MISA: Miradi ya hewa ukaa ya udongo Kaskazini mwa Tanzania, kuumiza Jamii ya Kimaasai

Na Dominic Allen

Muungano na Mshikamano wa Kimataifa wa Maasai (MISA) wiki hii umetoa ripoti ya uchunguzi wa kina kuhusu miradi ya biashara ya hewa ukaa ya udongo Kaskazini mwa Tanzania, ambapo imebainisha kuwa kuna uwezekano jamii za kimaasai zikaathirika pakubwa na miradi hiyo, ikiwemo upokaji wa ardhi ambayo ndiyo msingi wa uendeshaji wa maisha yao.

Ripoti hiyo ambayo imemulika wilaya za Longido, Monduli na Simanjiro imepewa jina la “Biashara ya Hewa Ukaa ya Udongo: Wimbi Jipya la Upokaji Ardhi Kaskazini mwa Tanzania” imejikita kuchambua miradi mikuu miwili ya hewa ukaa ya udongo ambayo ni The Longido and Monduli Rangelands Carbon Project (LMRCP) chini ya kampuni ya Soil for the Future Tanzania Ltd (SftFTZ) wakifadhiliwa Volkswagen ClimatePartners na  mradi mwingine ni The Resilient Tarangire Ecosystem Project (RTEP) unaoendeshwa na The Nature Conservancy (TNC).

Miradi hii ya hewa ukaa ya udongo imeibua mashaka makubwa kwa watetezi wa haki za binadamu hasa kwa wale wanaotetea haki za watu wa jamii za asili kutokana na hofu kuhusu namna mchakato mzima ulivyofanyika katika uanzishwaji na utekelezaji wa miradi hiyo, pamoja na athari zake kwa wafugaji wa jamii za kimaasai katika maeneo hayo.

Mradi wa The Longido na Monduli Rangelands Carbon Project (LMRCP) unaosimamiwa na kutekelezwa na Soil for the Future Tanzania Ltd (SftFTZ) kwa kushirikiana na CarbonSolve LLC, Volkswagen ClimatePartner, Converge Analytics pamoja na Biodiversity Research Institute, utadumu kwa kipindi cha miaka 40 na umechukua heka 970,000 ambao umelenga vijiji 49 vya wilaya ya Longido na vijiji 10 vya wilaya ya Monduli mkoani Arusha.

Kampuni hii ya Soil For Future pia inahusika na utekelezaji wa miradi mitatu kama hii nchini Kenya, ikiwemo mradi wa kaskazini mwa nchi hiyo maarufu kama Northern Rangelands Trust (NRT), yote ikigubikwa na mashaka kutoka kwa watetezi wa haki za binadamu.

Katika ripoti yenye jina “Watu hawa wameuza hewa yetu” iliyotolewa Machi 2023 na Shirika la Survival International, ilibainisha kuwa kampuni ya Soil For Future ilianza kutekeleza mradi wa hewa ukaa wa NRT tangu Januari 2013, ukichukua eneo linalokaliwa na watu zaidi ya 100,000 wa jamii za asili za Samburu, Masai, Borana na Rendille.

Kwa mujibu wa ripoti ya Survival International, mradi wa NRT umeathiri mifumo ya ufugaji wa jamii za asili katika maeneo hayo, umeharibu utamaduni wa jamii hizo pamoja na kuhatarisha hali ya usalama wao wa chakula, huku kukikosekana uwazi, mashauriano na idhini au uhiari wa jamii katika mradi huo.

Ni wazi kuwa kilichofanywa na Soil For Future nchini Kenya pia kimetokea nchini Tanzania, hii inatia doa kampuni hii ambayo inajinadi kuwa inajali mustakabali wa mazingira, kwani ripoti iliyotolewa na MISA wiki hii, imebaini kuwa hakukuwa na uwazi kuhusu mikataba iliyosainiwa ya miradi hiyo, huku kukiwa na ushirikishwaji hafifu wa jamii katika mchakato mzima wa kuanzishwa kwake.

Mradi wa huo nchini Kenya unaosimamiwa na Soil for the Future pia unahusishwa na ukiukaji wa haki za binadamu.

Mnamo mwaka 2021 wanajamii walioathiriwa na mradi wa hewa ukaa wa NRT Kaskazini mwa Kenya waliiburuza Mahakamani kampuni hii kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo unyanyasaji wa watu wa jamii za asili.

Kesi hiyo kwa kiasi ilizaa matunda ambapo mwanzoni mwa mwaka huu Mahakama iliamuru kuwa walinzi wa mradi wa NRT wenye silaha nzito ambao walihusika na ukikaji wa haki za binadamu kwa watu wa jamii za asili, waondoke katika maeneo ya uhifadhi.

Mama wa kimaasai akikamua ng’ombe maziwa. Picha na MISA

Tukirejea katika ripoti ya MISA ya “Biashara ya Hewa Ukaa ya Udongo: Wimbi Jipya la Upokaji Ardhi Kaskazini mwa Tanzania” inatutahadharisha kuwa mambo kama haya yaweza kuwakumba wafugaji wa jamii za kimaasai kaskazini mwa Tanzania kutokana na historia yenye ukakasi kwa kampuni ya Soil For the Future kwa majirani zetu wa Kenya.

Ripoti ya MISA pia imechunguza mradi wa The Resilient Tarangire Ecosystem Project (RTEP), unaoendeshwa na Shirika la The Nature Conservancy (TNC) wakishirikiana na TerraCarbon pamoja na Tanzania People and Wildlife (TPW), ambao unafadhiliwa na Taasisi ya UK Darwin Initiative kutoka nchini Uingereza.

Mradi huu utadumu kwa miaka 20, kuanzia October 1, 2020 hadi September 30, 2040, huku kukiwa na uwezekano wa kuongeza mkataba pindi utakapoisha.

Mradi wa The Resilient Tarangire Ecosystem Project (RTEP) umechukua heka 830,000, ukilenga vijiji 49 na Hifadhi moja ya Wanyapori katika wilaya za Longido, Monduli na Simanjiro.

Shirika la The Nature Conservancy (TNC) limesema kuwa limeishirikisha jamii ipasavyo  katika mchakato mzima wa mradi huu, na kwamba jamii ilipatiwa mafunzo kuhusiana na hewa ukaa ya udongo pamoja na ushirikishwaji wa wanawake, vijana na makundi maalum.

Licha ya Shirika la TNC kusema hayo, lakini miongoni wa mambo yaliyoibuliwa na ripoti ya MISA ni kukosekana kwa ushirikishwaji (FPIC) wa jamii katika mchakato mzima wa uanzishwaji wa miradi hiyo ya hewa ukaa ya udongo, na kubainisha kuwa katika miradi yote hiyo ya hewa ukaa kaskazini mwa Tanzania, kuna ushirikishwaji finyu wa jamii, usiowahusisha wanawake na vijana pamoja na kukosekana kwa uwazi kwenye mikataba.

Hii siyo mara ya kwanza Shirika la TNC kunyooshewa kidole, kwani mujibu wa taarifa ya iliyochapishwa Agosti 03, 2014 na gazeti la The New York Times nchini Marekani, mnamo mwaka 2014 shirika hili lilikosolewa vikali na wanaharakati wa mazingira kwa kuruhusu uchimbaji wa mafuta na gesi katika eneo la hifadhi huko Texas nchini Marekani, na kujipatia mamilioni ya fedha kama mirabaha.

Kashfa hii inaleta ukakasi juu ya dhamira halisi ya shirika hili ambalo linaendesha na kusimamia mradi wa The Resilient Tarangire Ecosystem Project (RTEP) kaskazini mwa Tanzania.

Sehemu ya ramani ya Tanzania na Kenya ikionesha maeneo ya miradi ya hewa ukaa ya udongo.
Ramani na MISA.

Uchunguzi uliyofanywa na MISA, umetahadharisha kuwa miradi hii ya hewa ukaa ya udongo huenda ikasabisha upokaji wa ardhi kutoka kwa jamii za wamaasai, kwani kuna kila dalili za unyang’anyi wa ardhi kutokana na mikataba kutowekwa wazi , ushirikishwaji mdogo wa jamii, kukiwa na hofu kuhusu wawekezaji wa kigeni kuchukua ardhi za wenyeji, huku na nyanda za malisho kubinafisishwa.

Katika ripoti ya MISA mapendekezo kadhaa yametolewa, ikwemo kusitishwa kwa muda wa miaka mitano kwa miradi yote ya hewa ukaa ya udongo katika maeneo ya malisho ya wamaasai, ili kutoa nafasi ya elimu kwa jamii pamoja na kuandaliwa kwa mifumo thabiti ya kisheria  katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.

Kutengeneza mfumo maalum wa kisheria kwa miradi ya hewa ukaa ya udongo, kuhakikisha ulinzi wa haki za binadamu na haki za ardhi kwa jamii za asili.

Ripoti pia imesisitiza kuwa jamii nzima inapaswa kushirikishwa kikamilifu na mikataba inayohusu miradi hii iwekwe wazi kwa jamii. Lakini pia kuwepo na upatikanaji huru wa kisheria na taarifa zisizo na upendeleo kuhusu biashara ya hewa ukaa na athari zake.

MISA imetaka uendeshwaji wa miradi ya hewa ukaa iheshimu mifumo ya asili ya ufugaji wa Wamaasai, pia kutozuia mfumo wa asili wa wamaasai wa kuhama kutoka eneo moja kwenda jingine, ambapo pia imesisitiza juu ya ushirikiano wa maeneo ya nyanda za malisho hasa kipindi cha ukame.

Ripoti ya MISA pia imetaka mikataba ya miradi ya hewa ukaa iwe ya wazi na haki, iandikwe kwa lugha ya wenyeji na pia isiwe na upendeleo kwa maslahi ya waendeshaji wa miradi hiyo na serikali.

Uchunguzi huu wa MISA umetufumbua macho kutazama kwa jicho la tatu siyo tu miradi ya hewa ukaa ya udongo, bali pamoja na miradi mingine ambayo uwepo wake hapa nchini ni maumivu kwa wazawa.

Mashirika ya kuteteka haki za binadamu pamoja na wanaharakati wanatakiwa kupaza sauti dhidi ya miradi ambayo inauwaumiza wananchi na wala haina tija kwa kwa maendeleo ya taifa.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inapaswa kupitia upya Sera, Sheria na Kanuni zinazohusu uwekezaji hapa nchini ili kuhakikisha kuwa hakuna uonevu wala unyonyaji wa wananchi, pamoja na kulinda rasilimali za nchi.

Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway

Hot this week

CHADEMA kutoa msimamo wake kuhusu maridhiano

By Veronica Mlyatu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa...

Mnyonge, mnyongeni ila haki yake mpeni

By Dorlingson Edward Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), leo...

Popular Articles

Safari ya Mashimba katika kutetea jamii ya Wahadzabe

Nchini Tanzania  kuna jumla ya makabila zaidi ya 120...

Polisi waendelea kuwashikilia viongozi wa CHADEMA

Ni siku ya kwanza tangu kukamatwa kwa viongozi wa...

Siku ya Vijana Duniani.

Kwa sasa ni kijana wa miaka 25 ambaye amejiajiri...

BWAWA LA ARBA’AT  LASABABISHA MAAFA NCHINI SUDAN

Watu 30 mashariki mwa Sudan na na wengine 60...

Sand Mining in Tanzania: Trails of Destruction in Lake Victoria and its Environs

By Dominic Allen On November 14th, 2021 in the Geita...

 Utekaji: Fumbo linalotushinda?

Na Yohani Gwangway Taifa la Tanzania kwa miaka mingi limekuwa...

Abduction: Is it a riddle we can’t solve?

By Yohani Gwangway For many years Tanzania has been an...

Mustakabali wa Hewa Safi kwa kila kiumbe

Na Dominic Allen Msingi wa maisha ya viumbe hai yaani...
LAND DWELLERS FACT CHECK HUB VERIFY FACTS STOP MISINFORMATION Trusted Fact-Checking in Tanzania Beyond What You Know VERIFY NOW

Related Articles

Popular Categories

DWELLERS CHECK-HUB Verify Facts. Stop Misinformation Trusted Fact-Checking in Tanzania • Beyond What You Know VERIFY NOW