Na Dkt. Bravious Kahyoza
Tanzania imezidi kupiga hatua chanya katika maendeleo ya uchumi wake, jambo linaloifanya kuibuka kama moja ya mataifa yanayokua kwa kasi katika bara la Afrika. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Januari 08, 2025, inaonesha matarajio ya ukuaji wa uchumi kufikia asilimia 6 kwa Tanzania Bara na asilimia 6.8 kwa Zanzibar kwa mwaka 2025.
Miongoni mwa mambo yanayotazamiwa kuchangia sehemu kubwa katika ukuaji huo wa uchumi nchini, ni ongezeko la uzalishaji katika shughuli za kilimo, utekeleza wa miradi ya ujenzi, maboresho katika usafirishaji na ugavi, nishati pamoja na utekelezaji wa sera za fedha na kibajeti.
Licha ya matarajio hayo ya kukua kwa uchumi, giza la umaskini bado limetanda kwa Watanzania walio wengi. Hali hii imechangiwa ni nini hasa? Kwanini ukuaji wa uchumi hauakisi maisha ya watu? Na kama Taifa lenye malengo bora kuhakikisha tunasonga mbele tunawezaje kutoka hapo. Makala hii inamulika kuhusu tatizo la umaskini licha ya kukua kwa uchumi nchini pamoja na juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kupambana na umaskini.
Hapo jana Mei 27, 2025 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kulifanyika Kongamano Maalum ambalo liliangazia Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) unavyoweza kuchochea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Kongamano hili ambalo liliandaliwa na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC) kwa kushirikianana Taasisi ya Utafiti na Elimu kwa Demokrasia Tanzania (REDET), pia lilijadili kwa undani tatizo la umaskini nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Benki ya Dunia (WB) iliyotolewa mwaka 2024 yenye jina Sayari, Ustawi na Umaskini imeeleza kuwa karibia watu milioni 700 ambao ni sawa na asilimia 8.5 ya watu duniani ni maskini wa kupindukia, wanaishi chini ya USD 2.15 kwa siku. Kwa ukanda wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwa ni mojawapo, wenye watu bilioni 1.27, asilimia 67 ya watu wake ni maskini wa kupindukia.
Katika kuangalia hali ya umaskini mbali na kuangalia kigezo cha viwango vya mapato na matumizi, vigezo vingine hutazamwa katika nyanja ya uchumi, huduma za jamii, nishati na ujenzi wa miundombinu, vyote vikiwa ni viashiria vya msingi katika kupima maendeleo ya watu. Nchini Tanzania kumekuwa na mjadala mpana kuhusiana umaskini na maendeleo ya watu, katika Ripoti ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2024/25 iliyotolewa na Tume ya Mipango mnamo Juni 2024 ilibainisha kuwa ukuaji wa idadi ya watu unaongezeka kwa kiwango cha asilimia 3.2 kila mwaka huku ukuaji wa uchumi ukiendelea kuwa asilimia 5 kila mwaka.Ripoti hiyo imeweka bayana kuwa ukuaji wa uchumi hauendani na jitihada za kupunguza umaskini hususan katika kuimarisha matumizi ya bidhaa na huduma kwa umma ikiwemo miundombinu na huduma za kijamii.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), Mhe. David Kafulila anaiona njia ya kupiga hatua kuwaokoa Watanzania kutoka kwenye dimbwi la umaskini, akirejelea utafiti uliofanywa na Taasisi ya Research on Poverty Alleviation (REPOA) ambao pia uligusia umuhimu wa kuiinua Sekta ya Kilimo katika kupunguza tatizo la umaskini nchini.
“Research on Poverty Alleviation (REPOA) walifanya utafiti wao mwaka 2006 na kuonesha kwamba tukikuza Sekta ya Kilimo katika dhana pana kwa asilimia 10 kwa miaka mitatu mfululizo, tutapunguza umaskini kwa asilimia 50″ amesema Mhe. Kafulila.
Mhe. Kafulila ametoa mchango huo wakati akizungumza katika Kongamano hilo ambalo limejadili kuhusu Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) unavyoweza kuchochea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambapo pia Sekta Binafsi imetajwa kwenye Dira hiyo kama mhimili mkuu wa ukuaji wa uchumi nchini.
“PPP itaipa zaidi nafasi serikali kwenye maeneo haya yanayopunguza umaskini hususan afya na elimu. Shida kubwa ya sisi kushindana ipo kwenye maarifa zaidi. Leo duniani wanasema maarifa ndiyo sarafu ya dunia, nchi duniani zinashindana kwa kiwango cha maarifa, lakini unawezaje kuwekeza kwenye maarifa kama unakabiliwa na majukumu ya barabarani…majukumu ya ujenzi wa bandari yanakuhitaji…kwa hiyo tunapozungumza Ubia tafsiri yake tunaipa serikali nafasi ya ili kusudi iwekeze hasa kwenye haya maeneo ambayo yanaweza kutusaidia kujenga rasilimali watu”ameeleza Mhe. Kafulila.

Chapisho la Aprili 04, 2025 la Benki ya Dunia (WB) lililoangazia hali ya uchumi nchini Tanzania limeonesha kuwa Pato la Wastani kwa mtu kwa mwaka ni USD 1,149. Katika chapisho hilo Sekta ya Kilimo nchini imetajwa kuchangia takriban robo ya jumla ya thamani ya uzalishaji, Sekta ya Viwanda theluthi moja huku sehemu iliyobaki ikiwa ni Sekta ya Huduma.
Benki ya Dunia (WB) imeeleza kuwa Sekta ya Kilimo nchini Tanzania ndiyo chanzo kikuu cha ajira, ambapo kati ya kila Watanzania watatu, wawili wanafanya kazi katika sekta hiyo.
Serikali ya Tanzania katika kutambua mchango wa Sekta ya Kilimo katika vita hii ya kupambana na umaskini, imeendelea kufanya jitihada mbalimbali, ikiwemo kuongeza bajeti katika Wizara ya Kilimo. Ikumbukwe kuwa wakati Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani mwaka 2021 bajeti ya wizara hiyo ilikuwa ni chini ya Tsh. Bilioni 300, ambapo ndani ya miaka minne bajeti imefika Trilioni 1.242.
Je, ongezeko hili la bajeti litawezesha kwa kiasi gani katika kukabiliana na umaskini nchini? Huu ni mtazamo wa Mtaalamu wa Masuala ya Uchumi, Dr. Bravious Kahyoza.
“Inasaidia kupunguza athari za mfumuko wa bei hasa za vyakula. Hii ni muhimu kwa sababu zaidi ya 60% ya Pato la Watanzania hutumika kwenye chakula. Vilevile inasaidia kuongeza vipato vya watu kwani tija kwenye uzalishaji kwenye Kilimo inaongezeka kwa sababu bajeti ya pembejeo inaongezeka. Lakini pia maana yake itaongeza uwezo wa watu kutumia (consumer spending) kwenye mchumi” amesema Dr. Kahyoza.
Kutokana na umuhimu wa Sekta ya Kilimo, Mhe. David Kafulila ameguswa na ongezeko la bajeti pamoja na uwekezaji katika katika Sekta ya Kilimo, huku akishauri kuwa uwekezaji zaidi bado unahitajika katika sekta hiyo.
“Unaweza ukaona kwamba kuna uwekezaji mkubwa sana kati ya mwaka 2021 na leo kwenye Sekta ya Kilimo, kuongeza bajeti na maeneo ya umwagiliaji kutoka hekta 500,000 mpaka hekta 900,000 ni mabadiliko makubwa sana, hata hivyo haitoshi ukilinganisha na hitaji la nchi katika hilo eneo. Kwa hiyo kuna wawekezaji ambao wamekwisha kuonesha kuvutiwa kuwekeza kwenye maeneo ya umwagiliaji”amesisitiza Mhe. Kafulila.

Katika Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeeleza kuwa Tanzania inatakiwa kubuni na kuibua vyanzo vipya vya mapato ili kukidhi mahitaji ya maendeleo, ambapo imevitaja vyanzo hivyo kuwa ni pamoja na masoko ya fedha na mitaji, Ushirikiano wa Sekta ya Umma na Binafsi pamoja na Uhisani wa kibinadamu.
Rasimu ya Dira hii imeona umuhimu wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) katika kuchagiza maendeleo ya Taifa na kuinua maisha ya Watanzania, Dr. Kahyoza anaona tuna nafasi ya kuifikia nchi ya ahadi kama tutatilia mkazo kwenye PPP.
“Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) unasaidia kuongeza mitaji, ubunifu na teknolojia, lakini pia kuongeza ufanisi kwenye uchumi na kusaidia kugatua mitaji kwa wananchi wengi”ameongeza Dr. Kahyoza.

Umoja wa Mataifa (UN) umeweka Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu yakikusudia kushughulikia changamoto za dunia ili kuwa na mustakabali endelevu ifikapo mwaka 2030, ambapo Lengo namba moja ni “Kumaliza Umaskini Duniani”.
Katika lengo hilo la kumaliza umaskini, limedhamiria kuondoa umaskini wa kupindukia, kuhakikisha watu wote hasa maskini wanakuwa na haki sawa za rasilimali za uchumi, upatikanaji wa huduma za msingi na udhibiti wa ardhi na rasilimali zingine.
Ripoti ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2024/25 iliyotolewa na Tume ya Mipango mwezi Juni 2024, imekiri kuwa ukuaji wa uchumi nchini umekuwa ukitegemea uwekezaji wa umma katika miundombinu huku Sekta Binafsi ikionekana kutochukua nafasi yake kikamilifu katika kuchochea ukuaji wa uchumi kama ilivyotarajiwa, ambapo imesisitiza kuwa uwekezaji kupitia Sekta Binafsi ndiyo unatarajiwa kuchochea ajira na uzalishaji nchini Tanzania.
Bila shaka Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) una nafasi kubwa katika maendeleo ya nchi. Baadhi ya wadau mbalimbali walioshiriki Kongamano hilo wamekipongeza Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC).
Dr. Kafigi Jeje ambaye ni miongoni mwa watoa mada aliipongeza PPPC kwa juhudi kubwa ambazo mpaka sasa imezifanya.
“Wameweza kuwezesha halmashauri zote 184 nchi nzima kwa mwaka huu. Zaidi ya viongozi wa halmashuri 2800 wamepata mafunzo, watu wamewezeshwa wameibua miradi, lakini PPPC bado inachakata inaona miradi mingine”amesema Dr. Jeje wakati akitoa maoni yake kuhusiana na PPPC chini ya Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Mhe. David Kafulila.
Dr. George Malonga ambaye ni mshiriki katika kongamano hili amesisitiza kuhusu elimu ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi kutolewa kwa watu ili kuwajengea uelewa zaidi.
“Tunaomba watu wetu tuwapeleke darasani, kuhusiana na hiki kipindi (PPP), kama vile tunavyowapeleka watoto shuleni kuhusiana na ‘field zao na discipline mbalimbali’ wanatoka wakiwa wameiva vizuri” amesisitiza Dr. Malonga.
Hata hivyo pendekezo lilitolewa kushauri uwepo wa makongamano ya namna hii nchini ambayo yatawakutanisha viongozi wa serikali, Wakuu wa Taasisi mbalimbali pamoja na wasomi, kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yenye maslahi kwa Taifa.
“Iwe ni midahalo ya kudumu kwamba badala ya kumleta tu Kafulila leo, tutegemee baadae mtuletee Mawaziri lakini hata Wakuu wa Taasisi mbalimbali ili Chuo Kikuu kiendelee kuwa chachu ya kuibua hii mijadala”amependekeza Dr. David Rwehikiza.

Kwa kuzingatia hali halisi ya Tanzania, ni dhahiri kuwa ukuaji wa uchumi pekee hauwezi kuwa tiba ya umaskini unaoendelea kuwatesa wananchi, hivyo ili kufanikisha maendeleo jumuishi na endelevu, kuna haja ya kushirikisha kikamilifu Sekta Binafsi kupitia mifumo ya Ubia kuhakikisha sera na rasilimali zinaelekezwa moja kwa moja katika maeneo yenye athari za moja kwa moja kwa wananchi, hususan Sekta ya Kilimo na Sekta ya Huduma za Kijamii. Kupitia utekelezaji madhubuti wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), Tanzania inaweza kuboresha maisha ya Watanzania na kuondokana kabisa na umaskini.
Ni wazi kuwa ustawi wa taifa hauwezi kupimwa kwa viwango vya ukuaji wa uchumi pekee, bali kwa namna ambavyo wananchi wanashirikishwa na kunufaika moja kwa moja na matunda ya maendeleo. Ili kuleta mabadiliko ya kweli na ya kudumu, ni muhimu kwa Tanzania kuimarisha ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Binafsi, hasa katika maeneo yenye umuhimu zaidi kama kilimo na huduma za kijamii. Kwa kuweka msukumo zaidi katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), taifa linaweza kujenga mazingira yenye usawa wa kiuchumi na kijamii, hatimaye kufuta kabisa umaskini nchini Tanzania.
Mwandishi: Dkt. Bravious Kahyoza
Mhariri: Dominic Allen


