Na Amiri Kilagalila
Mkuu wa wilaya ya Makete mkoani Njombe, Kissa Kasongwa amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi wilaya hiyo Mrakibu Mwandamizi, Assel Mwampamba, pamoja na Mshauri wa Jeshi la Akiba kukagua kampuni zote za ulinzi ili kubaini wale wote ambao hawajapitia mafunzo ya Jeshi la Akiba waondolewe.
Ametoa agizo hilo jana Mei 30, 2025 wakati akifungua mafunzo ya mgambo yanayofanyika katika Kata ya Tandala wilayani Makete, ambapo amesema watu wote waliopitia katika mafunzo ndiyo wawekwe kwenye kampuni za ulinzi huku akitaka ukaguzi huo ufanyike ndani ya siku 14 kuanzia sasa.
“OCD na ofisi yako mfanye ‘vetting’ je, hawa watu wanaolinda wamepitia kwenye mafunzo? Isije kuwa tuna watu wasiokuwa na mafunzo wapo kwenye maeneo nyeti. Lakini fursa yoyote ningependa sana sana sisi kama serikali tuweze kuwafikiria kwanza hawa vijana wenye mafunzo ya jeshi la akiba” amesema DC Kasongwa.

“hatuna nchi nyingine zaidi ya Tanzania, tusome tuyaelewe mafunzo vizuri huku tukitambua amani ndio nguzo yetu ya kwanza katika kuongeza ustawi wa taifa letu lakini tusisahau kuwa wakakamavu” ameongeza DC Kasongwa.
Imani Sanga ambaye ni miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo ameshukuru, akisema kuwa wapo tayari kwa mafunzo mpaka watakapohitimisha na kuiomba serikali kuwanunulia sare pindi watakapohitimu, jambo ambalo limeungwa mkono na Mkuu wa wilaya, Kissa Kasongwa na kiahidi kuchangia sehemu ya gharama ya mavazi.
“Tunamorali sana na tupo tayari kwa mafunzo na kujenga taifa letu, ila ombi letu tu serikali itusaidie upande wa sare” amesema Sanga.

Nae Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Tandala, Altin Sanga amesema kuwa watashirikiana kuona namna ya kuongeza idadi ya washiriki wa mafunzo hayo.
Kwa upande wake Diwani wa Kata Tandala, Daniel Hatanaka ameeleza kuwa mafunzo ya sasa ni ya muda mfupi na yameboreshwa zaidi kuliko kama ilivyokuwa zamani.
Mwandishi: Amiri Kilagalila
Mhariri: Dominic Allen


