Na Amiri Kilagalila
Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Umoja wa Wanawake (UWT) mkoa wa Njombe imesisitiza uwajibikaji kwa viongozi waliopo madarakani nchini Tanzania pamoja na kufanya kazi, ili kuleta maendeleo kwa wananchi.
Wito huo umetolewa jana Mei 14, 2025 na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake (UWT) mkoa wa Njombe, Dkt. Scholastika Kevela akiwa wilayani Ludewa mkoani humo wakati Kamati ya Siasa ilipofika kwa ziara ya kawaida yenye lengo la kujenga Chama cha Mapinduzi (CCM) na jumuiya hiyo, pamoja na kukumbushana mambo mbalimbali kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
“Kiongozi yeyote uliopo madarakani lazima utuonyeshe umefanya nini, kwa hiyo hatuko tayari kuwa na viongozi wasiofanya kazi lakini nawashukuru viongozi wangu wa mkoa wa Njombe wakiwemo Madiwani na Wabunge kwa kuwa wanafanya kazi vizuri na sasa tunatoa hamasa wanaokuja wafanye kazi kwa mifano na kuacha alama” amesema Dkt. Kevela.

Kwa upande wake Anna Mwalongo ambaye ni Mjumbe wa Baraza la UWT Taifa, amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amekwisha acha alama hivyo ni wajibu kwa wanawake kwenda kuzisemea kazi zake kwa wananchi na kumtafutia kura aweze kupata ushindi mkubwa.
“Kiongozi wa UWT ukiona kuna changamoto kwenye eneo lako lazima utoe taarifa kwenye ngazi yako ya Kata na Wilaya ili ziweze kufanyiwa kazi hatutakiwi kukaa kimya kwa sababu Rais Samia amefanya kazi kubwa na nzuri” amezungumza Mwalongo.

Nae Katibu wa UWT mkoa wa Njombe, Aziza Kiduda amesema ni wajibu wa viongozi wa UWT kwenda kuhamasisha wanawake kwenda kupiga kura kwa kuwa lengo ni kupata ushindi mkubwa.
“Ushindi wetu tunataka uwe wa kishindo utakaotikisa kwa kuwa sisi wanawake kwa idadi tuko wengi kwa hiyo tunatakiwa kuwa mbele kwenda kupiga kura” amesema Kiduda.

Nao baadhi ya wajumbe wa baraza la UWT wilaya ya Ludewa waliohudhuria kikao hicho akiwemo Agatha Kayombo wameshukuru uongozi ngazi ya mkoa kwa kufika wilayani humo na kutoa maelekezo ambapo wameahidi kwenda kufanyia kazi maelekezo hayo ili chama kiendelee kushika dola.
Mwandishi: Amiri Kilagalila
Mhariri: Dominic Allen


