Na Dominic Allen
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe amesema kuwa serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya nchini imeendelea kuwekeza katika teknolojia za urutubishaji wa vyakula kwa lengo la kuimarisha afua za lishe, ili kukabiliana na upungufu wa madini na vitamini kwa jamii.
Kigahe ameeleza hayo jana Aprili 03, 2025 wakati wa uzinduzi wa kanuni za uongezaji wa virutubishi kwenye vyakula za mwaka 2024, ambao ulifanyika Songea mkoani Ruvuma.
Katika uzinduzi wa kanuni hizo za uongezaji wa virutubishi kwenye vyakula, Kigahe amelielekeza Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kutoa elimu kwa wadau wote wanaotakiwa kufuata kanuni hizo, ikiwemo wazalishaji wa vyakula nchini na kupitia upya viwango vyao ili viendane na kanuni hizo.
“Napenda kutamka kuwa Wizara inatoa miezi saba kuanzia leo, utekelezaji wa kanuni hizi uanze kutekelezwa, namaanisha mpaka ifikapo mwishoni mwa mwezi Novemba, 2025.” Alisema Naibu Waziri Kigahe.

Picha na Wizara ya Afya.
Hata hivyo Naibu Waziri Kigahe ametoa wito kwa wananchi wote nchini kuunga mkono juhudi za serikali za kufikia malengo ya kuimarisha afua za lishe katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa madini na vitamini kwa jamii.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Waziri wa Afya, Mkurugenzi wa Mafunzo wa Wizara ya Afya, Dkt. Saitore Laizer amesema Serikali inaendelea kushirikiana na wadau kupanua wigo wa urutubishaji na kuzindua mpango wa kitaifa wa kurutubisha chakula kwa kutumia madini chuma, zinki, vitamini B12 na folic ya asidi kwa unga wa ngano, mahindi na vitamini A kwa mafuta ya kula.
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


