Kafulila: Tanzania kuingia Uchumi wa dola trilioni moja mwaka 2050

Na Dkt. Bravious Kahyoza

Katika juhudi za kuimarisha ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Binafsi, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), Mhe. David Kafulila, amesisitiza umuhimu wa uwekezaji kwa njia ya Ubia kama njia madhubuti ya kufanikisha maendeleo ya taifa. Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) lililofanyika jana Mei 27, 2025 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Mhe. Kafulila alieleza kuwa Tanzania inalenga kufikia uchumi wenye thamani ya dola trilioni moja kwa mwaka ifikapo mwaka 2050. Kongamano hilo limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya kituo hicho na Taasisi ya Utafiti na Elimu kwa Demokrasia Tanzania (REDET).

Wakati wa kongamano hilo lililojadili nafasi ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo Tanzania ya mwaka 2050, Mhe. David Kafulila alieleza dira hii imelenga Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zilizo katika kundi la Pato la Taifa la dola trilioni moja kwa mwaka.

“Tunapozungumza sasa kuhusu ujenzi wa huu uchumi kwenda mwaka 2050, kwamba tujenge uchumi utakaofikia dola trilioni moja, tunapozungumzia kuingia katika uchumi klabu wa dola trilioni moja, lazima tutazame tunataka kufafana na nani. Kwa mazingira ya sasa ni nchi 19 ambazo zimefikia uchumi dola trilioni moja” ameeleza Mhe.  Kafulila.

Mataifa yenye uchumi mkubwa duniani wanakuwa na Pato la Taifa kutokana na thamani ya bidhaa zilizouzwa katika nchi husika yenye kufikia dola trilioni moja ndani ya kipindi cha mwaka mmoja. Mataifa yenye uchumi huu ni mataifa yenye maendeleo makubwa ambayo mitaji inayowekezwa kwenye miradi husika ni mikubwa. Akitoa mfano jinsi kunavyohitajika juhudi ili kufikia malengo hayo, Mhe. Kafulila alitoa mfano wa Afrika kusini ambayo kwa sasa bado haipo kwenye nchi hizo.

“Uchumi wa Afrika Kusini unakaribia dola bilioni 400 kwa mwaka, ukizungumzia Uchumi wa Pato la dola trilioni 1, unazungumzia kwenda karibu mara mbili na nusu ya ilivyo Afrika kusini. Hii inaweza kuonekana kuwa ni malengo yaliyopitiliza, lakini inawezekana. Inahitaji mabadailiko makubwa ya jinsi tunavyofanya mambo” ameongeza Mhe. Kafulila.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), Mhe. David Kafulila akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano lililofanyika jana Mei 27, 2025 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambapo lilijadili nafasi ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo Tanzania ya mwaka 2050.

Afrika Kusini ni miongoni mwa nchi zenye uwekezaji mkubwa barani Afrika, hasa katika sekta mbalimbali. Akisisitiza nafasi ya PPP katika uwekezaji unaohitaji mitaji mikubwa, Mhe. Kafulila alitoa mfano wa maendeleo ya taifa la Afrika Kusini katika sekta mbalimbali.

“Iangalie Afrika Kusini, angalia  miundombinu ya Afrika Kusini katika umeme, reli, bandari, barabara na mengineyo. Angalia Afrika kusini picha yake, angalia hali tuliyonayo, unaweza ukajua ni kwa kiasi gani tunahitaji uwekezaji na uwekezaji huo hauwezi kutimizwa kwa tozo, kodi na mikopo kwa sababu ni uwekezaji mkubwa unaohitaji mtaji mkubwa” alifafanua Mhe. Kafulila.

Mhe. Kafulila alisema kuwa kwa sasa serikali nyingi duniani zinahitaji uwekezaji huo kwa sababu pesa za tozo, kodi na mikopo zinazidiwa na mahitaji ya watu. Wakati tukitaka kupata ufafanuzi wa maana ya Uchumi wenye Pato la  dola trilioni moja kwa mwaka, Mtaalamu na mchambuzi wa Uchumi, Dr. Bravious Kahyoza alisema kuwa kufikia uchumi na uwekezaji mkubwa, serikali pekee haiwezi. Nguvu ya sekta binafsi inatakiwa kuunganishwa.

“Huu ni uchumi ambao maana yake ni kuwa kuna kazi kubwa ambayo haiwezi kufanywa na serikali. Kiuhalisia hadi kufikia uchumi huo pato la kila Mtanzania linatakiwa liongezeke kutoka dola 1,300 ya leo hadi dola 7,000 kwa mwaka” alisema Dr. Bravious.

Baadhi ya wadau mbalimbali akiwemo Mchambuzi na Mwanahabari mkongwe, Jenerali Ulimwengu (katikati) wakifuatilia kwa umakini hoja zilizokuwa zikiibuliwa katika kongamano hilo.

Kwa mujibu wa Shirika la Fedha duniani (IMF) mataifa yenye uchumi wa pato la dola trilioni moja kwa mwaka ni 19 hadi sasa ikiwa ni pamoja na Marekani, China, Ujerumani, India, Japan, Uingereza, Ufaransa, Italia na Canada. Mataifa mengine yenye uchumi huu ni pamoja na Brazil, Urusi, Hispania, Korea Kiusini, Australia, Mexico, Uturuki, Indonesia, Uholanzi na Saudi Arabia. Kutoka bara la Afrika, Afrika Kusini ipo nafasi ya 30 duniani ikiwa na uchumi wenye pato la dola bilioni 413 kwa mwaka.

Kwa sasa Uchumi wa Tanzania upo nafasi ya 81 duniani ukiwa na uchumi wenye Pato la dola bilioni 85 kwa mwaka.

Kwanini PPP kwenye Uwekezaji wa sasa?

Katika uwasilishaji uliofanywa katika kongamano hilo, Mkurugenzi wa Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), Mhe. David Kafulila alisisitiza kuwa kuelekea kwenye ndoto ya uchumi imara, ni muhimu kuruhusu sekta binafsi kuleta mitaji mikubwa.

“Tunafanya ubia kwa sababu ya kuvuta mitaji ya sekta binafsi itekeleze majukumu ambayo msingi yalitakiwa kufanywa na serikali. Kwa mantiki nyingi, katika kufanya ubia tunatoa nafuu kwenye balance sheet ya serikali, yaani kwenye bajeti ya serikali, kwamba badala ya kila mradi utekelezwe kwa pesa ya kodi na mkopo, sasa kwa kutuimia utaratibu wa ubia kutekeleza nje ya bajeti ya serikali ama kwa asilimia 100  au kwa kiasi fulani kutegemeana na aina ya mkataba ambao tumeutengeneza” alisema Kafulila Mkurugenzi Mtendaji wa PPPC.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), David Kafulila (kushoto) akiteta jambo na Mwenyekiti wa Taasisi ya Utafiti na Elimu kwa Demokrasia Tanzania (REDET), Profesa Rwekaza Mukandala (kulia).

Katika kongamano hilo lililohudhuriwa na wanazuoni mbalimbali hapa nchini, mjadala mkubwa ulijikita katika nafasi ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo Tanzania ya mwaka 2050, Mhe. Kafulila alisema kuwa katika dhana ya Ubia kumeonekana ufanisi kutokana na matumizi ya teknolojia. Ameeleza kuwa ujuzi katika teknolojia unavutia ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi.

“Tunafanya ubia kwa ajili ya  kuvuta teknolojia,  ni uzoefu kuwa sekta binafsi duniani imeonesha ufanisi mkubwa katika teknolojia kuliko sekta ya Umma, na ni katika misingi hiyo tunaweza kusaini mkataba wa ubia kampuni binafsi itekeleze jukumu ambalo kimsingi ni jukumu la serikali kwa sababu ya teknolojia  tu” aliongeza Mhe. Kafulila.

Tanzania ilitunga sera ya PPP mwaka 2009 lakini historia ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi unaonekana ulikuwepo hata kabla ya kutungwa kwa sera hiyo. Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa miradi inayoendeshwa kwa njia ya Ubia ina ufanisi zaidi katika usimamizi wake. Akiwasilisha hoja katika kongamano hilo Mhe. Kafulila alisisitiza sababu ya kwanini miradi inahitajika kufanyika kwa njia ya Ubia.

“Tunafanya ubia kwa sababu ya ufanisi katika usimamizi. Tafiti zinaonesha kuwa sekta binafsi aidha kutokana na asili yake au sababu zingine zote, ina ufanisi katika usimamizi kuliko sekta ya Umma. Kwahiyo tunaweza kufanya ubia ili tu kuvuta ufani katika ufanisi”. Mhe. Kafulila kuhusiana na hoja ya ufanisi katika usimamizi.

Kwa upande mwingine Prof. Anna Tibaijuka ambaye ni Mbunge wa zamani wa Jimbo  la Muleba Kusini alisema kuwa licha ya kuhitaji kufanya miradi kwa njia ya Ubia au uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje yaani Foreign Direct Investment, lakini kunahitajika uwazi katika kutekeleza miradi ya PPP. Prof. Tibaijuka alisema kama mikataba na mijadala muhimu ya miradi ya PPP haitapelekwa Bungeni basi kuna uwezekano mkubwa miradi hiyo isifanikiwe.

“Hakuna utamaduni wa PPP. Hakuna uwazi. Watu wanasimama Bungeni wanaongea half truth. Mtu uko Bungeni na umetajwa katika jambo lakini haupewi nafasi ya kuzungumza. Sasa katika hali kama hii inakuwa ngumu, ndiyo maana migogoro katika PPP haiishi na haitaisha kwa sababu hakuna uwazi.” Maoni ya Prof. Anna Tibaijuka kuhusiana na miradi ya Ubia.

Mbunge wa zamani wa Jimbo  la Muleba Kusini, Prof. Anna Tibaijuka akichangia mada kuhusiana na dhana ya Ubia katika uwekezaji.

Hoja ya kuongezeka kwa deni la serikali

Wakati wa wasilisho lake Mhe. Kafulila alieleza kuwa uchumi wa serikali nyingi duniani kwa sasa umekuwa unaoendeshwa kwa madeni kutokana na ongezeko la mahitaji ya binadamu. Mahitaji haya yanafanya bajeti za serikali nyingi kulemewa na hivyo kuhitajika uwekezaji wa mbadala.

“Ukweli ni kwamba katika ulimwengu huu, mahitaji ya binadamu ni makubwa kuliko uwezo wa serikali nyingi duniani kama siyo zote katika kufikia mahitaji hayo. Ukisoma taarifa ya IMF ya mwaka 2024 unaonesha kuwa uchumi wa dunia yote unaendeshwa ni uchumi unaooendeshwa kwa mikopo yaani debt finances. Uchumi wa dunia wakati ukiwa dola trilioni 110 mwaka jana deni la dunia yote ilikuwa ni trilioni 10, uchumi wa Afrika uwiano wa deni na uchumi ni asilimia 67, huku Tanzania uwiano wa uchumi na deni ukiwa asilimia 47.” Ufafanuzi wa Mhe. Kafulila.

Nchini Tanzania kumekuwa na ongezeko la deni la taifa hadi kufikia shilingi trilioni 97.35 kwa mujibu wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2023/2024 wakati ikiwasilishwa mwezi Machi mwaka huu. Kwa mujibu wa CAG Bw. Charles Kichere deni hilo ni hadi kufikia Juni 30, 2024. Kufuatia kuongezeka kwa deni la serikali, Mhe. Kafulila anasema huo ni mjadala ambao hauna ubishi licha ya kuwa deni hilo bado ni himilivu.

“Ni mjadala kwamba deni linaongezeka na deni linakua, na ni kweli deni linakua. Lakini huu mwenendo ni mwenendo wa dunia. Na sababu kubwa ukiacha sababu zingine kama UVIKO-19 na global supply chain ni kuongezeka kwa mahitaji duniani ukilinganisha na kodi inayopatikana.” Alifafanua Mhe. Kafulila, Mkurugenzi Mtendaji wa PPPC.

Akitoa mwenendo wa mataifa mbalimbali pamoja na wastani wa uwiano kati ya deni na uchumi wa dunia, Mhe. Kafulila alisema kuwa bado Tanzania ina unafuu kwa nchi zilizo kusini mwa Afrika na mashariki mwa Afrika.

“Deni la serikali kwa mfano ni kubwa na hakuna mjadala kuhusu hilo. Lakini kama nilivyosema hapo awali wastani wa deni la serikali zote duniani ni asilimia 90, wastani wa deni la serikali zote za Afrika kwenye uchumi ni asilimia ni zaidi ya asilimia 67, wakati deni la serikali kwenye uchumi ni asilimia 47. Katika muktadha huo licha ya deni kuongezeka lakini uchumi huu ni himilivu ukilinganisha na mwenendo wa uchumi wa nchi nyingi za kusini mwa Afrika na mashariki mwa Afrika.” Mhe. Kafulila akielezea  kuhusu uwiano kati ya deni na uchumi katika maeneo mbalimbali duniani.

Akitaja hali ya wastani wa uwiano kati ya deni na uchumi, Mhe. Kafulila alitaja nchi ya Kenya kuwa na uwiano wa asilimia 70, Rwanda 71, Malawi 84 na Ghana ikiwa ni zaidi ya asilimia 90.

Kwanini tunakopesheka licha ya deni kuongezeka?

Swali kubwa kwa Watanzania ni kuhusiana na suala la deni la serikali kuongezeka huku baadhi ya miradi mikubwa ikiendelea kutekelezwa kwa mikopo. Akifafanua hoja hii Mkurugenzi Mtendaji wa PPPC Mhe. David Kafulila amesema kuwa Tanzania ilifanyiwa utafiti wakati wa serikali ya awamu ya nne, na ikaonekana kuna viashiria vya juu vya kuvutia mikopo yenye riba nafuu.

“Duniani kuna taasisi zinaitwa Credit Rating Agency, kuna taasisi tatu kubwa ambazo zinamiliki asilimia 95 ya kazi hiyo duniani, katika historia yetu tumefanyiwa solicit wakati ya awamu ya nne, na matokeo yake tulipata rating ya juu kuliko nchi zote kusini mwa Afrika na nyingi mashariki mwa Afrika. Na hii imekuwa ikitupa urahisi wa kupata mikono nafuu.” Alifafanua Mhe. Kafulila.

Kongamano hilo la siku moja pia lilijadili juu ya umuhimu kuwa na utamaduni wa kufanya mijadala ya wazi kama hii kati ya viongozi wa serikali pamoja na taasisi zake, na wasomi na taasisi za utafiti, ili kuongeza uwazi na uwajibikaji wa viongozi, jambo litakalochochea utendaji bora wa majukumu yao ya kitaifa.

Mwandishi: Dkt. Bravious Kahyoza
Mhariri: Yohani Gwangway

Hot this week

CHADEMA kutoa msimamo wake kuhusu maridhiano

By Veronica Mlyatu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa...

Mnyonge, mnyongeni ila haki yake mpeni

By Dorlingson Edward Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), leo...

Popular Articles

Safari ya Mashimba katika kutetea jamii ya Wahadzabe

Nchini Tanzania  kuna jumla ya makabila zaidi ya 120...

Polisi waendelea kuwashikilia viongozi wa CHADEMA

Ni siku ya kwanza tangu kukamatwa kwa viongozi wa...

Siku ya Vijana Duniani.

Kwa sasa ni kijana wa miaka 25 ambaye amejiajiri...

BWAWA LA ARBA’AT  LASABABISHA MAAFA NCHINI SUDAN

Watu 30 mashariki mwa Sudan na na wengine 60...

Sand Mining in Tanzania: Trails of Destruction in Lake Victoria and its Environs

By Dominic Allen On November 14th, 2021 in the Geita...

 Utekaji: Fumbo linalotushinda?

Na Yohani Gwangway Taifa la Tanzania kwa miaka mingi limekuwa...

Abduction: Is it a riddle we can’t solve?

By Yohani Gwangway For many years Tanzania has been an...

Mustakabali wa Hewa Safi kwa kila kiumbe

Na Dominic Allen Msingi wa maisha ya viumbe hai yaani...
LAND DWELLERS FACT CHECK HUB VERIFY FACTS STOP MISINFORMATION Trusted Fact-Checking in Tanzania Beyond What You Know VERIFY NOW

Related Articles

Popular Categories

DWELLERS CHECK-HUB Verify Facts. Stop Misinformation Trusted Fact-Checking in Tanzania • Beyond What You Know VERIFY NOW