Na Dkt. Bravious Kahyoza
Wadau mbalimbali walioshiriki katika kongamano Ubia kati ya sekta ya Umma na sekta binafsi lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) leo Mei 27, 2025 wamependekeza kuwa mijadala muhimu inayohusu mambo ya kitaifa inatakiwa kujadiliwa katika taasisi za elimu hasa vyuo vikuu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa kongamano hilo wadau hao walisema kuwa serikali inatakiwa kupeleka mijadala vyuoni ikiwemo inayohusisha Mawaziri, Wakuu wa taasisi ili vyuo vikuu viwe sehemu ya kuibua mijadala mbalimbali yenye maslahi kwa Taifa.
“Iwe ni midahalo ya kudumu kwamba badala ya kumleta tu Kafulila leo, tutegemee baadaye mtuletee Mawaziri lakini hata Wakuu wa Taasisi mbalimbali ili Chuo Kikuu kiendelee kuwa chachu ya kuibua hii mijadala.” Alipendekeza Dkt. David Rwehikiza.

Kwa upande mwingine wakati wa mawasilisho ya kongamano hili iliyowashirikisha wadau na wanazuoni mbalimbali, Dr. George Malonga ambaye ni mshiriki katika amesisitiza kuhusu elimu ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi kutolewa kwa watu ili kuwajengea uelewa zaidi.
“Tunaomba watu wetu tuwapeleke darasani, kuhusiana na hiki kipindi (PPP), kama vile tunavyowapeleka watoto shuleni kuhusiana na ‘field zao na discipline mbalimbali’ wanatoka wakiwa wameiva vizuri” amesisitiza Dr. Malonga.
Kiu ya wanazuoni mbalimbali katika kongamano hilo ilikuwa ni kuona mawaziri na wakuu wa taasisi za serikali wakileta mijadala kuhusu mwelekeo wa wizara zao ama taasisi wanazoziongoza ili jumuiya ya wanazuoni iwe sehemu ya kuzalisha mawazo mapya kama Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere aliyoamini katika hilo.
Historia ya mijadala vyuoni nchini Tanzania
Mapendekezo ya wadau katika kongamano la PPP lililofanyika chuo kikuu cha Dar es salaam siyo jambo jipya nchini Tanzania. Katika nchi mbalimbali wanasiasa pamoja na viongozi wa Umma wanapotaka kujadili mambo yanayohusu Taifa hupenda kupeleka mambo hayo kwa taasisi za elimu. Na kwa baadhi ya nchi hata watu mashuhuri wanapotaka kutangaza rasmi matarajio yao ya kisiasa na mtazamo wao kuhusu nchi yao, basi hufanya hivyo mbele ya wanazuoni.
Nchini Tanzania kwa miaka mingi Ukumbi wa Nkrumah (Nkurumah Hall) auliopo Chuo Kikuu cha Dar es salaam ulikuwa kitovu cha mijadala ya kitaifa ambapo viongozi wa kitaifa walipotaka kutoa maono yao ya wapi wanataka kupeleka nchi, basi walishiriki na wanazuoni. Hii ilikuwa muhimu kwa sababu ilitoa nafasi ya wao kuelezea maono yao, kuyapima pamoja na wanazuoni na kuyaboresha zaidi baada ya kupokea maoni ya wanazuoni wengine.
Mwalimu Julius Nyerere wakati wa uongozi wake na baada ya uongozi wake alipenda kushiriki katika mijadala hasa katika chuo Kikuu cha Dar es salaam. Kwahiyo dhana ya kufanya mijdala muhimu katika taasisi ya elimu ya juu hasa kwa viongozi wa serikali, wakuu wa taasisi za serikali na viongozi wa Umma kama ilivyopendekezwa na Dr. David Rwehikiza na suala muhimu kuzingatiwa katika wakati ulipo. Katika kipindi hiki Taifa linapojadili masuala ya Ubia, ajira, matatizo ya mabadiliko ya nchi, uwekezaji, teknolojia na masuala mablimbali yanayohusu taifa, basi ni muhimu viongozi wakaona ni vyema kushirikisha wasomi wa taifa hili ili waamini pamoja na wao katika maoni hayo.
Mwl. Nyerere wakati akiwa madarakani na baada ya kusataafu alikuwa na utaratibu wa kuhudhuria katika midahalo na mijadala ambayo mingi ilikuwa inafanyika chuo kikuu cha Dar es salaam. Mijadala na midahalo hiyo ilifanyika sana pia wakati Mwl. akitaka dhana ya Uchumi wa Ujamaa na Kujitegemea uweze kueleweka kwa wasomi wa kipindi hicho na uwe ndiyo mwelekeo wa wasomi. Katika Midahalo hiyo Mwl. Nyerere aliulizwa maswali kuhusu Ujamaa na mwelekeo wa taifa kwa wakati huo.
Bila kurudia maneno yake kama alivyotamka Mwl. Nyerere aliwahi kusema kuwa vyuo vikuu ni sehemu ambayo mawazo mapya huzaliwa. Kauli hii ya Mwl. ina maana kubwa sana katika kuelewa umuhimu wa kupeleka mijadala yetu mbele ya wanazuoni. Tunapojadili kuhusu mipango na mikakati yetu, tunahitaji wasomi watuelewe kwanza. Wasomi wakituelewa itakuwa rahisi kuelewesha Umma wote na kwa maana hiiyo wasomi hao watatusaidia kuelimisha Umma. Lakini kwa yale ambayo wasomi wanaona hayendi vizuri, ni muhimu kufanya mijadala ambayo itatoa mitazamo na fikra mpya ya kufanya mambo.

Tarehe 19 mwezi wa tano mwaka huu aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini Thabo Mbeki alishiriki mjadala pamoja na Rais wa awamu ya nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete katika mjadala mabo alizungmzia kuwa bara la Afrika linahitaji kutatfuta suluhisho la matatizo yake yenyewe na siyo kutegemea wwengine. Katika mtazamo wa aina hii ya kuwa Africa inatakiwa kuwa na suluhisho la matatizo yake basi ni vizuri zaidi mijadala yetu ikajikita kwa wasomi.
Wizara mbalimbali zinapopanga masuala yao na kupanga mwelekeo wao wanatakiwa kushirikisha wasomi ambao wanaweza kushauri na kuboresha mwelekeo wa taifa lao. Wasomi hawa pia wanaweza kuwa na mawazo mapya ambayo yanaweza kusaidia katika mweleko mpya wa taifa letu
Kwanini mijadala vyuoni?
Mchumi na gwiji duniani, Joseph Stiglitz alipoibua dhana ya Uhusiano wa Uchumi wa taarifa(Information Econmics) mwanzoni mwa mwaka 2000;s alilipa nguvu hoja ya Mawasiliano ya Sera (Policy Communication). Toka Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani mwaka 2021 hadi sasa ametoa hotuba 34 zenye uhusiano wa moja kwa moja na uchumi . Na tangu aingie maadarakani Rais Samia Suluhu Hassan ameuliza swali hili mara tatu.
Ni kitu gani nchi zilizo na rasilimali kidogo zimefanya na kuendelea ambacho sisi hatujafanya?
Swali hili la Rais ambalo linaonesha kiu yake ya kutaka Taifa letu kupiga hatua na wakati mwingine kuhitaji majibu kutoka kwa wanazuoni ambao wanatakiwa kutoa majibu ya matatizo yetu, linahitaji mijadala ya masuala muhimu ya taifa letu mebele ya wasomi. Sera zetu za maendeleo, dira yetu ya maendelo malengo yetu ya kiuchumi, miradi yetu ya kimkakati na mambo yote muhimu yanahitaji mawazo mapya kutoka kwa wasomi hawa. Kitakwimu zaidi ya theluthi moja wa watanzania ni vijana. Baadhi ya vijana hawa ambao wako vyuoni wanatakiwa kuwa sehemu ya mijadala ya kuamua hatma ya taifa lao.
Vyuo vikuu na taasisi za elimu kwa ujumla ni sehemu ya kupima kwa hakika sera zetu. Ni katika uwanda wa wasomi ambapo tutagundua makosa yetu ya kinadharia na wakati mwingine kupata nadharia mpya ya namna ya kufanya mambo yetu. Ni kwa msingi huu ni muhimu kuwa na mijadala mbele ya wasomi watuambie mtazamo wao wa namna ya kufanya mambo. Kama vyuo vikuu vitatumika vizuri ni rahisi kuwa na mwelekeo wa pamoja kama taifa.
Mkataba wa Ushiriki wa Wengi kwenye Maendeleo na Mabadiliko, Arusha
Mwaka 1990, The African Charter for Popular Participation in Development and Transformation ikiwa ni Mkataba wa Ushiriki wa Wengi katika Maendeleo ulipitishwa Arusha Tanzania. Lengo la mkataba huu ni kuvuta na kuhusisisha watu wengi katika kushiriki maendeleo yao. Huu ni ushahidi wa kwamba kama tunahitaji kupiga hatua, masuala yetu ya kiuchumi, kisera, rasilimali, dira na mengine muhimu yanatakiwa kujadiliwa katika kumbi za vyuo mbalimbali ili kuamsha ari ya watu kuelewa mwelekeo wetu na kutoa ushauri juu ya mwelekeo huo. Faida ya jambo hili ni kuwa kama wanazuoni hawa watakubalina na kwa sababu wanaelewa mwelekeo wetu wa Uchumi, dira, sera na maono yetu, basi ni rahisi kuwa mabalozi wa mwelekeo huo.
Wakati nchi nyingi za Afrika zilikumbana na matatizo ya kiuchumi miaka ya 1980’s, mawaziri wa Uchumi na Mipango kutoka nchi mbalimbali walikaa na kujadiliana na kuona kwanini matatizo yaliyopo yanahitaji ushiriki na maoni ya wengi. Katika kikao cha cha 16 mawaziri hawa walikutana Arusha nchini Tanzania kupitisha Mkataba huu unaosisitiza juu ya ushiriki wa wengi hasa pale inapohitajika mabadiliko. Sera zetu, dira yetu, maendeleo yetu na maono yetu kama taifa yanahitaji kupata uungwaji mkono wa wasomi na wanazuoni. Hii haiishii katika kusifia tu, bali tunatakiwa kuonesha njia ya wapi tutapita kufika tunakotaka, wapi ilipo changamoto na tutakabiliana nayo vipi.
Katika kongamano la PPP lililofanyika Chuo kikuu cha Dar es salaam, serikali ilionesha kuwa kwa sasa inalenga kuwa kwenye uchumi wa pato la dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050. Haya ni malengo ya dira ya maendeleo ya Taifa ifikapo mwaka 2050. Maswali ya msingi ni Je, ni kwa kiasi gani viongozi katika taasisi za Umma wamefanikiwa kuonesha malengo haya kwa watu? Na ni wapi walikuna na watu hao? Bila shaka tunahitaji kukutana na watu hawa maeneo mbalimbali. Hii inaweza kuwa siyo tu vyuoni, lakini angalau tukubaliane kwa pamoja kuwa kama taifa tunahitaji kuwahusisha vyakutosha wanazuoni wetu katika malengo muhimu yanayoakisi hatma ya taifa letu.

Kwenye isha maarufu na yenye ushawishi ya Frederic Bastiat ya “Yale yanayoonekana na Yale Yasiyoonekana” (That Which is Seen anda That Which is Not Seen) anajenga hoja kuwa sera ya kiuchumi hazipaswi kupimwa kwa yale yanayoonekana tu, yaani yale ya muda mfupi tu,lakini zaidi kwa yale yasiyoonekana, yaani yale ya muda mrefu ambayo hayakudhamiririwa. Mjadala yetu inatakiwa kulenga matarajio ya muda mrefu ya masuala yetu ya kiuchumi na maendeleo. Watu wengi zaidi wanahitaji kushirikishwa zaidi ili kushiriki safari ya Uchumi tuutakao kama Taifa.
Mifano ya nchi zingine
Katika mataifa mbalimbali duniani, viongozi wengi na wakati mwingine mawaziri au watu mashuhuri hupenda kutangaza nia zao za kisiasa au sera zao za kiuchumi katika vyuo vikuu. Nchini marekani midahalo ya wagombea Urais pia hufanyika katika vyuo mbalimbali. Lengo kubwa ni kuwavuta wasomi kushiriki katika siasa hizo au kuamini sera husika ili wajue mwelekeo wa mgombea husika. Mwaka 2008, wakati Barrack Obama anagombea kwa mara ya kwanza kuwa Rais wa Marekani alienda kushiriki mdahalo wa kwanza Chuo Kikuu cha Mississippi aliposhiriki dhidi ya Seneta Cavin Mccain wa Republican.
Obama akiwa Chuo Kikuu cha Cairo mwaka 2009
Baada ya Rais Obama kuingia madarakani katika ziara yake ya kwanza barani afrika na ya 10 tangu aingie madarakani, alipofika Misri Rais Obama alihutubia katika Chuo Kikuu cha Cairo tarehe 4 mwezi Juni mwaka 2009. Hotuba yake ilipewa jina la “Mwanzo Mpya” yaani The New Beginning akimaanisha mwelekeo wake mpya na nchi za Kiislamu
Mwaka 2016 wakati wa mdahalo wa Urais nchini Marekani Hilary Clinton na Trump walikuwa kwenye mdahalo wa Urais katika chuo kikuu cha St. Louis Missouri. Jambo kubwa hapa ni kuwa siyo kweli kuwa wagombea hawa walishindwa kupata kumbi kubwa katika hoteli katika miji ya New York au Washington DC, la hasha. Viongozi hawa walijua kuwa ili kushawishi watu unahitaji kushawishi wasomi na wanazuoni ili waone sera zako za uchumi, maendeleo, afya na sekta zingine muhimu.
Mwandishi: Dkt. Bravious Kahyoza
Mhariri: Yohani Gwangway


