Na Yohani Gwangway
Katika Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2025/2026 iliyowasilishwa leo na Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba ambayo ni shilingi za kitanzania trilioni 57, karibu robo ya bajeti hiyo ambayo ni asilimia 24 inatakiwa kulipa deni la serikali litakaloiva kwa mwaka huu wa fedha ambacho ni shilingi za kitanzania trilioni 14.22.
Wakati sehemu kubwa ya Bajeti Kuu ya Serikali ya Tanzania ikilazimika kutafunwa na deni la serikali, pia Bajeti Kuu za Serikali za nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimewasilishwa leo, huku sehemu kubwa ya bajeti hizo zikionekana kulenga kulipa madeni ya nchi husika.
Nchi ya Kenya imeonekana kuwa na bajeti kubwa ikiwa na Ksh. Trilioni 4 ikiwa sawa na trilioni 87 za kitanzania, huku Tanzania ikiwa ya pili kwa ukubwa wa bajeti ikiwa na bajeti ya Tsh. Trilioni 57 ikiwa ni ongezeko la takriban trilioni 3 ikifananishwa na bajeti ya mwaka 2024/2025. Burundi na Somalia zenyewe zina bajeti ndogo zikiwa na Shilingi za kitanzania trilioni 3.6 na 3.53 mtawalia.

Katika kumulika bajeti hizi na kuangalia je, ukubwa na udogo wa bajeti unamaanisha nini kwa nchi husika, Land Dwellers imezungumza na Mtaalamu wa Uchumi na Mchambuzi Dr. Bravious Kahyoza ambaye yeye anasema kila nchi imewasilisha bajeti yake kulingana na uwezo wake kiuchumi pamoja na uwezo wake wa kukusanya kodi.
“Ni kweli bajeti ya Kenya ni kubwa kuliko zote kwa sababu kubwa mbili. Moja, ni ukubwa wa uchumi wa Kenya kulinganisha na nchi zingine za Afrika Mashariki. Ni uchumi ambao una wastani dola bilioni 121, na uchumi unaofuatia ni wa Tanzania ambao ni dola bilioni 89. Sababu ya pili, ni matumizi makubwa ambayo Kenya inayo na sehemu kubwa ya bajeti hiyo inaenda kulipa deni hilo.” Dr. Kahyoza akifafanua kuhusu bajeti za nchi za EAC.
Licha ya Kenya kuonekana kuwa na deni la taifa, Dr. Kahyoza anasema kuwa Kenya ina uwezo mkubwa wa kukusanya mapato ya ndani kulinganisha na nchi zingine za Afrika Mashariki, huku akieleza uwezo wake wa uzalishaji ambao pia uko juu kulinganisha na nchi za zingine.
“Ukiangalia kwa mfano ni kweli kuwa wana (Kenya) deni kubwa la taifa lakini wanao uwanda mpana wa kukusanya mapato na mapato yake ni makubwa kuliko nchi zingine, lakini jambo lingine ni uwezo wa tija katika Uchumi ambao tunaita productivity, Ukiangalia ripoti za IMF, Kenya ina kiwango kikubwa cha tija.”
Akifafanua uhusiano uliopo kati ya ukubwa wa bajeti ya taifa na ukuaji wa uchumi wa nchi husika, Dr. Bravious anasema upo uhusiano ambapo bajeti kwa kiasi kikubwa inatokana na ulipaji kodi.
“Upo uhusiano kati ya ukuaji wa uchumi na ukusanyaji wa mapato (Bajeti). Ukiwa uchumi unakua kuna mambo kama matatu ambayo tunaangalia. Jambo la kwanza, kama uchumi unakua maana yake kiwango cha mtu mmoja kulipa kinakuwa kikubwa na inaitwa Per Capital Revenue. Lakini jambo la pili, linahusiana na matumizi yaani Per Capital Spending, kwamba kila mtu anatumia kiasi gani katika kila sekta. Mfano katika Sekta ya Afya tunapanga bajeti kwa kila mtu kwa kiasi gani. Na jambo la tatu, ni pato la mtu mmoja mmoja yaani Per Capital Income, maana yake kama pato la mtu linaongezeka basi uwezo wake wa kulipa kodi pia unaongezeka.”
Akizungumzia kuhusiana na bajeti ya Tanzania ambayo ni trilioni 57, Dr. Kahyoza amesema bajeti ya tanzania kwa mwaka huu ni bajeti ya uchaguzi. Ameeleza kuwa licha ya bajeti kuwa zana ya kiuchumi, lakini pia bajeti ni zana ya kisiasa kwa hiyo kwa sababu mwaka huu nchi inaingia kwenye uchaguzi basi masuala ya uchaguzi yamepewa nafasi kwa sababu uchaguzi ni suala muhimu kwa taifa la demokrasia.
“Lakini ni muhimu kujua kuwa bajeti ni zana yenye mambo mawili. Ni zana ya kisiasa kwa upande mmoja na ni zana ya kiuchumi kwa upande mwingine. Tanzania inakwenda kwenye uchaguzi kwa mwaka 2025 na hakuna nchi nyingine inakwenda kwenye uchaguzi katika eneo letu. Kwa hiyo bajeti hii ni bajeti ya uchaguzi kwa upande mmoja kwa sababu ni muhimu jambo hilo likafanyika, na tukaweka urari mzuri wa kisiasa. Na utaona kwa kweli katika bajeti za wizara, bajeti imepungua kwa kweli, ukiangalia kwenye Wizara ya Kilimo kwa mfano bajeti imepungua.”

Licha ya bajeti ya Tanzania kuongezeka karibu kila mwaka, Dr. Kahyoza nasema kuna eneo ambalo linahitaji kufanyiwa maboresho. Kuna uwiano wa kodi na pato la ghafi la taifa umebaki kati ya asilimia 12 hadi 13 kwa zaidi ya miaka 10 nchini Tanzania. Ameeleza kuwa jambo hili siyo jambo zuri katika uchumi wetu.
“Jambo moja hatujalifanya vizuri ni kwamba bajeti yetu inatanuka kila mwaka, lakini uwezo wetu wa kuhimili bajeti hiyo bado ni mdogo. Kwa mfano uwiano wa kodi na pato ghafi kwa miaka 10 iliyopita tanzania tumebaki kuwa na asilimia 12 hadi 13 kwa miaka yote 10 na hii siyo ishara nzuri tunapokwenda mbele. Ukiangalia uwiano kwa mfano wa VAT dhidi ya pato ghafi, kiwango chetu bado ni cha chini. Tuna asilimia 6, ni asiliamia 9 nchini Rwanda, ni asilimia 11 nchini Afrika kusini. Haya ni mambo ambayo tunahitaji kuyafanyia kazi.”
kutokana na tofauti kubwa za bajeti kati ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), hasa katika kutekeleza ajenda za pamoja za kimaendeleo, mtaalamu wa uchumi amesema kuwa utofauti huo unaweza kuwa na changamoto kidogo katika malengo ya pamoja ya Jumuiya ya Afrika mashariki (EAC).
“Bila shaka zipo changamoto ambazo zinatokana na utofauti wa bajeti hizi na utofauti huu ukiwa mkubwa kunakuwa na mosi, tofauti zinatofautisha hatua za kimaendeleo za kufanikisha mambo ambayo yanawaunganisha kama Jumuiya. Kwa hiyo nchi moja inakuwa mbele wakati fulani au nchi mbili au tatu. Mfano mzuri ni bajeti ya Afrika Mashariki ambapo Tanzania, Kenya na Uganda zinakuwa mbele kutokana na uwezo wao wa ndani wa mapato.”
Suala la Deni la Serikali upande wa Tanzania
Wakati bajeti hizi zinawasilishwa, suala la ongezeko la deni la serikali nchini Tanzania linaonekana kuwa mjadala huku likionesha kuwa karibu robo ya bajeti inatakiwa kulipa deni hilo kwa mwaka huu wa fedha 2025/2026. Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba malipo ya deni la serikali litakaloiva katika mwaka huu wa fedha ni kapaumbele cha wizara yake. Deni la Serikali litakaloiva ndani ya mwaka wa fedha wa 2025/2026 ni Shilingi za kitanzania trilioni 14.22.
Wakati bajeti kuu ya Tanzania ikiwa ni trilioni 57, maana yake asilimia 24 ya bajeti kuu ya Tanzania inatarajiwa kulipa deni la serikali litakaloiva katika mwaka huu wa fedha. Katika hotuba yake Dkt. Nchemba amesema kuwa deni la serikali sasa limefikia shilingi za kitanzania trilioni 107.7.

Bajeti ya serikali kwa mwaka 2024/2025 ilikuwa shilingi za kitanzania trilioni 49.3, huku serikali ikifanikiwa kukusanya shilingi za kitanzania trilioni 45.07 ikimaanisha ni chini ya makadirio ya bajeti kuu. Zaidi ya trilioni 4.23 hazikusanywa. Kiasi hiki ni sawa na asilimia 8.58 ya makadirio ya bajeti kuu ya serikali kwa mwaka huo.

Mwandishi: Yohani Gwangway
Mhariri: Dominic Allen


