Na Dr. Bravious Kahyoza
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuweka mikakati mbalimbali ili kuondokana na tatizo la ukosefu wa ajira hasa kwa kundi la vijana, ambalo ni asilimia 34.5 ya idadi ya Watanzania wote ambao ni milioni 61, hii ni kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.
Januari 07, 2022 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa Wilaya ya Mkoani, Kusini Pemba alikiri uwepo wa tatizo la ajira nchini na kuahidi kulishughulikia.
“Serikali yenu tunajua tatizo la ajira na tunajitahidi kutengeza fursa mbalimbali ili vijana wapate ajira”
Katika kutatua tatizo la ukosefu wa ajira, Serikali imefanikisha kuzalisha ajira zaidi ya milioni 8.08 katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2020 hadi mwaka 2025, jambo ambalo ni moja ya mafanikio makubwa ya kiuchumi hapa nchini.
Mafanikio haya ni matokeo ya ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na sekta binafsi, pamoja na utekelezaji wa mkakati wa makini wa kuboresha mazingira ya uwekezaji na kukuza fursa za ajira. Lengo hili lilikuwa moja wa ahadi kuu za Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya 2020–2025, ambayo ililenga kuzalisha ajira milioni 8 ifikapo 2025.

Mafanikio haya yanatokana na sera za kiuchumi zinazolenga kuimarisha uwekezaji katika sekta za kilimo, viwanda, uvuvi, utalii na teknolojia, ambazo zimechochea ukuaji wa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.
Kufikia lengo hili kunaonyesha uwezo wa Serikali ya Tanzania kutimiza ahadi zake kwa wananchi na kujenga uchumi wenye nguvu na endelevu. Hii ni ishara ya maendeleo ya kweli ya kiuchumi ambayo inagusa moja kwa moja maisha ya wananchi wa kawaida.
Mkakati wa Serikali katika kuzalisha ajira
Chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali imechukua hatua za makusudi za kuboresha mazingira ya uwekezaji na kukuza fursa za ajira kwa njia za kisasa na za kimkakati. Juhudi hizi zimejumuisha uwekezaji mkubwa katika miundombinu, kuboresha sera za kodi na kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi.
Serikali imefanikisha ujenzi wa viwanda vipya vya kisasa, hasa kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania, ambapo inatarajiwa viwanda vikubwa 500 vitajengwa kufikia 2025.
Miradi mikubwa kama ya Reli ya Kisasa (SGR) na bandari za Tanga na Dar es Salaam imechangia fursa nyingi za ajira, ikiwemo ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja. Kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi ya Huduma za Ajira Tanzania, Serikali imetangaza nafasi za kazi za umma, ikiwa ni pamoja na ajira 3,633 za walimu mwaka 2024. Serikali pia imefanikisha usajili wa ajira mtandaoni ili kuwafikia vijana wengi zaidi na kurahisisha mchakato wa kutafuta kazi.
Mchango wa Sekta Binafsi katika ajira
Sekta binafsi imeendelea kuchangia pakubwa katika ukuaji wa ajira nchini Tanzania, ikichangia asilimia kubwa ya ajira mpya zilizozalishwa. Serikali imeshirikiana na wadau wa sekta binafsi, ikiwa ni pamoja na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), kuboresha mazingira ya kazi na kima cha chini cha mshahara, ambacho kimepangwa kwa ushirikiano na wadau wa utatu yaani Serikali, Waajiri, na Wafanyakazi. Ushirikiano huu umesaidia kujenga mazingira ya kazi yanayostahimili na ya haki.
Mifano ya sekta binafsi inayochangia ajira ni pamoja na makampuni ya kimataifa kama Vodacom, AB InBev, na One Acre Fund, ambayo yametangaza nafasi za kazi za fani mbalimbali mwaka 2024 na 2025.
Sekta ya uvuvi imezalisha zaidi ya ajira milioni 4.5, ikiwa ni pamoja na wavuvi wa asili, wakulima wa mwani, na wafanyakazi wa ufugaji wa samaki. Uwekezaji wa viwanda vya kwala umelenga kuongeza ajira 400,000 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kupitia uwekezaji wa Dola za Marekani bilioni 3.

Mwenendo ongezeko la ajira nchini Tanzania
Mwenendo wa ajira zilizozalishwa unaonyesha ongezeko la hatua kwa hatua kuanzia mwaka 2020 hadi 2025. Mwaka wa kwanza wa kipindi hiki, yaani 2020/2021, ajira 482,601 zilizalishwa, na mwaka uliofuata 2021/2022, idadi iliongezeka hadi 584,333. Mwaka 2022/2023, ajira takribani milioni 1.2 zilizalishwa, na mwaka 2023/2024, idadi iliongezeka hadi takribani milioni 1.8.
Mwaka wa mwisho, 2024/2025, tumeshuhudia ongezeko kubwa la ajira zilizozalishwa, hadi takribani milioni 4.0, jambo ambalo linaleta jumla ya ajira 8,084,204 kwa kipindi kizima.

Ongezeko hili kubwa la ajira mwaka 2024/2025 linatokana na uwekezaji wa kimkakati katika miundombinu na viwanda, pamoja na kuimarika kwa mazingira ya biashara nchini. Hii inaonyesha kuwa juhudi za Serikali na sekta binafsi zimekuwa zikiongezeka kwa kasi zaidi katika miaka ya hivi karibuni.
Mafanikio ya ajira milioni 8.08 yanatokana na sera za kiuchumi zilizorahisisha uwekezaji wa ndani na wa nje. Kati ya Machi na Agosti 2021, Tanzania iliongoza Afrika Mashariki kwa kuvutia uwekezaji wa nje wa Dola za Marekani bilioni 2.9, itakumbukwa kuwa mwaka 2020 Tanzania ilipokea uwekezaji wa Dola za Marekani bilioni 1 licha ya changamoto za UVIKO-19. Hii inaonyesha kuwa sera za Tanzania ziliwaongoza wawekezaji wa kimataifa hata katika kipindi cha mgogoro wa kimataifa.
Serikali imerekebisha sheria za ardhi, kuunganisha mifumo ya kidijitali, na kupunguza utumizi wa makaratasi ili kurahisisha mazingira ya biashara. Kongamano la biashara na uwekezaji yamechochea ushirikiano wa kimataifa, na kusababisha miradi kama upanuzi wa Kiwanda cha Sukari cha Kilombero na uchimbaji wa madini ya nikeli huko Kabanga mkoani Kagera, ambayo imeongeza fursa za ajira na kuimarisha uchumi kwa ujumla.
Mikakati ya Serikali kukabiliana na changamoto zilizopo
Licha ya mafanikio haya ya kuvutia, lakini bado kuna changamoto zinazohitaji kushughulikiwa, ikiwemo utumikishwaji wa watoto katika shughuli za kilimo, migodini, na biashara ndogondogo.
Tatizo hili kwa kiasi kikubwa linasababishwa na umasikini, mafarakano ndani ya familia pamoja na desturi zisizofaa. Ili kuondokana na changamoto hii Serikali na wadau mbalimbali wanapaswa kuweka mkakati wa pamoja wa kijamii na kiuchumi, utakaoleta suluhisho la kudumu.
Ripoti ya Mustakabali wa Ajira ya Jukwaa la Kiuchumi Duniani ya 2023 inaonyesha kuwa kazi za jadi zinaweza kupungua kutokana na maendeleo ya teknolojia, hivyo kuhitaji ujuzi wa Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) na mafunzo ya mara kwa mara.
Aidha, Serikali inapaswa kuendelea kuimarisha elimu ya biashara na ushirikiano na sekta binafsi ili kukidhi mahitaji ya soko la ajira la kisasa. Hii inahitaji uwekezaji katika mafunzo ya ujuzi wa kisasa na kuboresha mfumo wa elimu ili kuwa na kazi za kisasa.
Mazingira ya uwekezaji na makusanyo ya kodi
Mazingira ya uwekezaji yaliyoboreshwa yameimarisha uchumi na kuongeza makusanyo ya kodi ya Serikali. Makusanyo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yamepanda hadi Shilingi za Kitanzania trilioni 3.587 mnamo Desemba 2024, ukuaji wa asilimia 17.59 ikilinganishwa na 2023. Hii inaonyesha kuwa uwekezaji haujaleta tu ajira, bali pia umeongeza mapato ya Serikali ambayo yanaweza kutumika katika miradi ya maendeleo.
Kuboresha mazingira ya biashara na kupunguza changamoto za kiutawala kumeongeza uwepo wa biashara rasmi na kuongeza makusanyo ya kodi, ambapo ajira za kibinafsi zinaongeza mapato ya wananchi, na hivyo kuongeza makusanyo ya kodi ya Serikali.
Tanzania imefanikisha lengo lake la kuzalisha ajira milioni 8.08 kati ya 2020 na 2025, ikiwa ni ushindi wa sera za kiuchumi na ushirikiano na sekta binafsi. Sekta za viwanda, uvuvi, na kilimo zimechukua nafasi ya mstari wa mbele, huku uwekezaji wa kimataifa ukichochea ukuaji wa ajira.
Mafanikio haya yamedhihirisha uwepo wa mikakati sahihi, uthabiti na ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi, vyote hivi kuifikisha Tanzania katika safari yake ya kujenga uchumi wenye nguvu na endelevu.
Mwandishi: Dr. Bravious Kahyoza
Mhariri: Dominic Allen


