Nondo: Viongozi wenye mamlaka hawataki kukiri kama ukosefu wa ajira ni tatizo kubwa nchini

Hotuba na Abdul Nondo

Napenda kutoa shukrani kwa idara ya SCaRO Baraza Kivuli ACT-Wazalendo  kwa kuandaa mjadala huu muhimu wa ukosefu wa ajira Tanzania. Hii ni Agenda muhimu ambayo Ngome ya vijana ACT–Wazalendo tumekuwa tukiibeba na tutaendelea kushirikiana na makundi yote Tanzania kuhakikisha sote kwa pamoja tunabeba Agenda hii. Nakuamsha vuguvugu la kudai suluhu na utatuzi wa tatizo la ukosefu wa Ajira Tanzania ambalo ni tatizo kubwa linalotukumba zaidi kundi la vijana chini ya umri 35 ambao takribani 70% ya idadi ya watu wote na vijana ndio nguvu kazi kubwa sawa na 55.6% ya nguvu kazi yote.

Leo hii ndani ya nchi yetu ukitamka neno ukosefu wa ajira unaonekana mchochezi dhidi ya serikali. Na wengi viongozi wenye mamlaka hawataki kukiri kama ukosefu wa ajira ni tatizo kubwa nchini ambalo linahitaji uvumbuzi wa haraka. Wao wanakimbilia utetezi ya kwamba tatizo la ajira ni tatizo la kiulimwengu,kidunia kwa nchi zote hata Marekani, Ulaya na China kuna tatizo la ukosefu wa ajira, nakubaliana ya kwamba tatizo la ajira ni la kiulimwengu ila nchi hizo za Ulaya, Marekani na China wana mikakati madhubuti ya utatuzi wa tatizo la ukosefu wa ajira katika nchi zao. Je, sisi mikakati yetu madhubuti ni ipi? Hoja za namna hii ni hoja za kukwepa uwajibikaji wa kutafuta suluhu madhubuti wa tatizo la ukosefu wa ajira ndani ya nchi yetu. Tatizo la ukosefu wa ajira  linazidi kuwa kubwa na ni bomu linalosubiri kuripuka ikiwa halitatuliwa. Vijana wenzangu tusimame,tuungane  na tupaze sauti zetu dhidi ya ukosefu wa ajira na hatma yetu.

Kwa mujibu wa takwimu ya nguvu kazi (Integrated labour Force Survey 2021) na Sera ya Maendeleo ya Vijana ya 2007, toleo la 2024 inasema kwa mwaka vijana 1,000,000 ambao ni nguvu kazi wenye uwezo wa kufanya kazi huingia kwenye soko la ajira ila ni vijana 200,000 tuu ndio hupata ajira sekta rasmi aidha sekta ya umma/serikali au binafsi kama vile ualimu,uuguzi,viwandani, kwenye makampuni n.k, huku vijana takribani 800,000 kwa mwaka wakiachwa nje ya mfumo wa uzalishaji na ajira huku wakiishia kuwa tegemezi  na wengine wakiamua kujiajiri na kuingia kwenye sekta isiyo rasmi kama bodaboda, mama lishe, machinga na wengine ambao wote hawa hawajui hatma yao, hawana uhakika wa kesho yao na hawana sehemu za uhakika kwa shughuli zao.

Vijana katika sekta isiyo rasmi wapo 80% wanateseka, wanafukuzwa kila uchwao, wanahamishwa na kukimbizwa kila uchwao, wananyanyaswa kila uchwao. Hawana bima kwa afya zao wala pension kwa kesho yao. Ndiyo maana nasema Vijana wenzangu tusimame, tuungane na tupaze sauti zetu dhidi ya ukosefu wa ajira na hatma yetu.

Shughuli zisizo rasmi zinakuwa kwa kazi kutoka 10.1% mwaka 2006 hadi 59.9% mwaka 2022 . Hii sio ishara njema kwa nchi yetu, siyo ishara njema kwetu vijana. Hii ina ashiria ya kwamba kuna kusinyaa kwa utengenezaji wa ajira katika sekta rasmi, inaashiria kuna kusinyaa kwa shughuli za uzalishaji za kiuchumi zinazotengeneza ajira rasmi,inaashiria kuna kusinyaa kwa jitihada za serikali katika kurasimisha sekta zisizo rasmi kuwa sekta rasmi kupitia uwezeshwaji wa kifedha (Mikopo), misamaha au punguzo la kikodi (Tax holiday), ujuzi, maeneo ya uhakika ya kufanyia biashara. Kukosekana kwa jitihada hizi kuna sekta isiyo rasmi kuzidi kupanuka na sekta rasmi kusinyaa. Ndiyo maana nasema Vijana wenzangu tusimame,tuungane  na tupaze sauti zetu dhidi ya ukosefu wa ajira na hatma yetu.

Hata Vijana wachache walio kwenye sekta rasmi, kazi wanazofanya sio za staha (indecent Jobs) ni kazi hohe-hahe. Wanalipwa kidogo sana (underpaid) mshahara /ujira wao hauwawezeshi kupiga hatua yeyote zaidi ya kulipa nauli,kodi ya nyumba ya kawaida na kula chakula cha kawaida sana.Mfano walimu,wafanyakazi viwandani,ulinzi na kwenye makampuni binafsi. Wengi kazi zao hazina mikataba,wengi pia hawana bima ya afya, mishahara yao kuchelewa, wengi hawana mfumo wa akiba kupitia mfuko ya hifadhi ya jamii (pension). Wanafanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi. Ndiyo maana nasema Vijana wenzangu tusimame,tuungane  na tupaze sauti zetu dhidi ya ukosefu wa ajira na hatma yetu.

Vyuo vyetu nchini Tanzania kwa mwaka vinazalisha zaidi ya wahitimu 55,000 (TCU, VitalStats, 2021). Hawa walianza kuambiwa wajitolee nguvu kazi zao bure ndio waajiriwe ,wakambiwa wajiajiri na sasa hivi wanaambiwa Waende VETA (Ufundi Mchundo). Kauli hii inalenga kukwepa wajibu wa serikali ,kauli hii inalenga kuwapa zigo la lawama wahitimu wa vyuo kwa kuonesha ya kwamba walikosea kusoma elimu ya nadharia hadi chuo kikuu badala ya kwenda VETA ambapo ndio kuna ajira. Wahitimu wa vyuo sasa wanaitwa ni nguvu kazi isiyo na ujuzi inayozalishwa kwa wingi kuliko mahitaji. Je, ni kweli hakuna mahitaji? Nchini kwetu hadi sasa tuna jumla ya wahitimu walimu 146,000 waliopo mtaani bila kazi huku shule zetu nchini tukiwa na uhaba wa walimu 279,202. Hata tukiajiri walimu wahitimu wote 146,000 leo bado tutakuwa na uhaba wa walimu 133,202. Ndiyo maana nasema Vijana wenzangu tusimame,tuungane na tupaze sauti zetu dhidi ya ukosefu wa ajira na hatma yetu.

Je, VETA ni suluhu ya utatuzi wa changamoto ya ajira? Tujiulize tuna VETA ngapi nchini tukilinganisha na mahitaji, tujiulize kijana akimaliza VETA uwezeshwaji (Mikopo) kwake upoje ili aweze kujiajiri? Kwa mujibu wa NACTVET hadi kufikia Januari, 2025 kuna Jumla ya vyuo vya VETA 91 vya umma/serikali na vya binafsi 814. Mfano halisi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Vijana ,Kazi na Ajira) kila mwaka hutoa fursa kwa vijana bure kwenda VETA kwa miezi kadhaa. Mwaka huu Januari 30 2025 dirisha lilifunguliwa hadi tar. 12 Februari 2025 ili vijana kuomba kwa vyuo 52 na nafasi zilikuwa 8000 tuu kwa vyuo  52 nchi nzima. VETA binafsi ya Don Bosco Dar es salaam ilipewa nafasi 250 tuu ila hadi siku ya Dirisha kufungwa tarehe 12 Februari, Don Bosco ilikuwa imepokea tayari maombi 8,789 kwa chuo kimoja, zaidi ya idadi iliyohitajika kwa vyuo vyote. Hii inaonesha uhitaji wa VETA kuwa mkubwa kwa vijana huku miundombinu ya kutokidhi na kutokuwa kipaumbele chao ndio maana hadi sasa suala la kuwa na VETA kila wilaya imebakia ndoto, maneno na ahadi. Lakini je, wanaohitimu VETA wanawezeshwa namna gani? Takwimu za nguvu kazi (2021-ILFS) inasema 10.5% ya wahitimu wa VETA  hawana ajira. Maana yake ni kwamba lazima tuwe na mipango uwezeshwaji kwa hawa vijana baada ya VETA. Ndiyo maana nasema Vijana wenzangu tusimame,tuungane  na tupaze sauti zetu dhidi ya ukosefu wa ajira na hatma yetu.

Mfumo wetu wa elimu pia unapaswa kubadilishwa, nimepitia Sera ya Elimu ya 2014, toleo la 2023 na mitaala iliyoboreshwa. Nawaombeni pia ambao hamjasoma mpate  kusoma. Kama itatekelezwa ipaswa mitaala hii na sera hii mfumo wetu wa elimu unakwenda kubadilika sababu wametambulisha Elimu ya Uwili = Mkondo wa Amali na Mkondo wa Jumla. Elimu ya lazima kuwa miaka 10 na masomo kadhaa ya ujuzi yametambulishwa. Changamoto ni moja tuu utekelezaji. Utekelezaji wake unahitaji fedha nyingi sana ili kuajiri wakufunzi, vifaa, karakana, miundombinu .Na hii serikali yetu elimu kwao ni kama sio kipaumbele. Bila dhamira ya kweli ya kisiasa, kubana matumizi, kuzuia ufisadi na matumizi ya fedha yasio ya lazima hakuna chochote kitakachotekelezwa . Sera ya 2014 ilikuwa nzuri pia ila haikutekezwa sababu ya uhaba wa fedha (Policy Forecast = Trend  Extrapolation) Vijana wenzangu tusimame,tuungane  na tupaze sauti zetu dhidi ya ukosefu wa ajira na hatma yetu

Kilimo ni sekta inayochangia utengenezaji wa ajira kwa 66% ,  kwa mujibu wa takwimu ya sera ya maendeleo ya vijana ya 2007 toleo la 2024 , na takwamu za nguvu kazi Integrated Labour force Survey 2021. Ushiriki wa vijana kwenye kilimo kumeporomoka kutoka 65.2  mwaka 2014 hadi 55.6% mwaka 2021. Mbali na jitihada ila bado changamoto  ni nyingi ukosefu wa ardhi, mitaji na masoko ya uhakika.

Serikali ilikuja na Mradi wa BBT (Building Better Tommorow ) wenye component 5 mimi nazungumzia moja ya Block Farms /Mashamba ya pamoja ilianza 2023. Ambapo vijana wamewekwa kambi huko Dodoma Chinangali na Ndogowe kulima mahindi, alizeti, pilipili. Awamu ya kwanza walikuwa vijana 800. Kwa uchungu naomba kumueleza Mhe.Bashe Waziri wa kilimo anajitihada kutaka matokeo lakini naomba nimwambie mradi wa BBT unakufa au umeshakufa asipouwahi. Sababu hana watendaji imara kwenye wizara yake, Sekretariati ya Wizara na Mratibu wa BBT Bi. Vumilia hawampi Waziri taarifa za kweli. Hadi sasa huko Chinangali ekari 300 za mahindi zimekauka zote sababu ya ukosefu wa mvua, Tume ya umwagiliaji hadi sasa haijaweka miundombinu ya umwagiliaji wanamwagilia kwa mikono, kuliuzwa mavuno ya alizeti million 100 ila million 60 vijana waligawana laki laki ili kujikimu sababu walistishiwa fedha ya kujikimu 240,000 kwa mwezi, Waziri afuatilie katika makambi huko Chinangali na ndogowe namna vijana wanavyoteseka kutafuta fedha ya kujikimu inafikia hatua mtu akipewa mifuko 3 ya mbolea kwenye shamba lake anauza mmoja ili apate fedha ya kujikimu.Vijana wanapungua kila ukichwa hadi sasa vijana 400 hawafiki katika makambi yote 2. Vijana wenzangu tusimame,tuungane  na tupaze sauti zetu dhidi ya ukosefu wa ajira na hatma yetu.

Kuna haja ya wizara kutafakari upya namna ya kuwezesha vijana kwenye kilimo  mashambani kuna vijana wanazalisha tayari wapo mashambani wakawezeshwe, huko Njombe, viazi kijana shamba kukodisha laki moja kwa msimu kwa ekari. Singida ni mkoa wa 3 maskini Tanzania. Wao ndio leading uzalishaji wa alizeti Tanzania kwa  48.8% , wana viwanda vina hitaji malighafi tani.434,725 kwa mwaka (Mount Meru kikubwa, medium 3, small 115 ) ila uzalishaji wao ni tan.160,000, tuwasaidie vijana huko shambani walime zaidi kuongeza Quantity ya uzalishaji,kuna upungufu wa malighafi tan.274,725. Uzalishaji wetu wa mafuta ya kula hapa kwetu ni tani 290,000 ikiwa mahitaji ni zaidi ya tani 650,000 zaidi ya Bil 700 tunatumia kuagiza  mafuta ya ziada nje. Ngano uzalishaji wa ngano TZ ni tani 10,000 ikiwa mahitaji kwa mwaka ni tani 1,000,000 upungufu 900,000 (90%). Vijana wenzangu tusimame,tuungane na tupaze sauti zetu dhidi ya ukosefu wa ajira na hatma yetu.

Tuwe huru kuongea, tujadiliane, tushikamane na kupaza sauti zetu kuhoji hatma yetu. Ahsanteni.

Abdul Nondo
Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana Taifa ACT Wazalendo

Hot this week

Mnyonge, mnyongeni ila haki yake mpeni

By Dorlingson Edward Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), leo...

CHADEMA kutoa msimamo wake kuhusu maridhiano

By Veronica Mlyatu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa...

Popular Articles

Safari ya Mashimba katika kutetea jamii ya Wahadzabe

Nchini Tanzania  kuna jumla ya makabila zaidi ya 120...

Polisi waendelea kuwashikilia viongozi wa CHADEMA

Ni siku ya kwanza tangu kukamatwa kwa viongozi wa...

Siku ya Vijana Duniani.

Kwa sasa ni kijana wa miaka 25 ambaye amejiajiri...

BWAWA LA ARBA’AT  LASABABISHA MAAFA NCHINI SUDAN

Watu 30 mashariki mwa Sudan na na wengine 60...

Sand Mining in Tanzania: Trails of Destruction in Lake Victoria and its Environs

By Dominic Allen On November 14th, 2021 in the Geita...

 Utekaji: Fumbo linalotushinda?

Na Yohani Gwangway Taifa la Tanzania kwa miaka mingi limekuwa...

Abduction: Is it a riddle we can’t solve?

By Yohani Gwangway For many years Tanzania has been an...

Mustakabali wa Hewa Safi kwa kila kiumbe

Na Dominic Allen Msingi wa maisha ya viumbe hai yaani...
LAND DWELLERS FACT CHECK HUB VERIFY FACTS STOP MISINFORMATION Trusted Fact-Checking in Tanzania Beyond What You Know VERIFY NOW

Related Articles

Popular Categories

DWELLERS CHECK-HUB Verify Facts. Stop Misinformation Trusted Fact-Checking in Tanzania • Beyond What You Know VERIFY NOW