Na Yohani Gwangway
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa jana usiku kuwa kutakuwa na mvua kubwa katika mikoa 25 ya Tanzania baada ya mvua kutokunyesha kwa takriban mwezi mmoja katika maeneo mengi. Taarifa hiyo ya TMA imetahadharisha vipindi vifupi vya mvua kubwa katika maeneo ya mikoa ya Tabora, Kigoma, Katavi, Singida, Dodoma, Simiyu, Mara, Arusha, Manyara na Kilimanjaro.
Baadhi ya mikoa hii inategemewa kwa baadhi ya mazao ya chakula pamoja na yale ya biashara. Mkoani Manyara zao kubwa la chakula ni mahindi huku wakizalisha pia maharage kwa matumizi ya chakula pamoja na biashara. Kwa upande wa Singida kuna mazao kama alizeti na vitunguu ambayo ni muhimu kwa uchumi wa mkoa huo wa katikati ya Tanzania.
Siku za hivi karibuni zilizagaa taarifa katika mitandao ya kijamii ikionesha mazao kunyauka yakiwa mashambani kutokana na jua kali na kutonyesha kwa mvua. Baadhi ya wakulima wamekuwa na wasiwasi kuhusu hali ya upatikanaji wa chakula kwa mwaka huu. Lakini kama mvua hizi zitanyesha kama inavyotabiriwa basi baadhi ya mazao yataendelea kustawi.
Wakati kukiwa bado kuna sintofahamu juu ya hali ya mvua nchini, kwa mujibu wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Sekta ya Kilimo imechangia kiasi cha shilingi za Kitanzania trilioni 38 katika Pato la Taifa kwa mwaka 2024, huku ikitoa fursa za ajira kwa takriban Watanzania milioni 28.6. Hivyo, endapo hali ya mvua itakuwa siyo ya kuridhisha, kwa kiasi kikubwa hali ya uchumi kuanzia ngazi ya chini hadi juu utayumba.

Baadhi ya maeneo ya mikoa ya Simiyu, Mwanza, Shinyanga na Geita ambayo ni wazalishaji wa mpunga kwa eneo la Kanda ya Ziwa, mashamba mengi yalikosa maji kwa muda wa takriban siku 40. Tangu tarehe 8 mwezi huu tayari mvua zimeanza katika baadhi ya maeneo ya mikoa hii jambo linaloleta ahueni kwa wakulima.
Wakati haya yakiendelea, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akihutubia wananchi katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mkoani Arusha hapo jana alisema kuwa Tanzania ina uhakika wa chakula kwa zaidi ya asilimia 100.
Mwandishi: Yohani Gwangway
Mhariri: Dominic Allen


