Na Dominic Allen
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imesema kuwa imeridhishwa ujenzi wa vihenge vya kuhifadhia mazao na maghala wilayani Babati mkoani Manyara, ambavyo vinasimamiwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA).
Katika ziara iliyofanywa na PAC jana Machi 18, 2025, Mwenyekiti wa PAC, Japhet Hasunga ameeleza kuwa lengo la ziara hiyo ilikuwa ni kukagua utekelezaji wa mradi huo na fedha iliyotumika.
“Tumekuja kuona mradi wa vihenge ambapo Kamati imefurahishwa sana na namna vihenge vilivyojengwa, kwani vinaongeza uwezo wa kuhifadhi chakula kwa manufaa ya Taifa” alisema Hasunga.
Kwa sasa tani 776,000 za mazao zimehifadhiwa katika vihenge hivyo, zikiwemo tani 32,000 za mpunga pamoja na tani 400 za mtama, ambapo lengo la serikali ni kuhakikisha kuwa wanahifadhi tani milioni 3 ifikapo mwaka 2030.

Picha na Wizara ya Kilimo.
Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli amesema kuwa tayari wamepokea maagizo kutoka kwa PAC ya kuhakikisha vituo vitano vilivyosalia kati ya vinane vinakamilika haraka ili kutoa huduma kwa wananchi.
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


