
Benki Kuu ya Tanzania (BOT), imepiga marufuku programu 69 za mikopo ya mitandaoni nchini kwa kufanya kazi bila kusajiliwa.
Taarifa iliyotolewa na BOT Novemba 21, 2024 imesema kuwa progamu hizo hazijakidhi vigezo vya matakwa ya mwongozo kwa Watoa Huduma Ndogo za Fedha wa Daraja la Pili wa mwaka 2024.
BOT imeongeza kuwa mwongozo huo umelenga kuimarisha usimamizi kwa watoaji wa huduma ndogo za fedha wa Daraja la Pili ili kuhakikisha uwazi, uwekaji wa riba na tozo, njia za ukusanyaji madeni, usalama wa watumiaji wa huduma hizo na utunzaji wa taarifa binafsi.
Katika hatua nyingine, BOT imetoa tahadhari kwa wananchi kutochukua mikopo kutoka kwenye programu hizo kama vile PesaX, CashX, Hakika Loan na nyinginezo ambazo zimeshapigwa marufuku kwa kukosa vigezo.


