CHADEMA yarejea ulingoni: Karata turufu mkononi

Na Dominic Allen

Aprili 15, 2026, Mahakama ya Rufaa Dodoma iliondoa zuio la kufanya shughuli za kisiasa dhidi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), uamuzi ambao unafungua ukurasa mpya wa matumaini kwa chama hicho, lakini pia umejaa maswali mazito kuhusu mustakabali wa demokrasia nchini Tanzania.

Kwa karibu mwaka mmoja, CHADEMA ilikuwa nje ya uwanja rasmi wa siasa baada ya Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam kuweka zuio kwa chama hicho kufanya shughuli za kisiasa mnamo Juni 10, 2025, katika kesi ya mgawanyo wa mali iliyofunguliwa na aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Zanzibar, Said Issa Mohamed pamoja na wenzake wawili dhidi ya Bodi ya Wadhamini na Katibu Mkuu wa chama. Lakini sasa, baada ya kushinda rufaa, chama hicho kinarejea tena kwenye uwanja wa siasa.

Kwa baadhi ya viongozi na wanachama wa CHADEMA, wamegubikwa hisia mchanganyiko, yaani ushindi lakini pia kujeruhiwa. Mkuu wa Idara ya Habari na Uenezi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Gervas Lyenda anaeleza wazi kuwa kilichotokea hakikuwa tu suala la kisheria bali ni ukiukwaji wa haki za msingi.

“Tukalalamika kwamba Jaji Mwanga hakutenda haki kutoa hukumu hii ya kukiumiza chama, na unawezaje kutoa hukumu hii ya kusimamisha shughuli za chama kwa maslahi ya watu watatu waliofungua kesi?…Tukaona hii kitu sio haki, kufanya siasa ni haki ya kikatiba, unapomzuia mtu kufanya siasa, umemnyima hata haki yake ya kikatiba.”

Kauli hiyo inaweka msingi wa mjadala mpana zaidi, je, uamuzi wa Mahakama ya Rufaa Dodoma unafuta kabisa doa lililoachwa na uamuzi wa awali wa Mahakama Kuu? Lyenda anasisitiza kuwa hakuna sababu ya kuipa Mahakama ya Rufaa sifa, akisema, “Ukiwasikiliza watu, kuna wanaoishukuru Mahakama kwamba imetenda haki. Kwangu mimi hatuna haja yoyote ya kuipa utukufu Mahakama ya Rufaa kwa kuturejeshea haki yetu. Mahakama ya Rufaa, yote ni Mahakama ya Tanzania, ipo kwenye mhimili mmoja. Kuipa utukufu Mahakama ya Rufaa, wakati kwenye Mahakama hiyo hiyo kwenye ngazi zake za chini ilituumiza sioni kama ni sawa sawa.”

Kuhusu sababu zilizochangia kuondolewa kwa zuio hilo, Mkurugenzi wa Mafunzo, Oganaizesheni na Uchaguzi wa CHADEMA, John Pambalu anaona kuwa shinikizo kutoka kwa jumuiya ya kimataifa, pamoja na taasisi mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi yamechangia pakubwa, “Tanzania haiwezi kuwa kisiwa, pamekuwa na kelele nyingi kutoka Jumuiya ya Ulaya, Umoja wa Mataifa, Taasisi za haki za binadamu kama Amnesty International, nchi marafiki, na shinikizo kubwa sana kutoka kwa watu wema wa ndani ya mipaka ya Tanzania, vyama vya siasa, asasi za kiraia, madhehebu ya kidini yanayojielewa…yamekuwa mstari wa mbele kupigania haki ya watu kukutana na kusema wazi wazi kuwa CHADEMA inaonewa kuzuiwa kufanya shughuli zake za kisiasa.”

Baadhi ya viongozi na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Magharibi wakishiriki kufanya usafi katika Ofisi za Kanda za chama hicho mkoani Tabora, Aprili 16, 2026, baada ya uamuzi wa Mahakama ya Rufaa Dodoma. Picha: CHADEMA

Kwa upande wake mchambuzi masuala ya siasa nchini Tanzania, Juma Mudimi amesema zuio lililowekwa hapo awali na Mahakama Kuu linaweza kuwa limeipa CHADEMA nguvu zaidi, akieleza kuwa katika mitazamo ya wananchi walio wengi hatua iliyochukuliwa dhidi ya chama hicho ilitafsiriwa kama kuonewa.

“Ukipima namna ambavyo watu wanakipokea na kukizungumza katika mitandao ya kijamii unaona hili suala limekiimarisha zaidi, kwa sababu huku nje wananchi ambacho walikuwa wanakiona au kujadili kwa yale ambayo yalikuwa yakitokea dhidi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), walikuwa wanaona kama ni kuonewa kwa chama hicho, walikuwa hawakipimi kama ni chama ambacho kimekosea na kinastahili adhabu hiyo. Na kutokana na suala kama hilo, maana yake mvuto na ushawishi wake kwa Watanzania kwa kiasi kikubwa umeongezeka zaidi kuliko kabla ya kuzuiwa kufanya mikutano hiyo,” ameeleza Mudimi.

Wakati Lyenda akiweka msimamo wa kutoitukuza Mahakama ya Rufaa kwa maamuzi iliyoyafanya, lakini Mudimi bado anautafsiri uamuzi huo kama ishara ya uwepo wa mfumo wa haki unaofanya kazi, “Uamuzi huo wa Mahakama ni ushindi kwa demokrasia, kama kunakuwa na mazuio ambayo yanawekwa kwa vyama pinzani, hasa kwa chama kikuu cha upinzaji cha CHADEMA, na kina uwezo wa kwenda Mahakamani na kikapata haki yake, maana yake huo ni ushindi kwa demokrasia, lakini pia inaonesha uwepo Mahakama.”

Ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kurejea huku kunachukuliwa kama mwanzo wa harakati mpya, “Wanachama nchi nzima, bendera zipande kwenye vijiwe na ofisi za chama. Shughuli zote za siasa ziendelee kama kawaida. Chama kinaanza upya, na kanda zote lazima ziwe katika utendaji wa hali ya juu kuanzia sasa,” alisema John Heche, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, John Heche akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya Mahakama ya Rufaa Dodoma kuondoa zuio la kufanya siasa kwa chama hicho. Picha: CHADEMA

Kwa vijana wa chama hicho wanaona kuwa hii ni nafasi ya kurudi kwa nguvu katika ukumbi wa siasa nchini Tanzania, Katibu wa Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA), mkoa wa kichama wa Temeke, Blessing Barabara, ana matumaini na mwelekeo wa chama.

“Matarajio makubwa nilionayo kwenye Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ni kwamba chama kitarejea kwenye operesheni za kupigania haki za wananchi, kama unavyokumbuka tulikuwa na operesheni mbalimbali za mikutano ya hadhara, makongamano na shughuli nyingine mbalimbali za kisiasa ambazo zilikuwa zinajikita katika kupigania na kuzungumzia kero na changamoto za wananchi,” amezungumza Barabara.

Matarajio hayo yanaungwa mkono na viongozi wengine, akiwemo Raphael Magowe, Katibu wa Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA), Kanda ya Pwani, ambaye anaamini kurejea kwa chama kutafungua mawasiliano mapya na wananchi, “Kama chama sasa tunatarajia kwamba tunaenda kuanza operesheni zetu za chama, tunaenda kufanya kazi kwa nguvu zote…tunaenda kuwaambia wananchi mwelekeo wetu wa mbele…tunatarajia kwamba wananchi wetu watatupokea vizuri.”

Pamoja na matumaini hayo, uhalisia wa kisiasa unabaki kuwa mgumu, ikizingatiwa kuwa CHADEMA inarejea bila uwakilishi Bungeni kufuatia kutoshiriki uchaguzi mkuu wa 2025, jambo ambalo lina athari za moja kwa moja kwa chama hicho.

“Tunakumbuka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hakikushiriki uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba mwaka jana, kwa hiyo miongoni mwa changamoto walizonazo, kwanza, wanakosa uwakilishi Bungeni, lakini pia hata ruzuku ile ya serikali, tunasema itakuwa ni changamoto ya kiuchumi…na wenyewe wanakuwa wanakosa, kwa hiyo wanaweza wakati fulani wakapitia mkwamo wa kifedha,” maoni ya Juma Mudimi, Mchambuzi wa masuala ya siasa.

Vilevile kutokuwepo kwa wawakilishi Bungeni pia kunamaanisha ukosefu wa sauti rasmi ya kuwasilisha ajenda za chama hicho, “Lakini kukosekana kwa wawakilishi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kiasi fulani kunaweza kuwasababishia baadhi ya changamoto ambazo ni pamoja na kushindwa kupata watu ambao watabeba ajenda za CHADEMA kuziwasilisha Bungeni,” ameongeza Mudimi.

Hata hivyo, CHADEMA ina nafasi ya kuweka mikakati na kutumia hali hiyo kama fursa, Mudimi anaona kuwa chama hicho kina “karata ya turufu” ya kujieleza kwa wananchi, “Tupo katika kipindi ambacho imani ya Watanzania kwa vyama vya siasa imeshuka kwa asilimia kubwa, lakini bahati ambayo wameipata Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ni kutokushiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, pia wana uwezo na nafasi ya kujitetea kwamba sisi hatukushiriki kwa sababu tulikuwa tumezuiwa kufanya shughuli za kisiasa. Kutokana na hivyo, bado CHADEMA wana karata ya turufu ya kwenda kujieleza kwa wananchi juu ya kile ambacho kimetokea, kuonesha namna gani walikuwa upande wa wananchi kuelekea uchaguzi mkuu mwaka jana.”

Kuhusu namna chama kilivyojipanga kisiasa mara baada ya kuondolewa kwa zuio hilo, John Pambalu anaonesha msimamo wa kujiamini huku akisisitiza kuwa chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM) sio tishio kwao katika ushindani wa kisiasa, akieleza kwamba wamejipanga kuimarisha chama kwa malengo ya muda mrefu ya kisiasa.

“Chama tawala hakiwezi kuwa mshindani wa CHADEMA, chama tawala kimeshapoteza sifa ya kuwa chama cha siasa…katika uwanja wa kisiasa kwamba CHADEMA wafanye siasa, CCM wafanye siasa, CCM hawana uwezo wa kushindana na CHADEMA. Kwa hiyo tutakachokifanya sisi ni kuendelea kukiimarisha chama, kwa ajili ya mapambano ya kupigania katiba mpya, tume huru ya uchaguzi na chaguzi zilizo mbele yetu, kwa sababu shabaha ya chama chochote cha siasa ni kushika dola,” amesema Pambalu.

Wakati maamuzi makubwa yakisubiriwa kupitia vikao vya juu vya chama hicho, viongozi wanaelekeza macho yao kwenye Kamati Kuu kama chombo kitakachobeba mwelekeo katika kipindi hiki kipya,“Kamati Kuu itaketi hivi karibuni, wiki ijayo, itaketi, itatoka sasa na mwelekeo kama chama tunakwenda kufanya nini, na mipango gani iliyopo mikononi mwetu,” amezungumza Mkuu wa Idara Habari na Uenezi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Gervas Lyenda.

“Bila kuingilia au kutangulia maamuzi yatakayofanywa na Kamati Kuu, lakini kuna ajenda tunazo tayari ambazo hazijafa, bado zipo hai na ni vilio vya Watanzania…Ajenda ya kwanza tunaiona ya ni Lissu aachiliwe, hiyo itakuwepo…Ajenda ya pili ambayo naona bado ni takwa la nchi ni ‘No reforms, No Election’, wote tunafahamu uchaguzi jinsi ulivyofanyika,” ameongeza Lyenda.

Hivi karibuni, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, John Heche alibainisha azma ya kuanzisha kampeni ndani na nje ya Tanzania kwa ajili ya kushinikiza kuachiliwa kwa Mwenyekiti wao, Tundu Lissu ambaye anakabiliwa na kesi ya uchochezi pamoja na uhaini. Kwa upande wake Mchambuzi wa masuala ya siasa, Juma Mudimi anaona kuwa kuondolewa kwa zuio hilo ni fursa kwa chama hicho kusukuma ajenda hiyo.

“CHADEMA kuruhusiwa kurejea kufanya siasa maana yake wamepata fursa ya kurejea katika ulimwengu wa kisiasa, na wana uwezo wa kuyazungumza yale yanayotakiwa kufanywa na chama, na kuweza kuyasimamia na kuyashinikiza, ili kuona ni namna gani CHADEMA inarejea vizuri katika ulimwengu wa siasa, lakini wanawezaje kushawishi jamii ili iweze kuwasaidia kushinikiza Mwenyekiti wao kuweza kuachiwa,” amezungumza Mudimi.

Kurejea kwa CHADEMA kwenye ulimwengu wa siasa hakumaanishi mwisho wa changamoto zake, ni mwanzo wa awamu nyingine ya kisiasa ambayo itapimwa kwa vitendo, uwezo wa chama kujijenga upya, kuunganisha wanachama wake na kurejesha imani ya wananchi.

Ujumbe kwa wanachama na wafuasi umewekwa wazi, ukisisitiza uvumilivu na mshikamano katika kipindi hiki kipya. John Pambalu anaonesha msimamo huo kwa kuwakumbusha kuwa mapambano ya kisiasa yanahitaji subira.

“Safari ya ukombozi haijawahi kuwa rahisi hata kidogo, Israel walitumia karibia siku 40 kutoka Israel kwenda Misri, lakini kutoka Misri kurudi katika nchi yao ya Israel iliwachukua miaka 400, hawakukata tamaa. Tusikate tamaa, tupo karibu sana na mafanikio ya kuikomboa nchi yetu. Watanzania wengi wapo nyuma yetu, wapo karibu na sisi kwa hiyo tusikate tamaa, tuungane, tushirikiane,” amesisitiza Pambalu.

“Tuendelee kushikamana, tuendelee kupigania maslahi ya taifa letu, tuendelee kupigania maslahi ya wananchi wetu…Wanachadema waendelee kubakia na Taasisi yao,” amesisitiza Gervas Lyenda juu ya mshikamano kama msingi muhimu katika kipindi hiki.

Mwandishi: Dominic Allen

Mhariri: Yohani Gwangway

Hot this week

Mnyonge, mnyongeni ila haki yake mpeni

By Dorlingson Edward Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), leo...

CHADEMA kutoa msimamo wake kuhusu maridhiano

By Veronica Mlyatu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa...

Popular Articles

Safari ya Mashimba katika kutetea jamii ya Wahadzabe

Nchini Tanzania  kuna jumla ya makabila zaidi ya 120...

Polisi waendelea kuwashikilia viongozi wa CHADEMA

Ni siku ya kwanza tangu kukamatwa kwa viongozi wa...

Siku ya Vijana Duniani.

Kwa sasa ni kijana wa miaka 25 ambaye amejiajiri...

BWAWA LA ARBA’AT  LASABABISHA MAAFA NCHINI SUDAN

Watu 30 mashariki mwa Sudan na na wengine 60...

Sand Mining in Tanzania: Trails of Destruction in Lake Victoria and its Environs

By Dominic Allen On November 14th, 2021 in the Geita...

 Utekaji: Fumbo linalotushinda?

Na Yohani Gwangway Taifa la Tanzania kwa miaka mingi limekuwa...

Abduction: Is it a riddle we can’t solve?

By Yohani Gwangway For many years Tanzania has been an...

Mustakabali wa Hewa Safi kwa kila kiumbe

Na Dominic Allen Msingi wa maisha ya viumbe hai yaani...
LAND DWELLERS FACT CHECK HUB VERIFY FACTS STOP MISINFORMATION Trusted Fact-Checking in Tanzania Beyond What You Know VERIFY NOW

Related Articles

Popular Categories

DWELLERS CHECK-HUB Verify Facts. Stop Misinformation Trusted Fact-Checking in Tanzania • Beyond What You Know VERIFY NOW