Taarifa za upotoshaji: Tishio kwa maisha, utamaduni na haki za jamii za asili

Na Dominic Allen

Mtu anaweza kuishi maisha yake yote ndani ya jamii, akijua mila, desturi na mfumo wa maisha wa watu wake, lakini siku moja akakutana na taarifa inayomweleza yeye na jamii yake kwa namna ambayo haijawahi kuwa sehemu ya maisha yao. Taarifa hiyo ikirudiwa mara kwa mara, inaweza kuanza kuaminika na watu walio nje ya jamii, huku wale wanaozungumziwa wakibaki na mzigo wa kueleza ukweli kuhusu maisha yao. Hii ni moja ya changamoto inayowakabili jamii za asili nchini Tanzania, ambazo zimekuwa zikikumbana na taarifa za upotoshaji kuhusu tamaduni zao, maisha yao, uhusiano wao na mazingira na namna wanavyotumia maeneo yao.

Katika kutambua jamii za asili, mnamo Desemba 23, 1994, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kupitia Azimio Na. 49/214 liliamua Agosti 09 kila mwaka kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Watu wa Jamii za Asili, ambapo siku hii huweka nafasi ya kutambua mchango wa jamii za asili, pamoja na changamoto zinazowakabili katika kulinda utamaduni, maisha na maarifa yao.

Wakati tukiadhimisha siku hii leo Agosti 09, 2026, kauli mbiu ya mwaka huu ni “Kuwaheshimu wakunga wa asili: Kulinda maisha na ustawi,” ikiweka mkazo kwenye heshima na ulinzi wa maarifa yanayotokana na jamii za asili, ikiwemo maarifa yanayohusiana na afya, maisha na ustawi wa jamii.

Hata hivyo, pamoja na utajiri huo wa maarifa na tamaduni, jamii hizi ikiwemo Wamasai, Wadatoga, Wahadzabe pamoja na Waakie, zimekuwa zikikumbana na taarifa za upotoshaji kuhusu maisha yao, jambo ambalo limekuwa likiwaathiri kwa namna moja au nyingine.

Itakumbukwa kuwa miaka michache iliyopita, Deodatus Balile, mwandishi wa habari mkongwe nchini Tanzania na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), alinukuliwa akisema kuwa jamii ya wamaasai huwa hawana desturi ya kuzikana, badala yake maiti au mgonjwa ambaye hana dalili ya kupona, huachwa ili aliwe na wanyama wakali kama vile fisi.

Kwa Lanyor Kuya, mwanaharakati wa haki za binadamu kutoka jamii ya Wamasai, taarifa kama hizo si jambo jipya, akisema kuwa baadhi ya taarifa kuhusu jamii za asili zimekuwa zikitolewa na watu ambao hawana uhalali wa kuzungumza kwa niaba ya jamii hizo.

“Taarifa ambazo zimekuwa zikitolewa na watu ambao sio sahihi kutoka ndani ya jamii wakitusema. Kwa mfano, kuna masuala yalikuwa yanasemwa na baadhi ya waandishi waliowahi kupelekwa Ngorongoro, kwenda kutoa taarifa, mpaka wanasema hatuzikani. Lakini vilevile, kuna habari zingine kwamba watu wanauawa na wanyama,” amezungumza Kuya.

Katika jamii za asili ambazo historia, mila na maarifa hupitishwa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine, taarifa za upotoshaji zinaweza kuathiri namna watu wa nje wanavyozitazama jamii hizo, ambapo wakati mwingine zinaweza kuathiri hata namna wanajamii wenyewe wanavyohusishwa na maamuzi yanayowagusa.

Moja ya maeneo ambayo yamekuwa yakihusishwa na jamii za asili, ni pamoja na uharibifu wa mazingira, jambo ambalo watu wa jamii za asili pamoja na watetezi wa haki za binadamu wamekuwa wakipinga.

“Hizo ni propaganda ambazo tumezizoea, zikitumika, wanaweza kutumia propaganda za kuharibu misitu, kuongezeka kwa watu na makazi, ongezeko la mifugo. Kwa hiyo, hizo ni propaganda, fisi akitaka kuwala watoto wake, ni lazima atawatungia majina mabaya,” amesema Kuya.

Sijakida Nanida, ambaye ni Mdatoga na Diwani wa Viti Maalum kutoka Tarafa ya Ngorongoro, anasema kuwa wakati mwingine hata baadhi ya taarifa zinazotolewa kuhusu idadi ya watu wa jamii za asili katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro hazilingani na anachokiona kama mwanajamii.

“Wakati mwingine sisi tunaambiwa labda Ngorongoro watu wamezidi, lakini mimi ninayetokea katika jamii ya Wadatoga, naona sio kweli. Kwa sababu serikali wangejaribu kutembea na kuona kwa macho, kuna maeneo mengine ni makubwa, ambayo sisi tunasema bado kuna haja ya watu kuendelea kuishi katika maeneo yao,” amezungumza Sijakida.

Sijakida anasema kuwa taarifa za upotoshaji kuhusu jamii za asili zimekuwa zikiwaathiri na kuwadhalilisha, akizungumzia taarifa ya kwamba hawana desturi ya kuzikana.

“Zinatuathiri, ni udhalilishaji, kwa sababu jamii zetu za kifugaji ikiwemo wamaasai, wadatoga, mtu anapofariki ni lazima ahifadhiwe kaburini. Wakati mwingine kuna wakati sasa kuna kuenzi, kama wa wa jamii zingine wanavyoenzi miaka mitano ya babu zao, hata sisi tinakuwa na kaburi kwa sababu ya kuenzi mababu zetu,” masikitiko ya Sijakida.

Kwa Sijakida, tatizo linatokea pale taarifa zinapotolewa na kupokelewa na jamii bila kufanyiwa uhakiki wa kutosha, “Mimi nafikiri kinachotakiwa kufanyika, watu wasichukue taarifa kwa kusikia, natamani jamii wafikiwe na waelimishwe kuhusiana na hali hiyo. Naomba basi serikali au watu wengine wanaohusika na hizo taarifa, ukusanyaji wa data, tunatamani wawafikie jamii na kupokea taarifa halisi, kuliko kutumia taarifa ya kufikia.”

Kauli yake inaingia kwenye swali kubwa kuhusu namna taarifa kuhusu jamii za asili zinavyokusanywa. Nani anazungumza? Nani anasikilizwa? Na ni kwa kiwango gani watu wanaoishi ndani ya jamii wanapewa nafasi ya kueleza maisha yao?

Rispa Joseph, akitokea jamii ya Wamasai na mkazi wa Wilaya ya Monduli mkoani Arusha, anazungumzia baadhi ya taarifa za upotoshaji ambazo wamekuwa wakikumbana nazo.

“Habari za upotoshaji ambazo tunakumbana nazo sana kuhusu jamii yetu, labda Wamasai wanachapa wake zao sana, au kwamba mwanamke wa kimaasai ni mtu ambaye haruhusiwi kutoka nyumbani, ni wa kukaa tu kuelea familia, ambavyo kwa sasa sivyo ilivyo,” amesema Rispa.

Kwa mtu anayesemwa kwa jambo ambalo sio la kweli, madhara yake yanaweza kuonekana kwenye maisha ya kawaida. Rispa anaeleza kuwa taarifa hizo zimekuwa zikimwathiri yeye na wengine kisaikolojia.

“Imekuwa ikituathiri kisaikolojia, kwamba unasemewa kitu ambacho sio. Kwa hiyo, inatuathiri kisaikolojia,” ameeleza Rispa.

Mwandishi wa habari za mazingira na jamii za asili, Yohani Gwangway (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na vijana wa jamii ya Wahadzabe katika moja ya sherehe za kitamaduni.

Eliud Letunga, mtaalamu wa mazingira na bioanuai kutoka jijini Arusha, anasema kuna upande wa jamii hizi za asili ambao mara nyingi huwa haupewi nafasi.

“Ukweli ambao haubainishwi ni kwamba jamii hizi wamekuwa na mchango mkubwa kwenye uhifadhi wa mazingira na utunzaji wa bioanuai popote wanapokuwa… Ukiangalia kwa mfano kwa jamii ya wahadzabe, kuna mtazamo hasi ambao umejengeka dhidi yao, kwamba wao kazi yao ni kuwinda, ni kula wanyama na vitu kama hivyo, lakini ukweli ambao hatuambiwi ni kwamba jamii kabla kuwinda, huwa inafanya tathmini, sio kila mnyama anawindwa. Kwa mfano wakimuona mnyama ambaye ana mimba, hawawezi kumuwinda,huyo wanamuacha na kutafuta mnyama ambaye hana mimba,” ameeleza Eliud.

Eliud anaeleza kuwa uhusiano kati ya ufugaji na mazingira pia unahitaji kuangaliwa kwa upana nchini Tanzania, akisisitiza kuwa jamii Wamasai ni watunzaji wa mazingira, huku wakitumia njia za asili.

“Wamasai wenyewe kwa asili, maisha yao yanategemea ufugaji kwa asilimia kubwa. Lakini, mtazamo hasi uliyopo ni kwamba, ufugaji umekuwa ukiharibu mazingira, kitu ambacho si kweli, isipokuwa tunasema ufugaji unaozidi kwenye eneo moja ndiyo unaweza kuharibu mazingira…Lakini, kimsingi jamii ya wamaasai pia wanatunza mazingira, ndiyo maana ukienda Ngorongoro wamaasai wameweza kuishi na wanyama kwa miongo au kwa karne nyingi,” ameongeza Eliud.

Kwa mujibu wa Eliud katika shughuli ya ufugaji, matumizi ya ardhi kwa jamii ya Wamasai yana mifumo yake kulingana na misimu, “Wamaasai wa asili kabisa kwenye maeneo yao ukiwakuta, miaka yote wamekuwa na kitu kinaitwa mpango bora wa matumizi ya ardhi. Wanajua kipindi cha kiangazi tuchunge wapi, kipindi cha masika tuchunge wapi. Hii inaondoa ile kutumia eneo kwa muda mrefu na kumaliza uoto wa asili au kuua bioanuai iliyopo pale.”

Maarifa hayo yanapopuuzwa, suala la taarifa za upotoshaji linaweza kuingia kwenye eneo la maamuzi, ambapo anaeleza kuwa kutokuheshimu mipango ya jamii kunaweza kuchangia migogoro ya ardhi kati ya jamii za asili na watu wengine wanaotaka kutumia maeneo hayo kwa shughuli mbalimbali.

“Njia mojawapo inayoathiri, ni kuleta mgongano wa kimaslahi. Kwa sababu, utaratibu wa watunga sera kimsingi huwa hatuheshimu ile mipango iliyopo kwenye jamii, na hiyo inaleta migorogoro mikubwa kati ya jamii za asili, kama wamaasai na wanaoitwa wawekezaji. Kwa sababu unapomleta mwekezaji, utachukua kipande kile kile cha ardhi ambacho mimi ninaweza kukiona pori, watunga sera au wataalamu wengine wanaweza kukiona kama ni pori, lakini kimsingi ni maeneo ya malisho ya wafugaji. Kwa hiyo, inapelekea kuanza kuwa na msuguano na jamii za asili zilizopo kwenye eneo husika,” amesema Eliud.

Athari za taarifa za upotoshaji zimeonekana katika maisha ya watu wa Ngorongoro, ambako Lanyor Kuya anasema kuwa huduma za kijamii bado hazijatengamaa hadi sasa.

“Tunapata madhara makubwa, mosi, tumeona madhara ya kutokupatikana kwa huduma za kijamii ndani ya eneo la Ngorongoro, na hata mpaka leo huduma hazijarejea vizuri kama ilivyokuwa awali…Bado kuna makatazo kadha wa kadha ambayo yamewekwa… Suala la malisho ni taabu, suala la mtu kujenga nyumba bado ni taabu,” amezungumza Kuya.

Hata hivyo, kutoa elimu kwa jamii kunatajwa kuwa sehemu ya mwarobaini katika mapambano dhidi ya taaifa za upotoshaji, “Tunapaswa kutoa elimu kwa jamii, ili waweze kupambana…Nitoe wito kwa jamii ya Wanangorongoro na wanaharakati, watetezi wote wa haki za binadamu, Watanzania wapenda haki na dunia kwa ujumla wasimame pamoja nasi.”

Rispa naye anaona elimu ikiwa muhimu katika kukabiliana na taarifa hizo, wito wake akiuelekeza kwa serikali, “Serikali itoe elimu kwa jamii kuhusiana na taarifa za upotoshaji kuhusu jamii za asili.”

Eliud Letunga anaona mabadiliko yanapaswa kuanzia kwenye mtazamo wa jamii na namna vyombo vya habari vinavyowasilisha taarifa kuhusu watu wa jamii za asili.

“Tubadilishe mtazamo, huu mtazamo hasi hatupaswi kuwa nao, kuanzia kwa vyombo vya habari ni sehemu mojawapo muhimu sana ambapo tunatakiwa kuwekeza kuelimisha jamii iliyopo nje. Pili, wafanya maamuzi waweze kuwa na mtazamo wa kwamba hizi jamii zinapaswa kuwepo. Tujiulize swali dogo, baada ya miaka 100 ijayo, kama tutaendelea kuwasukuma hawa jamii za asili, si ajabu hatutakuwa na jamii za wahadzabe, lakini pia hatutakuwa na wafugaji wa asili, kwa hiyo kuna haja ya kubadilika,” ameshauri Eliud.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, mnamo Machi 12, 2026 akipokea Ripoti kutoka kwa Jaji Dkt. Gerald Ndika, Mwenyekiti wa Tume ya kutathmini masuala yanayolalamikiwa na wakazi wa wilaya ya Ngorongoro. Picha: Ikulu.

Akisisitiza kuwa tafiti zaidi zifanyike ili kuelewa mchango wa jamii za asili na maarifa yaliyopo ndani yao, “Asasi za kiraia nazo tuendelee kufanya tafiti mbalimbali, lakini pia tuhamasishe jamii kuweza kutambua mchango wa hizi jamii asili kwa maana ya kutambua mfumo wao wa maisha. Ukirudi kwenye hizi jamii za asili utagundua kuna tiba asilia ambazo ni bora, ambapo tunapaswa kurithi sasa hayo maarifa kuyapitisha kwenye jamii zingine.”

Na kwa upande wa sheria, anasema kuwa kuna haja ya kuwa na utambuzi maalum wa kisheria kuhusu jamii za asili pamoja na maeneo yao, “Tuwe na sheria mahususi ambayo inatambua watu au jamii za asili na mfumo wao wa maisha. Kwa mfano, tutambue wahadzabe na eneo lao lilindwe.”

Taarifa kuhusu jamii za asili zinahitaji utafiti, uthibitisho na nafasi kwa watu wenyewe kueleza maisha yao. Vyombo vya habari, serikali, watafiti na wadau wengine wanapaswa kuhakikisha taarifa zinazowafikia wananchi hazijengi mtazamo wa uongo kuhusu mila, utamaduni, mazingira na mifumo ya maisha wa jamii hizi.

Hivyo, kuna haja ya kubadilisha mtazamo na kutambua mchango wa jamii za asili katika uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya jamii. Heshima kwa jamii hizi inaanza pale sauti zao zinaposikilizwa, taarifa zao zinapothibitishwa na maarifa yao yanapotambuliwa na kulindwa.

Mwandishi: Dominic Allen

Mhariri: Yohani Gwangway

Hot this week

Mnyonge, mnyongeni ila haki yake mpeni

By Dorlingson Edward Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), leo...

CHADEMA kutoa msimamo wake kuhusu maridhiano

By Veronica Mlyatu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa...

Popular Articles

Safari ya Mashimba katika kutetea jamii ya Wahadzabe

Nchini Tanzania  kuna jumla ya makabila zaidi ya 120...

Polisi waendelea kuwashikilia viongozi wa CHADEMA

Ni siku ya kwanza tangu kukamatwa kwa viongozi wa...

Siku ya Vijana Duniani.

Kwa sasa ni kijana wa miaka 25 ambaye amejiajiri...

BWAWA LA ARBA’AT  LASABABISHA MAAFA NCHINI SUDAN

Watu 30 mashariki mwa Sudan na na wengine 60...

Sand Mining in Tanzania: Trails of Destruction in Lake Victoria and its Environs

By Dominic Allen On November 14th, 2021 in the Geita...

 Utekaji: Fumbo linalotushinda?

Na Yohani Gwangway Taifa la Tanzania kwa miaka mingi limekuwa...

Abduction: Is it a riddle we can’t solve?

By Yohani Gwangway For many years Tanzania has been an...

Mustakabali wa Hewa Safi kwa kila kiumbe

Na Dominic Allen Msingi wa maisha ya viumbe hai yaani...
LAND DWELLERS FACT CHECK HUB VERIFY FACTS STOP MISINFORMATION Trusted Fact-Checking in Tanzania Beyond What You Know VERIFY NOW

Related Articles

Popular Categories

DWELLERS CHECK-HUB Verify Facts. Stop Misinformation Trusted Fact-Checking in Tanzania • Beyond What You Know VERIFY NOW