Miundombinu duni: Kikwazo cha elimu kwa watoto wenye ulemavu mkoani Mwanza

Na Dominic Allen

“Changamoto ya ngazi na vyoo, halafu kuna mawe, kwa hiyo ukienda vibaya unaweza kujikwaa…mtu asipofikisha wastani wa 64, viboko, wakati huku mwanzo hajapata matirio ya kutosha.”

Kauli ya Joasen Julius, mwenye ulemavu wa miguu na kuzungumza, ikiweka wazi uhalisia mchungu unaowakabili wanafunzi wenye ulemavu katika taasisi za elimu mkoani Mwanza. Badala ya kuwa na mazingira rafiki yanayowezesha kupata haki ya elimu, watoto wenye ulemavu hukumbana na changamoto ya miundombinu hatarishi na mfumo unaopuuza mahitaji yao ya msingi. Ngazi zisizopitika, vyoo visivyofikika pamoja na uduni wa vifaa maalum vya kujifunzia kwa wanafunzi wenye ulemavu hugeuka kuwa vikwazo vinavyohatarisha sio tu usalama bali pia kuathiri ufaulu wao kitaaluma.

Makala hii inaangazia changamoto ya miundombinu kwa wanafunzi wenye ulemavu katika shule za msingi na sekondari mkoani Mwanza, na namna ambavyo ukosefu wa usawa katika mazingira ya shule unavyonyima haki yao kupata ya elimu bora.

Miundombinu isiyo rafiki kwa watoto wenye ulemavu imekuwa tatizo sugu katika baadhi ya shule za msingi na sekondari mkoani Mwanza, hali inayowalazimu wanafunzi hawa kutumia nguvu zaidi ili kupata kile ambacho wenzao wanapata kwa urahisi. Kitendo cha miundombinu kujengwa bila kuzingatia viwango vya ufikivu, ni jambo linalogeuza elimu kutoka kuwa haki ya wote na kuwa mapambano ya kila siku kwa wachache.

Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, toleo la mwaka 2023, katika sehemu ya 3.2.1 imeweka hakikisho juu ya upatikanaji wa fursa mbalimbali za elimu na mafunzo, ikiwemo kwa watoto wenye ulemavu.

“Kila Mtanzania ana haki ya kupata fursa za elimu na mafunzo bila ubaguzi wa jinsi, rangi, kabila, dini, ulemavu na hali ya kijamii au kipato,” imebainisha Sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014, toleo la mwaka 2023.

Hata hivyo, licha ya sera kuweka matumaini katika mioyo ya watoto wenye ulemavu, hali halisi katika baadhi ya shule za msingi na sekondari katika wilaya ya Nyamagana, Ilemela na Misungwi, inakinzana na ahadi hizo.

Vifungu vya 27 na 28 vya Sheria ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2010 vinalinda haki yao ya kupata elimu bila ubaguzi, ikisisitiza kuwa wanapaswa kufurahia fursa sawa za kielimu kama raia wengine wote. Kwa mujibu wa sheria, watu wenye ulemavu wa rika na jinsia zote wana haki ya kupata elimu na mafunzo katika mazingira jumuishi pamoja na kunufaika na matokeo ya tafiti za kielimu.

“Watu wenye ulemavu wa rika zote na jinsia zote wanapaswa kuwa na haki sawa ya kupata elimu, mafunzo katika mazingira jumuishi, pamoja na kunufaika na matokeo ya tafiti kama raia wengine.”

Aidha, sheria hiyo imeweka bayana kuwa watoto wenye ulemavu hawapaswi kunyimwa nafasi ya kujiunga na shule, iwe ya umma au binafsi, kwa misingi ya ulemavu wao. “Kila mtoto mwenye ulemavu anapaswa kuwa na haki sawa kuhusiana na udahili katika shule za umma au binafsi.”

Sheria hiyo imeelekeza wajibu moja kwa moja kwa taasisi za elimu nchini kuhakikisha usawa huo. Shule na vyuo vinatakiwa kisheria kuhakikisha hakuna aina yoyote ya ubaguzi dhidi ya watu wenye ulemavu katika mifumo yao ya elimu. “Kila taasisi ya elimu inapaswa kuwa na wajibu wa jumla wa kutowabagua watu wenye ulemavu.”

Sheria hii imeweka msisitizo kuwa elimu jumuishi si suala la hiari, bali ni wajibu wa kisheria unaopaswa kuzingatiwa na taasisi zote za elimu ili kuhakikisha haki na usawa vinazingatiwa kwa kila mwanafunzi.

Katika mkoa wa Mwanza, takwimu zilizotolewa mwezi Januari, 2025 na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, idadi ya watu wenye ulemavu kwa mkoani hapa ni 10,896 ambapo kati ya hao wenye ulemavu wa viungo ni 5,362 wenye ulemavu wa macho 1,416 viziwi ni 1,862 huku wenye matatizo ya afya ya akili ni 2,004 na mwenye ualibino ni 609.

Kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), mkoa wa Mwanza una idadi ya shule za msingi 1,038, huku shule za sekondari zikiwa ni 330. Licha ya uwepo wa shule hizi, changamoto za kukosekana kwa miundombinu isiyo rafiki kwa wanafunzi wenye ulemavu zinatajwa kuwa jinamizi linalozikumba.

Mwalimu mmoja wa Shule ya Msingi Nyamagana (Jina limehifadhiwa) amesema kuwa katika mkoa wa Mwanza hali ya miundombinu rafiki kwa watoto wenye ulemavu bado iko chini, huku akibainisha kuwa vifaa na mazingira ya kujifunzia hayaridhishi.

“Unakuta vile vifaa na mazingira ya kujifunzia ni mabovu, hata aina ya walimu ambao wanatakiwa wawepo,” amesema mwalimu huyo.

Wakati kifungu cha 35 (4) kikianisha wajibu wa taasisi na mamlaka zinazotoa huduma kwa umma, ikiwemo shule za msingi na sekondari kuhakikisha kuwa majengo yanakidhi haja za watu wenye ulemavu bila vikwazo, mwalimu huyo anasema baadhi ya shule hazina madarasa maalum kwa ajili ya watoto wenye ulemavu.

“Kwanza madarasa yenyewe hayapo, yaani madarasa ya watu maalum…kwa sababu unapomchukua mtoto mwenye ulemavu ukasema kwamba umchanganye na wanafunzi wengine, hawezi kupata kusimamiwa vizuri…lazima liwepo darasa la maalum kwa ajili ya watoto ambao hawajiwezi ili hata huduma wazipate kiurahisi,” ameeleza.

Joasen Julius ambaye ni kijana mwenye ulemavu wa miguu na kuzungumza, mkazi wa Bulale, kata ya Buhongwa jijini Mwanza amesema baadhi ya wanafunzi walemavu wana changamoto ya uelewa kulinganisha na wanafunzi wengine, hivyo hujikuta wakiachwa nyuma darasani.

“Watu wenye ulemavu wanapata changamoto ya uelewa, kwa sababu mwalimu akija ubaoni atafundisha, yaani atajumulisha, hakuna cha sijui huyu ni mlemavu hajaelewa, huyu anataka kufafanuliwa, hata kuandika unakuta mwingine anaandika polepole,” amesema Julius.

Julius pia amezungumzia suala ya adhabu dhidi ya wanafunzi wenye ulemavu kutokana na kushindwa kwenda sambamba na kasi ya wanafunzi wasio na ulemavu, akisema vitendo hivyo dhidi ya wenye ulemavu sio haki.

“Kuna ulemavu wa mikono…sasa mlemavu wa mikono anaweza akawa ana akili ila akashindwa jinsi ya kusoma kwa bidii kutokana nae unakuta hajamaliza (kuandika), unafika unampiga, wakati mikono yake ni midhaifu kuandika,” masikitiko ya Julius kuhusu adhabu dhidi ya wanafunzi wenye ulemavu.

Katika Shule ya msingi Bulale iliyopo kata ya Buhongwa jijini Mwanza, baadhi ya miundombinu kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu, kama vile ngazi za kuingia kwenye vyumba vya madarasa, zimemomonyoka kwa chini, hali hiyo inaonesha kuwa endapo wanafunzi wenye ulemavu, hususan wanaotumia viti mwendo au baiskeli maalum watasajiliwa shuleni hapo, wanaweza kukumbana na changamoto ya kupandisha na kushuka katika maeneo hayo. Changamoto hiyo ya kumomonyoka kwa ngazi za kupandia walemavu zimeshuhudiwa pia katika Shule ya msingi na awali ya Amina Makilagi, ambayo nayo ipo Buhongwa.

Moja ya ngazi za kupandia wanafunzi wenye ulemavu katika Shule ya msingi Bulale zikiwa zimeanza kumomonyoka, hali inayohatarisha usalama wao. Picha: Dominic Allen.

Mbali ya kumomonyoka kwa ngazi za kupandia wanafunzi wenye ulemavu, katika shule hizi mbili hakuna miundombinu rafiki kwa ajili ya michezo kama vile viwanja maalum vya michezo kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu, licha ya Sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014, toleo la mwaka 2023 kuweka msisitizo juu ya elimu jumuishi, lakini wanafunzi wenye ulemavu hujikuta wakiwa kutokana na kukosekana kwa miundombinu itakayowawezesha kupata haki ya elimu sawa na wanafunzi wengine.


Ngazi za kupandia kwa wanafunzi wenye ulemavu katika Shule ya msingi Amina Makilagi, iliyopo jijini Mwanza, zikiwa zimemomonyoka na kuharibika kwa chini, hali inayowaweka kwenye hatari wanafunzi wenye ulemavu wanaozitegemea kuingilia darasani. Picha: Dominic Allen.

Ripoti ya Tathmini ya hali kuhusu haki za watu wenye ulemavu – Tanzania (2021/2022) imeeleza kuwa kwa mujibu wa takwimu za “Mapitio ya takwimu za watu wenye ulemavu” iliyotolewa na Leonard Cheshire (2018), nchini Tanzania, kiwango cha watoto wenye ulemavu wanaokamilisha elimu ya msingi ni asilimia 49 ikilinganishwa na asilimia 83 ya watoto wasio na ulemavu.

Ripoti imesema shule na madarasa mengi hayafikiki kwa wanafunzi wenye ulemavu kutokana na umbali na usafiri usio rafiki, miundombinu ya shule ikiwemo vyoo, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), mbinu mbadala za mawasiliano, pamoja na ufadhili mdogo au kipaumbele kidogo cha kugawa fedha kwa ajili ya kuboresha upatikanaji wa miundombinu shuleni.

Pia, ripoti ya “Ujumuishwaji wa watoto wenye ulemavu sio anasa ni haki” ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) ya mwaka 2021 imebainisha kuwa kote duniani, mtoto mmoja kati ya 10 ana ulemavu. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watoto wenye ulemavu wanakosa fursa ikilinganishwa na watoto wasio na ulemavu katika hatua nyingi za ustawi wa wao, ambapo wanakosa mahitaji ya msingi ikiwemo afya, elimu na ulinzi.

Makumba Mwemezi, ambaye ni Mkuu wa idara ya utafiti, ubunifu na uchambuzi wa sera kutoka shirika la HakiElimu, amesema shule zote zinatakiwa kuwa na miundombinu ambayo inaweza kuwapokea watoto wote kulingana na uwezo wao.

“Shule zote zinapaswa kuwapokea kulingana na uwezo wao. Uwezo wao kwa maana ya maumbo, uwezo wa kufika au kutofika, na mambo mengine,” amefafanua Mwemezi.

Mwemezi ameeleza kuwa suala la changamoto za miundombinu kwa upande wa wanafunzi wenye ulemavu ndiyo kubwa zaidi, kwani shule nyingi hujengwa bila kuwepo na mazingira wezeshi ya kuwafanya wanafunzi hao kupata haki ya elimu jumishi na bora.

“Miundombinu mingi ya shule inayoandaliwa, inaandaliwa bila kuweka viambata ambavyo vinawasaidia watoto wenye ulemavu kukaa…shule nyingi hazina miundombinu ya vyoo mahususi kwa ajili ya watoto wenye ulemavu, miundombinu mingine kama mabweni na kadhalika,” ameeleza Mwemezi.

Katibu wa Idara ya Haki za Binadamu na Vyombo vya Uwakilishi wa Wananchi, ACT Wazalendo Taifa, Mbarala Maharagande, anaona suala la bajeti kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu bado halijapewa kipaumbele ipasavyo.

“Bajeti ya nchi haijatoa kipaumbele katika eneo hilo. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya 2024/25 ameonesha kwamba kuna matumizi yasiokuwa ya lazima shilingi za Kitanzania bilioni 347. Kwa hiyo, bado changamoto iliyopo vilevile ni serikali kutotoa kipaumbele kinachostahiki na kutofanya matumizi mazuri ya rasilimali zetu,” amezungumza Maharagande.

Abdulrahman Lugone, Mweka Hazina mstaafu wa Shirikisho la Vyama vya Walemavu Tanzania (SHIVYAWATA), amesema baadhi ya watoto wenye ulemavu wamejikuta wakiathirika kiafya kutokana na kutojengewa vyoo maalum kwa ajili yao, hali inayowalazimu kuchangia vyoo na wanafunzi wasio na ulemavu.

“Wanaathirika kiafya, kwa sababu kuna maradhi kama vile UTI, wanaambukizwa kwa njia hiyo, na maradhi yote ambukizi ambayo yanatokana na mazingira machafu ambayo mtoto mwenye ulemavu anayetambaa yanaweza kumuathiri,” amezungumza Lugone.

Mtaalam wa masuala ya afya, Joyce Lukumay, ameeleza kuwa ni kweli watoto wenye ulemavu wapo katika hatari kubwa ya kupata magonjwa ya mlipuko na maambukizi kutokana na kukosekana kwa vyoo maalum kwa ajili yao.

“Ni lazima wapate madhara, wanapata maambukizi, magonjwa ya kuambukiza ya mlipuko, kuna kipindupindu, homa za matumbo,” ameeleza Lukumay.

Kwa upande wake Julius, ameizungumzia changamoto ambayo yeye binafsi wakati anasoma ilikuwa ikimkumba, ambayo ni umbali wa ilipokuwa shule anayosoma na kufikika kwa madarasa kwa wanafunzi wenye ulemavu, akieleza kuwa imekuwa kikwazo kikubwa kwa wanafunzi wenye ulemavu kupata haki ya elimu.

“Unaweza kukuta muda mwingine barabara inajaa maji, ukiteleza, madaftari yanaanguka, yakishaanguka kwenye maji yanaloana, kwa hiyo ni changamoto,” amezungumza Julius.

Hata hivyo sio shule zote zimekosa miundombinu kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu, katika Shule ya sekondari ya Mwasonge, iliyopo wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, ikiwa bado ni shule changa, kwa kiasi chake ina miundombinu iliyo rafiki kwa wanafunzi hao, ikiwemo ngazi za kupandia kwenye majengo ya shule pamoja na vyoo maalum kwa ajili yao.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mwasonge A, Robert Kahema, ameelezea ni kwa namna gani miundombinu katika shule hiyo, ikiwemo njia za kupita pamoja na vyoo, inavyowezesha upatikanaji wa elimu jumuishi.

“Ukifika pale, unakuta hata ile milango yake inaelekeza kwamba hata kama ingekuwa mtoto (mlemavu) anatumia baiskeli, anaingia tu vizuri,” amezungumza Kahema.

Hata hivyo, sintofahamu bado ipo katika Shule ya msingi St. Benjamin iliyopo katika kijiji hicho cha Mwasonge, kwani ina majengo chakavu, huku kukiwa na miundombinu duni ya kuwawezesha watoto wenye ulemavu kupata elimu bora. Mwenyekiti Kahema ameeleza kuwa hata kwa watoto wasio na ulemavu bado wanataabika na uchache wa madawati, jambo linaloathiri maendeleo yao shuleni.

“Kimsingi haipo vizuri sana hasa upande wa madawati, kumekuwa na madawati machache mno kiasi kwamba kuna baadhi ya wanafunzi wanakaa chini kwenye sakafu,” ameeleza Kahema.

“Miundombinu hii kimsingi haipo,” akieleza Kahema juu ya changamoto ya kukosekana kwa miundombinu kwa ajili ya watoto wenye ulemavu katika Shule ya msingi St. Benjamin.

Moja ya majengo ya madarasa katika Shule yasingi St. Benjamin, iliyopo Mwasonge, likiwa halina ngazi au njia maalum ya kupandia kwa wanafunzi wenye ulemavu, hali inayowakosesha urahisi na usalama wa kufika darasani. Picha: Dominic Allen.

Katika wilaya ya Ilemela, kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, wilaya hii ina jumla ya shule za msingi 130, kati ya hizo 76 ni za serikali na 54 ni za binafsi, huku shule za sekondari zikiwa ni 54, kati ya hizo shule 32 ni za serikali na shule 22 ni za binafsi.

Abdulrahman Kange, Diwani wa kata ya Nyamanoro kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), amesema kuwa miundombinu katika shule za msingi katika kata hiyo sio rafiki sana, kulingana na mahitaji maalum kwa wanafunzi wenye ulemavu ili kupata elimu bora, sawa na wanafunzi wengine.

“Ni rafiki (miundombinu), lakini si rafiki sana, kwa sababu kutokana na mazingira ya mahitaji ya vifaa vyao katika shule zetu,” ameeleza Diwani Kange, huku akizitaja shule ya Mwenge na Karume kuwa na mazingira rafiki kwa wanafunzi wenye ulemavu, ikiwemo vifaa vya kujifunzia pamoja na walimu maalum kwa ajili yao.

“Kwa shule zetu za Mwenge na Karume hali yao ni zuri, kwa sababu walimu hao wapo na wanafunzi hao wapo, na wanaendelea kupata taaluma kupitia walimu wetu. Kwa hiyo, kimsingi hapo ni sehemu ambayo ni rafiki kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum,” amezungumza Diwani Kange.

Magege Hailala Magege, mkazi wa kata ya Nyamanoro, ambaye pia ni Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilayani Ilemela, amesema baadhi ya shule katika wilaya hiyo ziko katika maeneo ya milimani, hivyo ni ngumu kufikika kwa urahisi kwa wanafunzi wenye ulemavu, hivyo kuwanyima fursa ya elimu wanafunzi hao.

“Miundombinu sio rafiki kwa watoto wenye ulemavu, kwa kuwa baadhi ya shule zipo milimani, kwenye miinuko ya milima, hapajatengenezewa miundombinu ya kufika shuleni. Shule ya sekondari ya Nyamanoro ipo juu ya mlima, shule ya msingi ya Ibungilo ipo juu ya mlima…na sehemu hizo hakuna usafiri wa moja kwa moja,” ameeleza Magege.

Magege akiwa ni mkazi wa Ilemela kwa takriban miaka 40, amesema kutokana na idadi chache ya wanafunzi wenye ulemavu katika baadhi ya shule wilayani hapo, kwa muda mwingi vyoo vyao huwa vimefungwa ili kuepuka kuchafuka na kuharibika, jambo ambalo linapelekea wanafunzi hawa kutumia vyoo vya jumuiya.

“Baadhi ya vyoo vipo vya watoto wenye ulemavu, lakini kwa muda mwingi vinakuwa vimefungwa…mara nyingi ili kukiepusha visiharibike au visichafuke, wanavifunga,” amezungumza Magege.

Kwa mtazamo wake Magege, kutokuwepo kwa mazingira rafiki katika shule za msingi za msingi na sekondari kumekuwa na chanzo wanafunzi hawa kushindwa kufanya vizuri kwenye masomo yao.

“Athari ni kubwa, kwa sababu maendeleo ya shule (wanafunzi wenye ulemavu) yanategemeana na mazingira, sasa wanapokutana na sehemu ambayo haina mazingira rafiki, uwezo wa kukaa na kushika yale wanayofundishwa unakuwa ni mdogo,” maoni ya Magege.

Hoja ya Magege haijaenda mbali sana na Mwemezi, ambaye amesema kuwa mazingira yana mchango mkubwa wa mtoto kuweza kujifunza, hivyo kukosekana kwa mazingira rafiki kwa watoto wenye ulemavu shuleni kuna madhara makubwa katika safari yao ya elimu.

“Mazingira yana mchango mkubwa sana wa mtoto kuweza kujifunza, kama mtoto hawezi kujifunza inachangia mambo matatu; moja, utoro wa watoto hawa…la pili wapo watoto wanaacha kabisa shule, inasababisha athari kwao kwa maana kuwa na watoto walemavu ambao hawana elimu…nyingine, mazingira haya yanawafanya wajisikie kutengwa na kushindwa kusoma vizuri kwa sababu wanakosa usaidizi,” amesema Mwemezi.

Licha ya kuibuka kwa maswali kadhaa yaliyohitaji ufafanuzi kutoka kwa uongozi wa shule pamoja na maafisa elimu, baadhi ya shule hizo zilisema haziwezi kutoa maelezo yoyote bila kibali cha Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza. Hata hivyo, hadi makala hii inachapishwa, Land Dwellers ilikuwa imefanya jitihada za kuwasiliana na ofisi ya Mkurugenzi kwa ajili ya kupata kibali hicho, lakini hakukuwa na mafanikio.

Changamoto ya miundombinu katika shule za msingi na sekondari kwa watoto wenye ulemavu sio la Mwanza pekee, bali ni tatizo pana lililopo katika maeneo mengi nchini Tanzania. Kukosekana kwa njia maalum kwa ajili yao, vyoo rafiki, madarasa yanayofikika pamoja na mazingira salama, kunawafanya watoto wengi wenye ulemavu kushindwa kuhudhuria masomo au kuacha shule kabisa. Hali hii inaendeleza mzunguko wa kutengwa na kukiuka haki ya msingi ya elimu kwa kundi hili ambalo tayari linakabiliwa na vikwazo vingi vya kijamii na kiuchumi.

Wakati sheria na sera zikisisitiza haki ya elimu jumuishi, utekelezaji wake bado unaacha maswali mengi. Baada ya kuangalia ukubwa na athari za changamoto za miundombinu kwenye shule za msingi na sekondari katika mkoa wa Mwanza kwa watoto wenye ulemavu, sehemu inayofuata ya makala hii itaangazia suala la uwajibikaji, ikichunguza ni nani hasa anapaswa kubeba dhamana ya kuhakikisha shule zinakuwa na miundombinu rafiki, na kwa nini wajibu huo umeendelea kuwa hafifu licha ya uwepo wa mifumo ya kisheria.

Mwandishi: Dominic Allen

Mhariri: Yohani Gwangway

Hot this week

Mnyonge, mnyongeni ila haki yake mpeni

By Dorlingson Edward Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), leo...

CHADEMA kutoa msimamo wake kuhusu maridhiano

By Veronica Mlyatu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa...

Popular Articles

Safari ya Mashimba katika kutetea jamii ya Wahadzabe

Nchini Tanzania  kuna jumla ya makabila zaidi ya 120...

Polisi waendelea kuwashikilia viongozi wa CHADEMA

Ni siku ya kwanza tangu kukamatwa kwa viongozi wa...

Siku ya Vijana Duniani.

Kwa sasa ni kijana wa miaka 25 ambaye amejiajiri...

BWAWA LA ARBA’AT  LASABABISHA MAAFA NCHINI SUDAN

Watu 30 mashariki mwa Sudan na na wengine 60...

Sand Mining in Tanzania: Trails of Destruction in Lake Victoria and its Environs

By Dominic Allen On November 14th, 2021 in the Geita...

 Utekaji: Fumbo linalotushinda?

Na Yohani Gwangway Taifa la Tanzania kwa miaka mingi limekuwa...

Abduction: Is it a riddle we can’t solve?

By Yohani Gwangway For many years Tanzania has been an...

Mustakabali wa Hewa Safi kwa kila kiumbe

Na Dominic Allen Msingi wa maisha ya viumbe hai yaani...
LAND DWELLERS FACT CHECK HUB VERIFY FACTS STOP MISINFORMATION Trusted Fact-Checking in Tanzania Beyond What You Know VERIFY NOW

Related Articles

Popular Categories

DWELLERS CHECK-HUB Verify Facts. Stop Misinformation Trusted Fact-Checking in Tanzania • Beyond What You Know VERIFY NOW