ni pamoja na vijiji vilivyokuwa havipatikani hapo awali. Mafanikio haya ni ya kipekee kwa kuwa yameshinda ujenzi wa miaka 59 ya awali kwa takriban mara 11, jambo linaloonyesha weledi wa utawala wa sasa katika kufanyakazi.
Jitihada za Serikali za kuimarisha Sekta ya Mawasiliano
Serikali chini ya Rais Samia imechukua hatua mbalimbali za kukuza miundombinu ya mawasiliano, ambapo pia serikali imewekeza fedha za ndani na kushirikiana na wadau wa sekta binafsi ikiwemo kampuni za simu kama Vodacom, Airtel na Tigo, kujenga minara ya mawasiliano katika maeneo ya vijijini na mijini. Ushirikiano huu wa umma na sekta binafsi umehakikisha uongozi bora wa miradi na matumizi bora ya rasilimali.
Serikali pia imeshirikiana na taasisi za kimataifa kama Benki ya Dunia na wafadhili wengine kupata rasilimali za kujenga miundombinu ya mawasiliano ya kisasa. Kupitia sera za kuimarisha uchumi wa kidijitali, serikali imehimiza matumizi ya huduma za mtandao kama biashara za mtandaoni, malipo ya kidijitali, na huduma za serikali za mtandaoni.
Maboresho ya mazingira ya kisheria kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) yamehakikisha mazingira wezeshi kwa uwekezaji katika sekta ya mawasiliano na kuongeza uhakika wa wawekezaji wa ndani na wa nje.
Ujenzi wa minara ya mawasiliano na maendeleo nchini Tanzania
Ujenzi wa minara 8,524 ya mawasiliano umeendelea kuchangia pakubwa katika maendeleo nchini Tanzania. Upatikanaji wa mawasiliano katika maeneo ya mbali umekuwa moja ya mafanikio makubwa, ambapo minara hiyo imehakikisha huduma za simu na intaneti zinapatikana katika maeneo yenye changamoto za kijiografia, kama vile vijiji vya mbali katika mikoa ya Simiyu, Katavi, na Rukwa. Hatua hii imewezesha unganishaji wa jamii za vijijini na mzunguko wa habari na fursa za kiuchumi.
Ukuaji wa biashara za mtandao ni miongoni mwa maendeleo yaliyochochewa na ujenzi wa minara hii, ambapo upatikanaji wa intaneti umewezesha wajasiriamali, hasa vijana, kushiriki katika biashara za mtandaoni, kama vile mauzo ya bidhaa kupitia mifumo kama Jumia na malipo ya kidijitali kupitia M-Pesa, Airtel Money, na Tigo Pesa.
Maendeleo haya yametoa fursa za kipato kwa vijana na kuongeza ushiriki wa wanawake katika uchumi wa taifa. Zaidi ya hayo, huduma za serikali za mtandaoni, kama usajili wa biashara, malipo ya kodi na huduma za afya, zimeboreshwa kutokana na upatikanaji wa mtandao wa intaneti, na hivyo kuongeza ufanisi na kupunguza mzunguko wa rushwa.
Vilevile,ujenzi wa minara ya mawasiliano umechangia ajira za moja kwa moja kwa wafanyakazi wa ujenzi na za zisizo za moja kwa moja kupitia biashara zinazotegemea mtandao, kama vile wauzaji wa huduma za simu na intaneti. Maendeleo haya yamewezesha ongezeko la shughuli za kiuchumi katika maeneo ya vijijini, ambapo sasa familia zinaweza kuongeza mapato yao kupitia huduma za kidijitali na biashara za mtandao.
Kwa upande wa elimu pia, watoto wa vijijini sasa wanaweza kupata habari za kisasa na kujifunza kutumia teknolojia za kisasa katika masomo yao shuleni.
Juhudi za serikali kutatua changamoto katika sekta ya mawasiliano
Licha ya mafanikio haya, sekta ya mawasiliano bado inakabiliwa na changamoto kama vile gharama za juu za ujenzi wa minara katika maeneo ya mbali, uchakavu wa miundombinu na hitaji la kuhakikisha huduma za intaneti za bei nafuu.
Serikali inalenga kushughulikia changamoto hizi kwa kuongeza uwekezaji katika miundombinu ya mawasiliano kupitia ushirikiano wa umma na binafsi, kuhimiza kampuni za simu kutoa huduma za intaneti za bei nafuu kwa Watanzania wengi, na kuimarisha usimamizi wa miundombinu ya mawasiliano kupitia TCRA ili kuhakikisha uendelevu.
Lengo la serikali ni kuhakikisha kuwa asilimia 90 ya Watanzania wanapata huduma za simu na intaneti ifikapo mwaka 2030. Ujenzi wa minara ya mawasiliano unapaswa kuwa endelevu na pia kuongeza ushirikiano wa kimkakati na wadau wote muhimu katika sekta ya mawasiliano.
Mafanikio yote haya katika sekta ya mawasiliano chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka 4 yamefungua fursa za kiuchumi kwa Watanzania. Hatua hizi zinaonyesha dhamira ya serikali ya Awamu ya Sita ya kukuza uchumi wa kidijitali na kuhakikisha maendeleo ya pamoja yanawafikia Watanzania wote, hasa wale wanaoishi katika maeneo yenye changamoto.
Msingi huu wa miundombinu ya mawasiliano utakuwa ni msingi wa maendeleo ya uchumi wa kidijitali wa Tanzania katika miaka ijayo, na kuiwezesha nchi kushindana kwa ufanisi katika uchumi wa kimataifa.
Mwandishi: Dr. Bravious Kahyoza
Mhariri: Dominic Allen


