Na Amiri Kilagalila
Uongozi wa Kata ya Utalingolo kwa kushirikiana na wataalamu wa Idara ya Ardhi Halmashauri ya Mji Njombe jana Mei 13, 2025 wamekamilisha zoezi la uwekaji wa alama za mipaka (bikoni) kwenye eneo la Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Tawi la Njombe lenye ukubwa wa takribani ekari 300 lililopo katika kijiji cha Ihalula, ambalo litatumiwa na wanafunzi wa chuo hicho kwa ajili ya mazoezi ya vitendo.
Hapo jana akiongoza zoezi la uwekaji wa alama za mipaka, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Njombe ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Utalingolo, Erasto Mpete amewataka wananchi wa kijiji hicho kuendelea kuimarisha ulinzi wa eneo hilo kwa maslahi ya Watanzania.
“Niwaombe wananchi waendelee kulinda hili eneo kwa maslahi ya kizazi chetu na vizazi vijavyo, lakini pia wananchi muwe na subira kwa sababu ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya chuo hiki unaenda kwa awamu. Na kwa hatua ya kwanza ujenzi umeanza ofisi kuu pale Njombe mjini na huku ni eneo la mazoezi kwa vitendo kwa hiyo wananchi wanaozunguka hili eneo huko mbeleni watanufaika kiuchumi” amesema Mpete.

Mpete pia ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha fedha za ujenzi wa Chuo Kikuu mkoani Njombe ambapo ametoa pongezi kwa Mkuu wa mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, Mbunge wa Njombe Mjini, Deodatus Mwanyika pamoja na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kuendelea kushikamana ili kukuza uchumi na miradi ya maendeleo mkoani humo.

Stanley Nyangachi ambaye ni mkazi wa Utalingolo ameishukuru serikali kwa kukubali kujenga Chuo Kikuu mkoani Njombe kwa kuwa nao pia wanakwenda kunufaika na uwepo wa chuo hicho.
“Kimsingi hata sisi wananchi wa Utalingolo tunakwenda kunufaika na chuo hiki lakini na sisi tunawakaribisha wawekezaji kwa sababu fursa zitafunguliwa kwenye maeneo yetu” ameeleza Nyangachi.
Zoezi hilo la uwekaji wa alama za mipaka limefuatia baada ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Tawi la Njombe na kampuni ya Dimetoclasa Real Hope Limited kusaini mkataba wa ujenzi wa miundombinu ya chuo hicho siku ya Jumatatu Mei 12, 2025 unaotarajia kufanyika katika mtaa wa Kihesa uliopo Halmashauri ya Mji wa Njombe.

Kwa mujibu wa Naibu Mratibu wa Mradi wa HEET kutoka Chuo kikuu cha Dodoma Dkt. Happiness Nnko alipozungumza mkoani Njombe wakati wa kusaini mkataba wa ujenzi wa miundombinu ya chuo hicho, alisema kuwa kiasi cha Tsh. Bilioni 17.17 kimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu sita ya msingi katika chuo hicho, ambapo ujenzi unafanyika katika mtaa wa Kihesa mjini Njombe.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni inayokwenda kutekeleza mradi huo ya Dimetoclasa Real Hope Limited, Bwana Dickson Mwipopo aliahidi kufikisha mitambo eneo la ujenzi katika mtaa wa Kihesa ili kazi ianze mapema, ambapo utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa chuo kikuu hicho unatarajia kugharimu kiasi cha Tsh. Bilioni 20.
Aidha, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Prof. Rwekaza Mukandala alisema kutokana na ongezeko kubwa la wanafunzi kwenye vyuo vikuu nchini, Rais Samia Suluhu Hassan aliamua kuongezwa kwa matawi ya vyuo likiwemo tawi la Njombe.
Hata hivyo Mkuu wa mkoa wa Njombe, Antony Mtaka alisema suala la elimu kwa wakazi mkoani humo ni muhimu, ambapo wazazi wanahamasa kubwa ya kusomesha watoto wao.
Mwandishi: Amiri Kilagalila
Mhariri: Dominic Allen


