Na Dominic Allen
Waziri Kivuli wa Viwanda na Biashara wa ACT Wazalendo, Mwanaisha Mndeme ametoa wito kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NAFRA) kuongeza juhudi za kuingiza chakula (nafaka) kwenye mzunguko ili kutoa unafuu wa bei za vyakula kwa wafanyabiashara na wateja.
Wito huo wa Waziri Kivuli, Mndeme umetolewa hapo jana mara baada ya kutembelea masoko mbalimbali jijini Dar es Salaam, ambapo aliongozana na Naibu Waziri Kivuli wa Viwanda na Biashara, Julius Massabo.
Mndeme na Massabo walipata wasaa wa kutembelea soko la Mbagala, Buguruni na Mabibo na kuzungumza na wafanyabiashara na wanunuzi wa bidhaa ili kujua changamoto mbalimbali wanazokutana zao katika biashara zao ikiwa ni pamoja na hali ya masoko hasa katika kipindi hiki cha mvua.
Wafanyabiashara wamemueleza Waziri Kivuli, Mndeme kuwa hali ya miundombinu ya masoko hayo hairidhishi, huku kukiwa na changamoto ya upatikanaji wa wateja kutokana na mfungo wa Ramadhani na Kwaresma.
Kwa upande wa wananchi, wamesema kuwa kwa kupanda kwa bei ya bidhaa ndani ya kipindi cha miezi mitatu imekuwa ni pigo kwao, wakitolea mfano wa bei ya unga wa ugali ambayo imepanda kutoka Tsh. 1,000 kwa kilo hadi Tsh. 1,400; mchele kutoka Tsh. 1,400 kwa kilo hadi Tsh. 3,000 huku mafuta kupikia yakipanda kutoka Tsh. 4,500 kwa lita hadi Tsh. 5,000.

Waziri Kivuli, Mndeme ameeleza kuwa taarifa za uchumi zinaonesha kuwa mfumuko wa bei za vyakula na vinywaji visivyokuwa na kilevi umeongezeka kutoka asilimia 4.6 mwezi Disemba 2024 hadi asilimia 5.3 mwezi Januari 2025, jambo limewasukuma kufanya ziara hiyo kwenye masoko.
Mndeme pia ameonesha kutoridhishwa na hali ya usafi kwenye masoko hayo na kuzitaka Halmashauri za Temeke, Ilala na Kinondoni kushirikiana na uongozi wa masoko na kuwa na programu maalum ya usafi na kuboresha mazingira ili shughuli zifanyike kwa usalama zaidi.

Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


