Wasomi: Mikataba inayoingiwa na Serikali iwekwe wazi

Na Dkt. Bravious Kahyoza

Katika mazingira ya sasa ya kiutawala na maendeleo ya Taifa, kuna umuhimu mkubwa wa kuimarisha mawasiliano na mijadala ya wazi kati ya viongozi wa serikali pamoja na taasisi zake, na wasomi na taasisi za utafiti. Utamaduni huu wa mijadala ya mara kwa mara si tu unasaidia kuongeza uwazi na uwajibikaji wa viongozi, bali pia huwapa nafasi ya kupimwa kifikra na kimawazo, hali inayochochea utendaji bora wa majukumu yao ya kitaifa. Wasomi wakiwa na hazina kubwa ya ujuzi nchini, wanaweza kutoa mchango wa kipekee katika kutoa dira mbadala na hoja za msingi zinazoweza kusaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazolikabili Taifa la Tanzania.

Kupitia mijadala hii, viongozi wanaweza kujifunza mitazamo mipya, kupokea mrejesho wa moja kwa moja kutoka kwa wananchi kuhusiana na utendaji wao wa kazi, pia hufungua mlango wa kupanga mikakati ya pamoja itakayowezesha utekeleza thabiti wa mipango ya kitaifa. Hii ni njia mojawapo ya kuondoa maamuzi ya kisiasa yasiyo na msingi wa kitaalamu, na badala yake kuweka mbele maslahi ya Taifa kwa kushirikisha wadau mbalimbali.

Hoja ya mapendekezo haya ya kuimarisha mijadala kati ya viongozi wa serikali na wasomi ilitolewa katika Kongamano maalum lililofanyika Mei 27, 2025 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), lililoangazia namna Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) unavyoweza kuchochea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Kongamano hili liliandaliwa na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti na Elimu kwa Demokrasia Tanzania (REDET), ambapo wadau kutoka serikalini, sekta binafsi pamoja na wasomi walijadili kwa kina nafasi ya mijadala ya kitaaluma katika kusaidia mageuzi ya kimaendeleo.

Dr. David Rwehikiza ambaye alipata wasaa wa kushiriki na kuchangia katika kongamano hili maalumu ambalo lilijadili kwa mapana kuhusu nafasi ya PPP katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, anaona ni muda  muafaka sasa kwa viongozi wa serikali pamoja taasisi za kiserikali kuweka utamaduni wa midahalo.

“Iwe ni midahalo ya kudumu kwamba badala ya kumleta tu Kafulila (Mkurugenzi wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi_PPPC, David Kafulila ) leo, tutegemee baadae mtuletee Mawaziri lakini hata Wakuu wa Taasisi mbalimbali ili Chuo Kikuu kiendelee kuwa chachu ya kuibua hii mijadala” amependekeza Dr. Rwehikiza.

Baadhi ya wadau mbalimbali walioshiriki katika Kongamano hili lililowakutanisha kwa ajili ya kujadili namna ambavyo Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) unavyoweza kuchochea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Dr. Rwehikiza hakuishia tu kwenye suala la kkuwa na mijadala endelevu, pia aliweka msisitizo kwa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC) na Taasisi ya Utafiti na Elimu kwa Demokrasia Tanzania (REDET) pindi inapoitisha mijadala ya namna hii kuwepo na tafiti ambazo tayari zimekwishafanyika, lengo ikiwa ni kuipa uhai mijadala hiyo.

“Nilivyowasikiliza wazungumzaji walio wengi kuna changamoto ya tafiti katika eneo hili (PPP), kwa hiyo tunaweza kuangalia ni kwa namna gani Kituo cha Ubia kinaweza kikafadhili au kikahamasisha tafiti katika eneo hili hapa (PPP) ili tukija kwenye makongamano kama haya tayari tunakuwa na mijadala ambayo ina ushahidi, ama tunaweza kuandaa warsha (Workshop)” ameongeza Dr. Rwehikiza.

Kwa upande wake Dr. George Malonga wakati achangia katika kongamano hili ametupia jicho umuhimu wa watu kupatiwa elimu ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) ili waweze kuwa na uelewa mpana kuhusu faida zake kwa maendeleo ya nchi.

“Tunaomba watu wetu tuwapeleke darasani, kuhusiana na hiki kipindi (PPP), kama vile tunavyowapeleka watoto shuleni kuhusiana na ‘field zao na discipline mbalimbali’ wanatoka wakiwa wameiva vizuri” amesisitiza Dr. Malonga.

Suala la uwekezaji ni moja ya mambo yaliyowekwa mezani wakati wa kongamano, hii ni kutokana muhimu wake katika kukuza uchumi wa nchi, kwani ni kichocheo cha maendeleo ya miundombinu, ajira pamoja na kuongeza mapato ya serikali kupitia kodi na tozo mbalimbali.

Kupitia uwekezaji wa kigeni, nchi hupata fursa ya teknolojia mpya, ujuzi na kuongeza uzalishaji na ushindani katika soko la kimataifa. Mbali na hayo pia huchagiza maendeleo katika sekta ya kilimo, madini, nishati, viwanda pamoja na sekta nyinginezo.

Katika kuhakikisha nchi inapiga hatua katika kiuchumi na maeneo mengine muhimu, Serikali ya Tanzania imeingia mikataba kadha wa kadha na wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali katika sekta tofauti tofauti.

Licha ya nia njema hiyo, lakini baadhi ya mikataba hiyo ambayo serikali imeingia imezua mijadala kama inayo tija na kulinda maslahi mapana ya wananchi, lakini pia suala la uwazi kuhusiana na mikataba hiyo ambayo serikali huingia.

Miongoni mwa mikataba ambayo serikali ilingia, ikagonga vichwa vya wananchi na kuzua mjadala ni pamoja na ule ambao serikali ya Tanzania uliingia na Kampuni ya DP World kutoka Dubai.

Katika mkataba huo ambao uliidhinishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo Juni 10, 2023 na kusainiwa Oktoba 22, 2023 katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, DP World ilitakiwa kuwekeza kiasi cha USD bilioni 675, ambapo kwa miaka mitano ya mwanzo ilipaswa kutoa kiasi cha USD bilioni 250, hadi kufikia Novemba, 2024 tayari ilishatoa USD bilioni 214.42.

Suala la kutokuwepo na uwazi pia lilichochea baadhi ya wananchi kutokuwa na imani na mkataba huo. Kukosekana kwa uwazi katika mikataba ya namna hii kumewafanya washiriki wa kongamano hili lililoandaliwa na PPPC pamoja REDET kupigilia msumari uwazi katika mikataba ambayo serikali inaingia na wawekezaji, hasa wa kigeni.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), David Kafulila (kushoto) akiteta jambo na Mwenyekiti wa Taasisi ya Utafiti na Elimu kwa Demokrasia Tanzania (REDET), Profesa Rwekaza Mukandala (kulia).

Prof. Abel Kinyondo ambaye alikuwa ni miongoni mwa watoa mada katika kongamano amesema kuwa haoni haja ya mikataba hiyo kuwekwa mbali na macho ya wananchi.

“Sioni sababu ya viongozi wa serikali, wale watu walio karibu na mamlaka kufikiria kwamba wakiuficha huo mkataba wanafanya kitu sahihi, wakati mwingine wanaweza wakatuhumiwa vitu ambavyo hata hawafanyi” amesema Prof. Kinyondo.

Wakati Prof. Kinyondo akisema kuwa usiri katika mikataba ambayo serikali inaingia unaweza kuibua hisia tofauti, itakumbukwa kuwa mapema mwaka huu Serikali ya Tanzania ilipoingia kwenye makubaliano na Kampuni ya Uwekezaji na Maendeleo ya Saudi Arabia (SADC) kuhusu Bandari ya Bagamoyo, hisia tofauti ziliibuka hasa kutoka kwa wanaharakati wakisema kuwa Serikali imeiachilia bandari hiyo kwa kampuni hiyo, hata hivyo serikali ilikanusha vikali madai hayo ikisema kuwa makubaliano hayo hayakuhusisha ujenzi wa moja kwa moja wa bandari bali ni kwa ajili ya hatua za awali kama upembuzi yakinifu na maandalizi mengine.

Prof. Kinyondo amesisitiza kuwa kuna umuhimu mkubwa sana kwa mikataba kuwekwa wazi kwa wananchi ili waone kama ina malengo mazuri yenye  maslahi kwa Taifa.

 “Wapo Watanzania milioni 65, Watanzania wachache tu hawawezi kufikiria kwa niaba ya kila mtu. Hawawezi wakawa wazalendo kwa niaba ya wengine waliobaki” amesisitia Prof. Kinyondo kuhusiana na suala la uwazi katika mikataba ambayo Serikali ya Tanzania inaingia.

Kama ilivyoelewa hapo awali kuhusu umuhimu wa uwekezaji nchini Tanzania, Meneja wa Uhamasishaji Uwekezaji wa Ndani kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Felix John akijibu hoja zilizoibuliwa wakati wa mjadala katika kongamano, amebainisha kuwa serikali imeendelea kuweka vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi ili kuwavutia wawekezaji wa kigeni.

“Ili kutekeleza kwa ufanisi miradi ya uwekezaji, Serikali inatoa vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi. Hivi vya kikodi lengo lake ni kupunguza gharama za mradi husika…lakini pia visivyo vya kikodi ni pamoja na kuleta wataalamu wasiozidi kumi kwa ajili ya kutekeleza mradi kwa ufanisi” ameeleza Bw. Felix.

Katika kongamano hili ambalo lilijikita katika kumulika mchango wa PPP katika utelelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, nae Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), Mhe. David Kafulila amezitaja sababu ya kufanya Ubia, ambapo amesema kuwa sababu mojawapo ni kuvuta mitaji ya sekta binafsi itekeleze majukumu ambayo yalitakiwa kufanywa na serikali, vilevile kuvuta teknolojia nchini kutoka kwa wawekezaji wa kigeni, bila kusahau ufanisi katika usimamizi wa miradi husika.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), Mhe. David Kafulila akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano hili lililofanyika leo Mei 27, 2025 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Uwekezaji wa kigeni kama utasimamiwa ipasavyo unaweza kuinufaisha nchi kwani huchochea ukuaji wa uchumi na Pato la Taifa, kuongezeka kwa mapato ya serikali kupitia kodi, tozo na ada, uboreshaji wa miundombinu kama vile bandari, barabara, reli pamoja na kukuza ajira kwa wananchi zile za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, pamoja na faida nyingizeo.

Kwa ujumla, kongamano hili si tu limeibua hoja za msingi kuhusu Ubia  kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP), bali pia limedhihirisha umuhimu wa kuwepo kwa uhusiano wa karibu kati ya viongozi wa serikali pamoja na wasomi.

Vilevile, suala la uwazi katika mikataba ya uwekezaji limeonekana kuvaliwa njuga na wasomi, ambapo wadau mbalimbali walisisitiza kuwa mikataba inayohusu rasilimali za taifa haipaswi kufanywa kwa usiri, kwani uwajibikaji na ushirikishwaji wa wananchi ni nguzo muhimu katika kujenga imani ya umma na kuhakikisha kuwa mikataba hiyo inalinda maslahi ya taifa. Ni wazi kuwa utamaduni wa kuwepo kwa mijadala ya wazi na ushirikiano ni misingi isiyoepukika katika kulijenga Taifa lenye mwelekeo wa pamoja, lenye uwazi wa kimaamuzi na maendeleo jumuishi kwa wote.

Mwandishi: Dkt. Bravious Kahyoza
Mhariri: Dominic Allen

Hot this week

Mnyonge, mnyongeni ila haki yake mpeni

By Dorlingson Edward Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), leo...

CHADEMA kutoa msimamo wake kuhusu maridhiano

By Veronica Mlyatu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa...

Popular Articles

Safari ya Mashimba katika kutetea jamii ya Wahadzabe

Nchini Tanzania  kuna jumla ya makabila zaidi ya 120...

Polisi waendelea kuwashikilia viongozi wa CHADEMA

Ni siku ya kwanza tangu kukamatwa kwa viongozi wa...

Siku ya Vijana Duniani.

Kwa sasa ni kijana wa miaka 25 ambaye amejiajiri...

BWAWA LA ARBA’AT  LASABABISHA MAAFA NCHINI SUDAN

Watu 30 mashariki mwa Sudan na na wengine 60...

Sand Mining in Tanzania: Trails of Destruction in Lake Victoria and its Environs

By Dominic Allen On November 14th, 2021 in the Geita...

 Utekaji: Fumbo linalotushinda?

Na Yohani Gwangway Taifa la Tanzania kwa miaka mingi limekuwa...

Abduction: Is it a riddle we can’t solve?

By Yohani Gwangway For many years Tanzania has been an...

Mustakabali wa Hewa Safi kwa kila kiumbe

Na Dominic Allen Msingi wa maisha ya viumbe hai yaani...
LAND DWELLERS FACT CHECK HUB VERIFY FACTS STOP MISINFORMATION Trusted Fact-Checking in Tanzania Beyond What You Know VERIFY NOW

Related Articles

Popular Categories

DWELLERS CHECK-HUB Verify Facts. Stop Misinformation Trusted Fact-Checking in Tanzania • Beyond What You Know VERIFY NOW