Na Dominic Allen
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi leo Machi 06, 2025 ameufuta uongozi wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) kufuatia tuhuma mbalimbali zilizowasilishwa na wadau wa mchezo wa ngumi nchini.
Wadau wa mchezo wa ngumi waliwasilisha malalamiko yao dhidi ya TPBRC kuhusiana na matumizi mabaya ya madaraka na fedha, ambapo Mei 8, 2024 Waziri mwenye dhamana aliunda Kamati Maalum ya Uchunguzi kwa ajili ya kuchunguza malalamiko hayo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara, baada ya uchunguzi kukamilisha, imebainika kuwa kulikuwa na matumizi mabaya ya madaraka na fedha kinyume na Sheria za nchi, Katiba ya Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania ya mwaka 2018 pamoja na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora na usimamizi wa rasilimali za Kamisheni.
Kufuatia mapungufu hayo, Waziri Prof. Palamagamba Kabudi ameelekeza hatua zaidi za kisheria zichukuliwe dhidi ya viongozi walioondolewa madarakani, ili iwe fundisho kwa viongozi wengine wa vyama na mashirikisho ya michezo nchini.
Hata hivyo Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imewataka viongozi wa vyama na mashirikisho mengine ya michezo nchini kuzingatia utawala bora unaofuata misingi ya katiba kulingana na taasisi zao na nyadhifa wanazoshikilia katika taasisi hizo.

Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


