Na Dominic Allen
Serikali ya Tanzania imetakiwa kulipa fidia ya kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni 70.9 kufuatia mgogoro ulioibuka baada ya kuchukua mali za mradi wa Wigu Hill za kampuni ya uchimbaji madini ya Montero Mining and Exploration Ltd ya Canada.
Mgogoro katika ya kampuni ya Montero na serikali ya Tanzania ulianza mwaka 2019 kufuatia hatua ya serikali ya Tanzania kuipokonya kampuni hiyo leseni ya uhifadhi ya madini ya mradi wa Wigu Hill baada ya kuchapishwa kwa Kanuni za Uchimbaji Madini mnamo Januari 10, 2018 ambazo zilifuta leseni zote za uhifadhi madini zilizotolewa awali.
Mnamo Januari 08, 2021 kampuni hiyo ilituma maombi ya usuluhishi katika Kituo cha Kimataifa cha Utatuzi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) kudai fidia kwa uharibifu wa unyakuzi wa mradi wa Wigu Hill uliyofanywa na serikali ya Tanzania, ambapo Januari 09, ICSID ilipitisha maombi hayo.
Rais na Mkurugenzi wa kampuni ya Montero, Dkt. Antony Harwood katika taarifa iliyotolewa na Montero mwaka Novemba 21, 2021 alisema kuwa waliamua kupeleka kesi hiyo ICSID baada ya kushindwa kuelewana na serikali ya Tanzania.
Mradi wa Wigu Hill wenye eneo la kilomita za mraba 15.14 uliopo karibu na mji wa Kisaki mkoani Morogoro ulianza kutekelezwa na kampuni ya Montero mwezi Machi 2008 chini ya leseni ya uchimbaji, kabla ya kupata leseni ya uhifadhi ya miaka mitano mwaka 2015.
Baada ya mvutano huo wa takriban miaka mitano, kampuni hiyo imefikia makubaliano ambapo serikali ya Tanzania itatakiwa kulipa fidia hiyo ya kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni 70.9 kwa awamu tatu kati ya mwezi Novemba 20, 2024 hadi Februari 28, 2025.
Mpaka sasa tayari serikali ya Tanzania imeshalipa kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni 31.5, huku ikitakiwa kulipa kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni 21 kabla ya Januari 31, 2025 na kumalizia malipo ya mwisho ambayo ni shilingi za Kitanzania bilioni 18.3 kabla ya Februari 28, 2025.
Kampuni ya Montero na serikali ya Tanzania walituma ombi la pamoja kusitisha kesi iliyokuwa ikisikilizwa katika Kituo cha Kimataifa cha Utatuzi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSDI), kwani tayari malipo ya awali yameshafanywa na Tanzania huku malipo mengine yakitakiwa kulipwa kama ilivyoafikiwa.
Kabla ya makubaliano haya ya sasa, kampuni ya Montero hapo awali ilikuwa inadai kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni 183.8.
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


