Na Dominic Allen
Kundi la G55 limetangaza rasmi kujitoa katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa uongozi wa sasa chini ya Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Lissu, wakisema kuwa miongoni mwa mambo mengine mengi, pia kuna ubaguzi dhidi yao ndani ya chama hicho.
Msimamo huo wa kujitoa CHADEMA umetolewa leo na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Bara, Benson Kigaila wakati kundi hilo lilipofanya mkutano na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, ambapo ameeleza kuwa wanachama waliokuwa wanamuunga mkono Mwenyekiti wa zamani wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe kwenye uchaguzi wa ndani hicho uliyomalizika mwezi Januari 2025, wamekuwa wakibaguliwa na kuitwa wasaliti, jambo ambalo sio sawa.
“Wanachama ambao wanaitwa ni timu ya Mbowe wanabaguliwa kuanzia kwenye Kamati Kuu mpaka kwenye misingi. Kila mtu anayejulikana anamuunga mkono Mbowe anaitwa msaliti” amesema Kigaila.
Kigaila amesema kuwa hawawezi kuendelea kuwa wanachama wa chama ambacho maamuzi yake hayafanywi kwa vikao, wala katiba yake haifuatwi.
“Sisi tumeamua wote pamoja tunajiondoa CHADEMA, ili tuwaachie hicho chama waendeshe wanavyotaka” ameongeza Kigaila.
Miongoni wa waliyojitoa CHADEMA ni pamoja na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Bara, Benson Kigaila, Salum Mwalimu, (alikuwa Naibu Katibu Mkuu Zanzibar), Catherine Ruge (alikuwa Mtalamu wa Dawati la Jinsia), Julius Mwita pamoja na John Mrema (alikuwa Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje) ambaye tayari alishavuliwa uanachama.
Kwa upande wake Salum Mwalimu ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Zanzibar, amekosoa kampeni ya ‘No reforms, No election’ akisema kuwa chama hicho hakiwezi kuendeshwa kwa kampeni hiyo peke yake.
“Hiki chama kitaendeshwa na “No reforms, No election’ peke yake?… Nini kinafuata baada ya mwezi Novemba?…Hakuna chochote kinachoendelea ndani ya chama” amehoji Mwalimu kuhusu mkakati wa CHADEMA mara baada ya uchaguzi kupita.
Mwalimu ameeleza kuwa ameitumikia CHADEMA kwa miaka 17 hivyo anawashangaa wanaosema kuwa anatumika kukivuruga chama hicho kwa kuwa na mtazamo tofauti na chama.
“Wanakidondosha chama hiki kwa makusudi, kutengeneza ubinafsi, wachache kumiliki nguvu, kujipa mamlaka, kujipa uhalali wa mbele ya umma kwamba wao wakisema ndiyo waaminike” ameongeza Mwalimu.
Salum Mwalimu ametilia shaka mwelekeo wa sasa wa CHADEMA, akisema kuwa hakina dira wala nguvu ya kitaasisi.
“Lakini ukweli ni kwamba CHADEMA imepoteza muelekeo, CHADEMA imepoteza dira, CHADEMA imepoteza nguvu ya kitaasisi, CHADEMA imepoteza umoja wa kuhakikisha kwamba inasimamia inachokiamini” ameeleza Mwalimu.
Nae Catherine Ruge ambaye alikuwa ni Mtalamu wa Dawati la Jinsia kabla ya kuondolewa katika nafasi hiyo, na mwanachama wa CHADEMA tangu mwaka 2010, amesema kuwa chama hicho kimewajaza hofu wananchi kupitia kampeni yake ya ‘No reforms, No election’.
“Badala ya chama kubuni mbinu mpya na mapambano mapya ya namna mpya ya namna ya kuikabili CCM, imeamua kuwajaza hofu wananchi kutoshiriki uchaguzi, lakini wakati huo huo inawashawishi wananchi kuzuia uchaguzi” amezungumza Catherine Ruge.
Catherine pia amesema kwa sasa anaona CHADEMA imekosa dira na uelekeo, licha ya ushauri ambao Kundi la G55 liliutoa kwa chama hicho kuhusiana na kampeni ya ‘No reforms, No election’.
Hata hivyo Emmanuel Ntobi, ambaye pia ni mmoja wa Kundi la G55 hii leo kupitia mtandao wa X amekanusha kuhama CHADEMA, akisema kuwa yeye ni mwanachama halali na bado yupo ndani ya chama hicho.
“Napenda kuchukua fursa hii kuwajulisha rasmi kwamba mimi, Emmanuel Ntobi, bado ni mwanachama halali wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), na sijawahi wala sina nia ya kujiondoa katika Chama hiki” ameandika Ntobi.
Emmanuel Ntobi ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Shinyanga ameeleza kuwa ataendelea kuwa mwanachama mtiifu, akiamini katika misingi, itikadi, na malengo ya CHADEMA kama chama kinachopigania haki, usawa pamoja na maendeleo ya kweli kwa Watanzania wote.
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


