Siku ya Vijana Duniani.

Kwa sasa ni kijana wa miaka 25 ambaye amejiajiri kwenye fursa za kidijitali. Alianza kutumia mitandao ya kijamii mwaka 2015 akiamini kuwa ipo siku mitandao hiyo itamtangaza na kutambulisha kazi zake mbalimbali. Jerome Robert ni mwandishi wa habari kijana anayefanya kazi nyingi za matangazo kwa njia ya mtandao. Hii ni simulizi ya maisha ya vijana waliojiajiri kidijitali wakati leo ni maadhimisho ya siku ya vijana duniani.

Wakati dunia inapitia mabadiliko makubwa kutokana na ukuaji wa teknolojia, rika la vijana ndiyo tegemeo la kuleta mabadiliko kutokana na nguvu walizo nazo na muda wa kutosha wa kuendelea kuzalisha.

Nchini Tanzania idadi ya vijana ilikadiriwa kuwa milioni 21.8 ikiwa ni kwa mujibu wa sensa ya mwisho iliyofanyika mwaka 2022. Vijana hawa ni wale wa miaka 15 hadi 35. Idadi hii ya vijana inafanya asilimia 34 ya watu wote nchini kuwa katika kundi hili. Hii ni kumaanisha kuwa kwa kila kundi la watu 10, basi watu watatu au zaidi ni vijana hapa nchini.

Wingi huu una mahitaji mbalimbali ikiwemo elimu, huduma za afya, ajira na nyinginezo. Wakati dunia ikikabiliwa na kitisho cha ukosefu wa ajira, sekta ya kidijitali inaonekana kuwa mkombozi kwa baadhi ya vijana. Takwimu za umoja wa mataifa (World Youth Report 2020) zinakadiria kuwa kuna vijana bilioni 1.2 kwa makadirio ya mwaka 2020. Tofauti na sera ya vijana hapa nchini ambayo hutambua vijana kama kundi la miaka 15 hadi 35, Umoja wa mataifa hutambua kundi hili kuanzia miaka 15 hadi 24.

Wakati leo dunia inaadhimisha kwa mara ya 25 siku ya vijana duniani, kauli mbiu ya mwaka huu ni “Vijana na matumizi ya fursa za kidijitali kwa Maendeleo Endelevu”. Kauli mbiu ya mwaka huu inaangazia jinsi vijana walivyojiajiri katika sekta za kidijitali.

Hapa nchini vijana mbalimbali wamekuwa wakifanya biashara au kazi za kitaaluma kupitia njia za kidijitali ikiwemo fursa katika mitandao ya kijamii. Jerome Robert ni miongoni mwa vijana milioni 21.8 ambaye yeye amejikita katika kutafuta soko lake kupitia mitandao.

Kijana huyu kitaaluma ni mwandishi wa habari. Akiwa bado mwanafunzi aliona fursa ya kutangaza kazi zake kupitia mitandao ya kijamii. Kwa sasa Jerome anafanya kazi za matangazo lakini sehemu kubwa ya soko lake ikiwa ni mitandao ya kijamii.

“Huwa ninahusika na utengenezaji wa matangazo ya aina mbalimbali, ikiwemo ya sauti na vidio, lakini pia graphic design. Hizi ni kazi zangu. Kila kazi ambayo ninaifanya ya kampuni fulani au wateja fulani, basi huwa inanilazimu mimi kuweka katika mitandao yangu ya kijamii ili kuonesha ni kazi gani naifanya”. Anasema Jerome Robert ambaye ni mwandishi wa habari

Kufanya kazi kutokana na maendeleo ya kiteknolojia ambayo yanafanya dunia kuwa kama kijiji, kumemfanya Jerome kufanya kazi na wateja ambao hajawahi kuwaona lakini wanamwamini kutokana na kazi zake. Jerome anakiri matumizi haya ya mitandao yamemfanya kutambua na kulifikia soko la watu ambao isingekuwa rahisi kuwafikia ana kwa ana.

“Matumizi ya mitandao yamenibadili namna ya kulifikia soko langu, ilikuwa zamani mtu hadi akusikie sehemu fulani. Lakini sasa hivi imekuwa rahisi sana. Ninaweza kusambaza kazi yangu katika mitandao ya kijamii kama Facebook, Tik Tok, Instagram na Youtube. Nikiweka kazi zangu kule watu wanaziona. Kuna wengine wanitafuta ili kufanya nami kazi”. Anasema Jerome

Vijana wakichangamkia fursa za kidijitali, kuna hofu ya kuongezeka kwa tatizo la ukosefu wa ajira duniani pamoja  na ukosefu wa usawa wa kiuchumi. Ripoti ya “Mienendo ya mtazamo wa dunia wa ajira na kijamii 2024- WESO Trends inaonesha kuimarika kidogo kwa hali ya ajira duniani kulinganisha na wakati wa UVIKO-19.

Kwa mfano, ripoti ya shirika la kazi duniani ILO mwaka 2023 ilionesha kuwa ukosefu wa ajira ulikabili asilimia 5.1 ya watu kote duniani ikilinganishwa na asilimia 5.3 mwaka 2022. Lakini kuna hofu katika masuala ya ajira duniani licha ya ahueni kidogo mwaka 2023.

Moja ya changamoto ambayo inawakumba vijana waliowekeza katika uchumi wa dijitali mfano wasanii ni suala la Haki Miliki.

Kijana Lenis Leonard Kagera anajishughulisha na shughuli za kuimba na kazi zake huzisambaza kwa njia ya kidijitali kwa ajili ya mashabiki zake.

Lenis anapitia changamoto ya Haki Miliki kwa ni rahisi mtu kuiba kazi zake.

“Hiyo ina madhara kwa sababu yule mtu akitumia maudhui ambayo umeyatumia atakunyima nafasi, kwa hiyo hautapata nafasi yoyote kwa sababu kitu utakacholeta hata mtu akisikiliza kazi yako atasema huyu kaiga .

  Tatizo la ajira kwa vijana nchini Tanzania linakabili asimilia 12 ya vijana wote. Hii ni kwa mujibu wa hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliyoitoa mkoani Kagera mwaka 2022 akirejea utafiti uliofanywa na Ofisi ya takwimu ya Taifa mwaka 2021.

“Asilimia hii 12 ya vijana ni wengi sana, kwa sababu idadi ya watanzania wengi ni vijana, kuliko watoto kuliko wakubwa. Kwahiyo kazi yetu sasa ni kuhakikisha asilimia hii 12 tunaijengea uwezo, tunaipa ujuzi ili iweze kujiajiri na iweze kuajiriwa”. Alisema Rais Samia Suluhu Hassan katika hotuba yake aliyitoa akiwa mkoani Kagera.

Kulinganisha takwimu hii na matokeo ya sensa ya watu na makazi iliyofanyika mwaka 2022 ambayo ilionesha vijana wa umri kati ya miaka 15 hadi 35 kukadiriwa kufika milioni 21, basi kati yao vijana milioni 2 na nusu hawana kazi.

Mtaalamu wa masuala ya uchumi Dk. Bravious Kahyoza anautazama uchumi wa kidijitali kama suluhisho la ukosefu wa ajira kwa vijana.“Hakika uchumi wa kidijitali ni sehemu muhimu ya kupambana na tatizo la ajira hapa nchini na maeneo mengine. Uchumu huu wa kidijitali unatoa nafasi nzuri ya kujifunza na kupata taarifa zaidi na kujua ni kitu gani kinaendelea pahala gani na ni fursa gani ambayo naweza nikaipata hapa kwetu nyumbani, nje ya nchi au kupitia kwa marafiki.” Alisema

Dk. Bravios anaongeza kuwa  ili vijana waweze kujiajiri vizuri katika uchumi wa kidijitali, serikali inapaswa kuwekeza kwenye miundombinu ya umma ya kidijitali.

“Serikali kuwekeza vilivyo  kwenye kitu kinaitwa miundombinu ya umma ya kidijitali zinaitwa Digital Public Infrastructure, kama ambavyo serikali zimekuwa zikiwekeza kwenye miundombinu kama hard economic infrastructer kama barabara reli na vitu vingine vya namna hiyo, mjadala mkubwa sasa hivi duniani ni kwamba nchi lazima ziwekeze pia kwenye miundombinu ya umma ya kidijitali na hapa unazungumza njia ambazo ni rahisi zaidi kuweza kuwafanya watu au vijana kuwasiliana kwa haraka amba kwa gharama zilizo nafuu .”

Umoja wa mataifa unatambua kundi la vijana kama kundi muhimu linalohitaji kuandaliwa ili kutatua chanagamoto zinazoikabili dunia. Kupitia Malengo ya maendeleo endelevu, kundi la vijana linahusika pakubwa katika lengo la 4 yaani kupata elimu bora, 8 ambayo mazingira mazuri ya kazi  na ukuaji wa kiuchumi na lengo la 13 ambalo ni kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi.

Kwa mukatadha huu, vijana pia wanahusika au kuguswa na malengo mengine tofauti na haya. Nchini Tanzania, vijana wanaohitimu vyuo vikuu wanakutana na changamoto ya ajira. Kwa sasa kunakadiriwa kuwa ni wastani wa wahitimu wa vyuo vikuu 54000 kila mwaka ambao karibu wote ni vijana. Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya TCU ambayo haijahusisha vyuo vya kati,

Uchumi wa kidijitali pamoja na fursa zake hazikwepiki katika taifa linalohitaji kuwa na vijana ambao ni chachu ya mabadiliko ya kiuchumi. Licha ya watumiaji wa huduma ya intaneti kuongezeka kutoka watu milioni 29 mwezi Juni mwaka 2022 hadi watu milioni 34 mwezi Septemba mwaka 2023, hakuna uhakika ni kwa kiasi gani vijana wa kitanzania wanatazama mabadiliko haya kama soko la kazi, weledi au ujuzi wao na kuuuza kupitia mitandao.

Licha ya changamoto ya ajira katika sekta za kiuchumi kwa vijana, bado kuna fursa  za kidijitali kwa vijana ambao wako tayari kujifunza na kutoa huduma zao kwa njia za kimtandao. Kuna faida na fursa anuwai za kutumia njia za kidijitali katika kunyanyua kipato cha kijana kama ifuatavyo

Kupata masoko kwa urahihisi

Katika uchumi wa kidijitali au myororo wa matumizi ya mitandao kunyayua uchumi vijana wanayo fursa ya kupata soko kubwa la bidhaa au huduma wanayoitoa kama watatumia mitandao kusambaza na kutangaza kazi zao tofauti na kipindi ambacho ili kazi yako ijulikane lazima ukutane na soko lako ana kwa ana. Kama vijana wa kitanzania watatumia fursa hii na serikali ikaboresha sera zake katika masuala ya kidijitali basi itakuwa rahisi kwa vijana kupata masoko ya ubunifu, ujuzi, bidhaa au huduma wanazotoa kwa urahisi zaidi.

Mtazamo wa Dk. Bravious Kahyoza ni kuwa uchumi wa kidijitali umepanua wigo zaidi katika sekta ya biashara.

“Moja ni sekta ya ubunifu kwa sehemu kubwa sana ina nafasi kubwa sana kwenye uchumi wa kidijitali kwa sababu ni eneo ambalo unaweza kupeleka bidhaa, tukiita bidhaa yaani kile unachokizalisha na kuweza kuwafikia watu wengi ndani pale ulipo lakini hata nje ya mipaka ya nchi.” Alisema Dk. Bravious

Kuokoa muda

Matumizi ya kidijitali kwa vijana katika shughuli zao za kiuchumi yanaokoa muda ambao ungeweza kutumika kutafuta fursa au hata kufanya biashara na  mtu fulani. Kwa mfano, kama kuna kijana Mbeya ambaye ni mpiga picha mzuri na akaweka kazi zake katika mitandao ya kijamii, basi ni rahisi kijana huyo kupata watu wengi wenye kuhitaji huduma yake ndani ya muda mfupi bila kuonana nao. Hii inaondoa muda ambao ungetumika kuonana ana kwa ana na kuanza kuelezea kazi zake. Hivyo basi, kama vijana wataamua kujitangaza na kutumia fursa ya kidijitali wanaweza kutumia mtu mfupi kufanya kazi tofauti tofauti ili kujiingizia kipato

Gharama kidogo

Matumizi mazuri ya fursa za kidijitali yanapunguza gharama za mtu kusafiri kupeleka huduma na badala yake mtu anaweza kutumia mitandao kutoa huduma. Kwa mfano, sasa hivi kuna wachungaji wanatoa huduma ya maombi kwa njia ya mitandao, kuna watu wanaendesha mafunzo kwa njia ya mitandao, kuna wengine wanasoma kwa njia ya mitandao. Yote haya ni fursa za kidijitali ambazo zimekuja kuleta mapinduzi ya namna ya kufanya kazi.

Akili bandia/mnemba

Fursa ya kutumia akili bandia (Artificial Intelligence-AI) inakua kwa kasi kote duniani. Katika upande wa kidijitali akili bandia zimekuwa msaada mkubwa ambazo kama vijana wataamua kuwa na ujuzi wa namna ya kuzitumia basi watapata faida za kiuchumi. Kwa mfano, akili bandia kwa sasa inatumika na watengeneza maudhui ya mitandaoni (online content creators), na kurahisisha utendaji wao wa kazi.

Nchini Tanzania bado hakuna sera rasmi ya matumizi wa akili bandia. Sasa ni wajibu wa serikali kuandaa sera nzuri itakayosimamia na kuthibiti akili bandia. Vijana ambao wanataka kuboresha kazi zao mitandaoni wanaweza kujiandaa kwa matumizi ya AI na kubadilisha kabisa ubora wa huduma zao.

Katika maadhimisho ya 25 tangu kuanza kutambuliwa rasmi kwa siku ya vijana duniani mwaka 1999, sasa ni wajibu wa vijana kuzitumia fursa za kidijitali katika kuleta maendeleo endelevu, huku serikali ikiandaa mazingira mazuri kwa vijana hawa kujiajiri. 

Maadhimisho ya siku ya vijana mwaka huu yatafanyika mkoani Dodoma ambapo yanatarajiwa kuhudhuriwa na vijana zaidi ya 3000 kote nchini.

Mwandishi: Yohani Gwangway
Mhariri: Dominic Allen

Hot this week

CHADEMA kutoa msimamo wake kuhusu maridhiano

By Veronica Mlyatu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa...

Mnyonge, mnyongeni ila haki yake mpeni

By Dorlingson Edward Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), leo...

Popular Articles

Safari ya Mashimba katika kutetea jamii ya Wahadzabe

Nchini Tanzania  kuna jumla ya makabila zaidi ya 120...

Polisi waendelea kuwashikilia viongozi wa CHADEMA

Ni siku ya kwanza tangu kukamatwa kwa viongozi wa...

BWAWA LA ARBA’AT  LASABABISHA MAAFA NCHINI SUDAN

Watu 30 mashariki mwa Sudan na na wengine 60...

Sand Mining in Tanzania: Trails of Destruction in Lake Victoria and its Environs

By Dominic Allen On November 14th, 2021 in the Geita...

 Utekaji: Fumbo linalotushinda?

Na Yohani Gwangway Taifa la Tanzania kwa miaka mingi limekuwa...

Abduction: Is it a riddle we can’t solve?

By Yohani Gwangway For many years Tanzania has been an...

Mustakabali wa Hewa Safi kwa kila kiumbe

Na Dominic Allen Msingi wa maisha ya viumbe hai yaani...

Clean Air for Every Creature

By Dominic Allen Survival of all living and non-living organisms...
LAND DWELLERS FACT CHECK HUB VERIFY FACTS STOP MISINFORMATION Trusted Fact-Checking in Tanzania Beyond What You Know VERIFY NOW

Related Articles

Popular Categories

DWELLERS CHECK-HUB Verify Facts. Stop Misinformation Trusted Fact-Checking in Tanzania • Beyond What You Know VERIFY NOW