Nchini Tanzania kuna jumla ya makabila zaidi ya 120 hadi 125, lakini kabila linalofahamika kwa jina la Hadza au wahadzabe limekuwa maarufu kwa namna yake ya kipekee katika kutumia lugha za sauti za “bonyezo” au “marudio” (clicks). Ingawa hapo awali wataalamu walidhani ina uhusiano na lugha za Khoisan za Kusini mwa Afrika, japokuwa tafiti za sasa zinaonesha kuwa Kihadzabe hakina uhusiano na lugha nyingine yoyote duniani
Kutana na Edward Mashimba ambaye ni Mwenyekiti wa jamii ya Wahadzabe mkoa wa Singida nchini Tanzania, akitokea kijiji cha Munguli, kata ya Mwangeza, iliyopo Mkalama. Katika jamii hii ambayo viongozi mara nyingi hupatikana kwa uwezo wao mkubwa wa kuwinda, kusuluhisha migogoro, kuaminiwa ama hata kupewa heshima na jamii yake, lakini safari yake uongozi ilipatikana kwa njia tu ya kuaminiwa.
Kijiji cha Munguli kinajulikana sana kwa kuwa moja ya maeneo ya asili yanayokaliwa na jamii ya wawandaji na waokotaji ya Wahadzabe kwani eneo hilo lina msitu wa jamii unaolindwa ili kulinda utamaduni na mfumo wa ikolojia wa Wahadzabe dhidi ya uharibifu wa mazingira, uvamizi wa mifugo, na kilimo kisicho endelevu. Jamii yake ilimkabidhi hatamu za uongozi wa serikali ya kitongoji kwa miaka 15, kabla ya kumvua kofia hiyo na kumvika taji kubwa zaidi la kuwa kiongozi wa kimila na jamii ya Wahadzabe kutokana na kuaminiwa kwake ambapo kwa sasa ana miaka takribani 20 kuwa kiongozi wa jamii nzima ya Wahadzabe.
Katika ulimwengu wa sasa ambao unakumbana na changamoto ya taarifa za upotoshaji, Mashimba ni Balozi wa mradi wa Dwellers Check Hub, aliyeshiriki katika mafunzo ya mradi huu unaotekelezwa na Land Dwellers na Shirika la International Media Support (IMS), ambapo unajikita katika kupambana na taarifa za upotoshaji kuhusu jamii za asili na mazingira nchini Tanzania.
Mafunzo ya mradi huu ambao unafadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) na Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania, yamempa kiongozi huyu uwezo wa kuwa msemaji mkuu wa jamii yake, akihakikisha ukweli wa utamaduni wao unalindwa dhidi ya taarifa za upotoshaji kuhusu jamii za asili, ikiwemo Wahadzabe
Mashimba alizaliwa mwaka 1996 katika msitu wa pori la Wahadzabe huko Munguli mkoani Singida. Mzee huyu mwenye umri wa miaka 60 anabeba mzigo mzito kwani ana jukumu la kuwaongoza watu wake katika ulimwengu wa kisasa unaobadilika kwa kasi, kulinda utamaduni wa jamii yake usipotee kabisa.
Akiwa amekumbana na changamoto mbalimbali katika maisha yake, ikiwemo kutokuwa na elimu, Mashimba ni mfano hai wa changamoto za kijamii zinazowakabili Wahadzabe. Hakuwahi kukanyaga darasani. Safari yake ya elimu iliishia ukingoni kabla hata haijaanza, baada ya wazazi wake kuamua kuhamia ndani zaidi porini kufuata mtindo wao wa maisha wa kuhamahama.

Hata hivyo, kutokuwa na cheti hakukumzuia kuwa mwerevu. Kupitia mwingiliano wake wa kila siku na watu wa nje, Mashimba alijifunza lugha ya Kiswahili kwa kusikiliza na kusoma kutoka kwa wengine. Leo hii, anajivunia uwezo wake mkubwa wa kuelewa na kuzungumza lugha hiyo ya Kiswahili japo si katika kiwango kile kikamilifu kinachotakiwa,” anakiri kwa unyenyekevu.
Katika safari ukuaji wake, Mashimba alieleza kuwa changamoto kuu ambayo ilikuwa ikimkumba na bado inaikumba jamii yake ya wahadzabe ni changamoto ya mawasiliano (lugha) kutokana na mtindo wao wa utamkaji wa maneno hivyo si rahisi kuelewana kwa uharaka na makabila mengine kama yanawazunguka . Kutokana na changamoto alizopitia, Mashimba amekuwa mpiganaji mkuu wa elimu kwa watu wake.
“Natamani kuona jamii yangu inaelimika kama jamii zingine za asili nchini Tanzania,”alisema Mashimba.
Asili ni asili tu, licha ya uongozi wake, Mashimba bado anaingia porini kuwinda. Katika utamaduni wa Kihadzabe, uwindaji ni wajibu wa mwanaume tangu ujana hadi uzee. Hakuna ‘kustaafu’; iwe umesoma au la, lazima mwanaume ashiriki kupata kitoweo cha nyama, asali safi huku wanawake wakikusanya matunda pori na kucimba mizizi inayotumika kama chakula.
Hadzabe au Wahadzabe ni moja ya makabila ya kale zaidi duniani yanayopatikana nchini Tanzania, katikati na kaskazini mwa Tanzania, karibu na Bonde la Ziwa Eyasi. Wanaaminika kuishi katika eneo hili kwa miaka mingi bila kubadilisha mfumo wao wa maisha, huku wakitajwa kuwa miongoni mwa jamii za asili duniani zinazoishi kwa kutegemea mfumo wa kuwinda na kuokota matunda.


