Na Dominic Allen
Mwanaharakati na mchoraji wa katuni maarufu nchini Kenya, Gideon Kibet maarufu kama ‘Kibet Bull’ na ndugu yake Ronny Kiplagat waliyotekwa wiki mbili zilizopita wamepatikana siku ya jana katika maeneo tofauti tofauti.
Kwa mujibu wa dada yao, Mercy Cherotich amesema kuwa siku ya jana majira ya saa 12 jioni Kibet aliwapigia simu na kuwajulisha kuwa ameachiwa huru na yupo salama.
“Tuna furaha sana, tumepokea simu kutoka kwa kaka yangu Gideon Kibet ameniambia yupo Vihiga, Magharibi mwa Kenya na yupo salama” alisema Cherotich.
Cherotich ameongeza kuwa Kibet hakuweza kumaliza mazungumzo kwenye simu kwani anaonekana hayupo sawa kisaikolojia.

Kwa upande wa Ronny Kiplagat, nae alipatikana hapo jana katika kaunti ya Machakos, ambapo Jeshi la Polisi nchini humo limethibitisha taarifa za kupatikana kwake.
Familia ya ndugu hao wawili imeishi na maumivu makali katika kipindi cha hivi karibuni tangu kutekwa kwa Ronny Kiplagat mnamo Disemba 21, 2024 wakati akihudhuria kanisani huko Ngong, Kajiado na Gideon Kibet aliyetekwa jijini Nairobi siku ya Krismasi Disemba 25, 2024 mara baada ya kumtembelea Seneta wa Busia, Okiya Omtata.
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


