Na Dominic Allen
Takriban viongozi wa ngazi za juu 35 kutoka nchi 25 Afrika wanatarajiwa kuhudhuria Mkutano wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati uliopangwa kufanyika hapa nchini Januari 27 na 28, 2025.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo amesema kuwa mkutano huo utahudhuriwa na Wakuu wa nchi 25 na Makamu wa Rais, Mawaziri Wakuu na Naibu Mawaziri Wakuu 10 na kufanya idadi ya viongozi wa ngazi ya juu kuwa 35, ambapo inaifanya Tanzania kwa mara kwanza kupokea idadi kubwa ya namna hii ya viongozi kama hao katika tukio moja.
“Tulipokea Wakuu wa Nchi 19 wakati wa kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Julius Kambarage Nyerere mwaka 1999 na Wakuu wa Nchi 15 wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) mwaka 2019, mkiangalia idadi ya Wakuu wa Nchi katika mkutano huu ni kubwa ukilinganisha na matukio hayo mawili yaliyopita.” Alisema Waziri Kombo.
Wazir Kombo amezitaja nchi zimethibisha Wakuu wa nchi zao kushiriki kuwa ni pamoja na Algeria, Comoro, Liberia, Lesotho, Botswana, Kenya, Ghana, Gabon, Sierra Leone, Ethiopia, Sudan, Malawi, Zambia, Somalia, Guine Bisau, Burundi, Mauritania, Kongo Brazzaville, Madagascar, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Libya, Nigeria, Djibouti na Gabon.
Makamu wa Rais watakaoshiriki ni kutoka Gambia na Benin, kw upande wa Mawaziri Wakuu ni kutoka Cote d’Ivoire, Uganda, São Tomé and Príncipe na Equatorial Guinea na Naibu Mawaziri Wakuu ni kutoka Eswatine na Namibia.
Waziri Kombo amesema mkutano huo ni mwendelezo wa matunda ya diplomasia ya Tanzania ambapo serikali imejipanga kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kutangazika barani Afrika na duniani kwa ujumla.
Katika hatua nyingine, ameongeza kuwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kushiriki katika Mkutano wa Nchi 20 Tajiri zaidi duniani (G20) uliofanyika Brazil mwezi Novemba 2024 na Mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya Afrika na China (FOCAC) na kupewa na nafasi ya kuzungumza kwa niaba ya Bara la Afrika ni kielelezo cha diplomasia ya Tanzania kuimarika duniani.
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


