Na Dominic Allen
Prof. Philemon Mikol Sarungi, ambaye ni mzaliwa wa Rorya mkoani Mara ni miongoni mwa madaktari wa kwanza kabisa nchini Tanzania kufuzu kuwa Daktari Bingwa wa Mifupa, aliyepata kibali cha kushika nafasi mbalimbali za juu za uongozi hapa nchini.
Mnamo Machi 23, 1936 familia ya Sarungi Igogo Yusufu na mkewe Amimo (Maria) Sarungi ilijaliwa kupata mtoto wa kiume, ni Prof. Philemon Mikol Sarungi.
Safari yake ya elimu ya juu
Mwaka 1966, Prof. Sarungi alifanikiwa kupata Shahada ya Udaktari kutoka Chuo Kikuu cha Tiba, Szeged nchini Hungary, na mwaka 1970 katika chuo hicho alipata Shahada ya Uzamilivu katika Upasuaji.
Safari yake ya elimu haikuishia hapo, kwani mwaka 1973 alipata Diploma ya Tiba ya Mifupa/Matibabu ya Majeraha kutoka Chuo Kikuu cha Tiba, Vienna nchini Austria, na mwaka 1975 alihitimu katika Chuo Kikuu cha Shanghai, China na kupata Diploma ya Upasuaji wa kurejesha viungo.
Maisha yake Binafsi
Prof. Philemon Mikol Sarungi anatokea ukoo wa Nyiratho wa Utegi. Safari yake ya maisha ya ndoa ilianza Oktoba 10, 1962 ambapo alifunga ndoa na Esther Nagy Czirok. Ndoa baina ya wawili hao ilidumu kwa miaka saba, na waliachana mwezi Aprili, 1970.
Baada ya kuachana na Esther Nagy Czirok, Prof. Sarungi alifunga ndoa na mwanamama Veronica Marton mnamo Oktoba 30, 1970.
Prof. Sarungi alibahatika kupata watoto wanne, ambao ni Martin Sarungi, Emoke Sarungi, Veronica Sarungi na Maria Sarungi.

Maisha yake Kitaaluma
Kutokea mwaka 1971 hadi miaka ya 1990, Prof. Sarungi alifanya kazi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Tanzania na alihudumu katika nafasi mbalimbali kama ifuatavyo;
Kuanzia mwaka 1971 hadi 1973, Prof. Sarungi alikuwa Mhadhiri wa Upasuaji. Kutokea mwaka 1973 hadi 1976 alishika wadhifa wa Mhadhiri Mwandamizi.
Ilipofika mwaka 1977 alikuwa ni Profesa Msaidizi huku akihudumu nafasi ya Mkuu wa Idara katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambapo baadae mnamo mwaka 1979 akawa Profesa, na alihudumu kwenye nafasi ya Mkuu wa Idara kuanzia mwaka 1977 hadi 1984.
Kuanzia mwaka 1984 hadi 1990, Prof. Philemon Mikol Sarungi alikuwa ni Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Tiba cha Muhimbili, pia alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu, kati ya mwaka 1989 na 1991.
Prof. Sarungi alikuwa ni Mwanachama wa Chama cha Madaktari Tanzania, na katika kipindi chote hicho ametoa mchango mkubwa katika maendeleo ya elimu ya tiba kwa kutoa elimu na mafunzo kwa wasomi ambao wameleta matokeo chanya kwenye Sekta ya Afya nchini.
Maisha yake kisiasa na uongozi serikalini
Enzi za uhai wake, Prof. Philemon Mikol Sarungi alikuwa ni mwanachama wa Tanganyika African National Union (TANU) tangu mwaka 1971 na baadae kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) baada ya Chama cha TANU na Afro-Shirazi Party (ASP) kuungana mwaka 1977.
Prof. Sarungi akiwa Mbunge wa Jimbo la Rorya, mkoani Mara ameshika nyadhfa mbalimbali za uongozi serikalini kuanzia miaka ya 1990.
Mwaka 1990 hadi 1992, Prof. Sarungi alikuwa ni Waziri wa Afya, kisha kuwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi kati ya mwaka 1992 hadi 1993. Ilipofika mwaka 1993 hadi 1994, Prof. Sarungi alikuwa ni Waziri wa Elimu na Utamaduni.

Kuanzia mwezi Disemba, 1995 hadi Juni, 1998 Prof. Sarungi alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani.
Mbali na kushika nafasi hizo za uongozi, pia alishawahi kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Prof. Philemon Mikol Sarungi ambaye ni baba mzazi wa mwanaharakati na mtetezi wa haki za binadamu, Maria Sarungi atakumbukwa kwa mengi, kwani maisha yake yametoa funzo na motisha kwa wasomi, wanaharakati na watanzania kwa ujumla.
Safari ya maisha ya shujaa huyu imeishia Machi 05, 2025 jijini Dar es Salaam, akiwa na umri wa miaka 88. Daima Watanzania wataendelea kumkumbuka kwa yale ambayo ameyafanya enzi za uhai wake yaliyoleta mchango mkubwa kwa Taifa la Tanzania.
Pumzika kwa amani, Prof. Philemon Mikol Sarungi (Machi 23, 1936 – Machi 05, 2025)
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


