Watanzania, amkeni!

Na Fredrick M. Justine

Mnashika Biblia kwa mikono, lakini macho yamefungwa. Mnaabudu kama vipofu, mmefunikwa macho kwa dini na kuzibwa masikio na siasa. Mmeambiwa “dini na siasa havichangamani” mkapiga makofi, mkafikiri huo ni utakatifu, kumbe ni ujinga wa kiroho.

Lakini mnaona kwa macho yenu, Kanisa la Ufufuo na Uzima la Askofu Josephat Gwajima limefungwa, lakini si kwa mapungufu ya kiroho, bali kwa sababu amekemea maovu ya utekaji na ukatili. Amesema tu kwa sauti ndogo,“Hili si sawa” na mara moja mlango wa ibada ukafungwa, si na Mungu, bali na mamlaka ya dunia.

Hivi ndivyo mfumo unavyofanya kazi, ukimsema mnyang’anyi, unanyang’anywa. Ukisema ukweli, unapokonywa jukwaa. Lakini ukimsujudia mfalme, ukamsifu Rais, ukaweka mikono yako juu yake kama nduli ni mtakatifu, unapewa chai Ikulu. Kwa hiyo, Askofu Gwajima amenyamazishwa, si kwa hoja, bali kwa kifungo.

Lakini tunamwambia: Umesimama kwenye upande sahihi wa historia. Haki huumiza kwa muda, lakini huishinda daima. Uliyenyoosha kidole kwa ujasiri, usiogope waliokufungia kanisa, maana Mungu hawajafunga Mbingu.

WATANZANIA, mnapaswa kujiuliza:

Je, kweli dini na siasa havichangamani? Au mmefundishwa kuogopa siasa ili msiseme kweli?
Je, Yesu alikaa kimya mbele ya Herode na Pilato? La hasha! Alikaa kimya si kwa woga, bali kwa hekima, kwa sababu alikwisha sema kweli. Alipovuruga meza za fedha hekaluni, hakusubiri kibali cha kuhani mkuu. Alipowaita Mafarisayo “Wana wa yule nyoka” hakuandika barua ya maombi. Haki haisubiri vibali. Haki haijui mipaka. Haki ya Mungu ni moto, ukiikanyaga, unateketea.

Mmezoea injili ya pesa, si injili ya kweli. Mmezoea kubarikiwa, si kutakaswa. Mmezoea kuombewa kazi, si kuitwa kwa kazi ya msalaba. Mmezoea makanisa ya vipaza sauti, si madhabahu za moto wa Roho.

Lakini saa imefika ya kuamka. Wale wanaotafuta HAKI kwa gharama yoyote, waamke! Wale wanaosimama hata kama wanafukuzwa makanisani, waamke! Wale wanaosema “SIO SAWA” hata kama wanapokonywa mimbari, waamke!

Tunamwambia Askofu Gwajima, na wote walio kama yeye:

Endeleeni kusimama. Mungu si bubu. Madhabahu ya kweli haijengwi na serikali wala haifungwi kwa hati. Ulimi wa haki unaweza kunyamazishwa kwa muda, lakini si milele. Kwa sababu, Mungu ni HAKI. Na HAKI ya Mungu haina mipaka. HAKI ya Mungu haisubiri kibali. HAKI ya Mungu haipigwi marufuku. HAKI ya Mungu ni kama mto, ikizuiwa hujaa na ikijaa huvunja kingo.

Watanzania, tafuteni uso wa Mungu. Sio vibali vya kuabudu, bali kibali cha mbinguni. Sio sifa kutoka kwa mfalme, bali sauti ya Mchungaji wa kweli. Maana siku ya Bwana haiji na chai ya Ikulu, inakuja na hukumu kwa wale waliogeuza hekalu kuwa maskani ya wanyang’anyi.

 “Lakini saa yaja, naam, ipo sasa, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli…” (Yohana 4:23).

(Haya ni maoni binafsi ya Mwanaharakati Fredrick M. Justine)

Hot this week

Mnyonge, mnyongeni ila haki yake mpeni

By Dorlingson Edward Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), leo...

CHADEMA kutoa msimamo wake kuhusu maridhiano

By Veronica Mlyatu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa...

Popular Articles

Safari ya Mashimba katika kutetea jamii ya Wahadzabe

Nchini Tanzania  kuna jumla ya makabila zaidi ya 120...

Polisi waendelea kuwashikilia viongozi wa CHADEMA

Ni siku ya kwanza tangu kukamatwa kwa viongozi wa...

Siku ya Vijana Duniani.

Kwa sasa ni kijana wa miaka 25 ambaye amejiajiri...

BWAWA LA ARBA’AT  LASABABISHA MAAFA NCHINI SUDAN

Watu 30 mashariki mwa Sudan na na wengine 60...

Sand Mining in Tanzania: Trails of Destruction in Lake Victoria and its Environs

By Dominic Allen On November 14th, 2021 in the Geita...

 Utekaji: Fumbo linalotushinda?

Na Yohani Gwangway Taifa la Tanzania kwa miaka mingi limekuwa...

Abduction: Is it a riddle we can’t solve?

By Yohani Gwangway For many years Tanzania has been an...

Mustakabali wa Hewa Safi kwa kila kiumbe

Na Dominic Allen Msingi wa maisha ya viumbe hai yaani...
LAND DWELLERS FACT CHECK HUB VERIFY FACTS STOP MISINFORMATION Trusted Fact-Checking in Tanzania Beyond What You Know VERIFY NOW

Related Articles

Popular Categories

DWELLERS CHECK-HUB Verify Facts. Stop Misinformation Trusted Fact-Checking in Tanzania • Beyond What You Know VERIFY NOW