Maendeleo ya wachimbaji wadogo wa madini Tanzania

Na Dr. Bravious Kahyoza

Sekta ya madini nchini Tanzania imeendelea kuwa mhimili muhimu wa uchumi, na katika kipindi cha miaka minne iliyopita, kumekuwa na mafanikio makubwa, hasa kwa upande wa wachimbaji wadogo wa madini.

Kwa muda mrefu, kundi hili lilionekana kutengwa kwenye mnyororo wa thamani wa rasilimali za madini, lakini tangu mwaka 2021 hali imebadilika kwa kasi kubwa, ambapo mapato ya wachimbaji wadogo yameripotiwa kuongezeka mara nne, mafanikio ambayo Serikali ya Awamu ya Sita inajivunia kama ishara ya mageuzi ya kisekta yenye tija kwa wananchi wa kawaida.

Waziri wa Madini, Mhe. Antony Mavunde mnamo mwezi Aprili 2024 akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/2025, alieleza kuwa katika mwaka wa fedha 2021/2022 ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kutoka sekta ya madini ulifikia Shilingi za Kitanzania bilioni 623, ambapo wachimbaji wadogo walichangia takriban asilimia 20 ya kiasi hicho, sawa na Shilingi za Kitanzania bilioni 124.6.

Hali hiyo ilidhihirisha kwamba licha ya kuwepo kwa wachimbaji wadogo katika maeneo mengi ya nchi, walikuwa bado hawajapewa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika uchumi rasmi wa sekta hiyo.

Sekta ya madini kwa ujumla, katika mwaka 2021, ilichangia asilimia 6.8 ya Pato la Taifa.

Katika kipindi cha miaka minne tangu kuingia madarakani kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Serikali imechukua hatua mbalimbali zilizolenga kuhuisha sekta ya madini, hasa kwa kuwainua wachimbaji wadogo.

Hatua hizi zikiwemo maboresho ya sera, kuimarishwa kwa mifumo ya usimamizi, na upanuzi wa masoko ya madini zimechangia ongezeko kubwa la mapato.

Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2025 zilizotolewa na Wizara ya Madini zimeonyesha kuwaSekta ya Madini kwa mwaka wa fedha 2024/25 ukusanyaji wa maduhuli umeongezeka hadi kufikia ya kiasi cha Shilingi za Kitanzania trilioni 1.063, ambapo wachimbaji wadogo wamechangia asilimia 40 ya kiasi hicho, sawa na Shilingi za Kitanzania bilioni 464.

Hii ni zaidi ya mara nne ya kiwango walichochangia mwaka 2021.

Pamoja na ongezeko hilo la mapato, mchango wa sekta ya madini kwa Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 6.8 hadi asilimia 10 ndani ya kipindi hicho hicho.

Kwa lugha nyepesi, madini yameendelea kuwa chanzo kikuu cha mapato ya Serikali, ajira na mitaji ya maendeleo kwa jamii.

Tanzania pia imepanda chati katika bara la Afrika, ikiwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa kasi ya ukuaji wa uchumi, sehemu kubwa ikichangiwa na mageuzi kwenye sekta ya madini.

Mafanikio haya yamejengwa juu ya misingi kadhaa, ikiwemo Serikalikuongeza idadi ya vituo vya ununuzi wa madini kutoka 61 mwaka 2020 hadi 109 mwaka 2025.

Hii imerahisisha upatikanaji wa masoko rasmi, kupunguza utoroshaji wa madini, na kuhakikisha wachimbaji wanapata bei yenye ushindani kupitia minada ya wazi.

Vilevile, masoko ya madini yameongezeka kutoka 41 hadi 43, hatua iliyoleta uhakika wa mapato na kuongeza ushindani wa kibiashara.

Serikali pia imeanzisha mifumo ya usimamizi wa sekta ya madini katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dodoma, Dar es Salaam, Geita na Chunya. Mfumo huu umelenga kuweka uwazi katika shughuli zote za uchimbaji, kuongeza ufuatiliaji wa mapato na kuondoa mianya ya rushwa. Kupitia mifumo hiyo, wachimbaji wadogo sasa wanapata leseni kwa urahisi zaidi, taarifa za soko kwa wakati pamoja na huduma za kitaalamu kuhusu afya na usalama wa kazi migodini.

Mbali na mifumo hiyo, Serikali pia imeimarisha Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa kulielekeza kushirikiana moja kwa moja na wachimbaji wadogo.

Kupitia STAMICO, wachimbaji hupatiwa mafunzo, msaada wa kitaalamu na pia msaada wa vifaa vya awali ili kuongeza ufanisi katika uzalishaji. Shirika hili limekuwa kiunganishi kati ya wachimbaji wadogo na taasisi za kifedha, hali iliyowasaidia baadhi ya wachimbaji kupata mikopo ya kuendeleza shughuli zao.

Mabadiliko haya yamekuwa na athari chanya kwa jamii, kwani kwa sasa wachimbaji wengi wanapata kipato cha uhakika, hali inayowawezesha kugharamia elimu ya watoto wao, huduma za afya na hata kuwekeza kwenye shughuli nyingine za kiuchumi.

Katika mikoa kama Geita, Shinyanga, Songwe, Mbeya na Mara, mapato kutoka kwenye madini yamechangia ongezeko la biashara ndogo ndogo, ujenzi wa nyumba bora, na hata kuibuka kwa miradi ya kijamii kama shule na vituo vya afya.

Aidha, ongezeko la mapato kwa wachimbaji wadogo limeongeza idadi ya ajira si tu kwa wachimbaji wenyewe, bali pia kwa maelfu ya watu wanaojihusisha na huduma za usafirishaji, uuzaji wa vifaa vya uchimbaji, upishi na usambazaji wa bidhaa kwenye maeneo ya migodi.

Mzunguko huu wa kiuchumi umeongeza kasi ya maendeleo ya mikoa inayotegemea madini kama nyenzo kuu ya uchumi wa wananchi wake.

Pamoja na mafanikio haya, bado kuna changamoto, ambapo wachimbaji wengi wadogo wanakabiliwa na upungufu wa teknolojia ya kisasa ya uchimbaji, hali inayopunguza uzalishaji na kuongeza hatari za kiafya.

Pia, mabadiliko ya bei ya madini katika masoko ya dunia yanaweza kuwaweka katika hatari ya kupata hasara kwa sababu ya kutokuwa na mifumo ya kinga dhidi ya kuyumba kwa soko.

Zaidi ya hayo, bado kuna idadi kubwa ya wachimbaji wadogo wanaoendesha shughuli zao bila kusajiliwa rasmi au bila kuwa na leseni.

Hata hivyo, kwa kuzingatia mafanikio yaliyopatikana hadi sasa, sekta ya wachimbaji wadogo wa madini inapaswa kupewa kipaumbele zaidi.

Serikali inayo nafasi ya kuendeleza mafanikio haya kwa kuongeza urasimishaji, kuimarisha elimu ya wachimbaji, kutoa motisha kwa taasisi za kifedha kushirikiana nao, na kuhakikisha miundombinu ya msingi inafika maeneo ya migodi.

Ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wachimbaji wenyewe unaweza kuwa kichocheo kikubwa cha kukuza sekta hii kwa miaka ijayo.

Mageuzi yanayoendelea katika sekta ya madini yanaonesha wazi dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuifanya rasilimali hii kuwa chanzo cha ustawi wa watu wa kawaida.

Ongezeko la mapato kwa wachimbaji wadogo kutoka Shilingi bilioni 124.6 mwaka 2021 hadi Shilingi bilioni 464 mwaka 2025 linaashiria mafanikio makubwa na fursa pana za maendeleo endelevu ikiwa juhudi hizi zitaendelezwa.

Mwandishi: Dr. Bravious Kahyoza
Mhariri: Dominic Allen

Hot this week

Mnyonge, mnyongeni ila haki yake mpeni

By Dorlingson Edward Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), leo...

CHADEMA kutoa msimamo wake kuhusu maridhiano

By Veronica Mlyatu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa...

Popular Articles

Safari ya Mashimba katika kutetea jamii ya Wahadzabe

Nchini Tanzania  kuna jumla ya makabila zaidi ya 120...

Polisi waendelea kuwashikilia viongozi wa CHADEMA

Ni siku ya kwanza tangu kukamatwa kwa viongozi wa...

Siku ya Vijana Duniani.

Kwa sasa ni kijana wa miaka 25 ambaye amejiajiri...

BWAWA LA ARBA’AT  LASABABISHA MAAFA NCHINI SUDAN

Watu 30 mashariki mwa Sudan na na wengine 60...

Sand Mining in Tanzania: Trails of Destruction in Lake Victoria and its Environs

By Dominic Allen On November 14th, 2021 in the Geita...

 Utekaji: Fumbo linalotushinda?

Na Yohani Gwangway Taifa la Tanzania kwa miaka mingi limekuwa...

Abduction: Is it a riddle we can’t solve?

By Yohani Gwangway For many years Tanzania has been an...

Mustakabali wa Hewa Safi kwa kila kiumbe

Na Dominic Allen Msingi wa maisha ya viumbe hai yaani...
LAND DWELLERS FACT CHECK HUB VERIFY FACTS STOP MISINFORMATION Trusted Fact-Checking in Tanzania Beyond What You Know VERIFY NOW

Related Articles

Popular Categories

DWELLERS CHECK-HUB Verify Facts. Stop Misinformation Trusted Fact-Checking in Tanzania • Beyond What You Know VERIFY NOW