Na Dominic Allen
Wizara ya Afya nchini Tanzania hii leo imesema kuwa watu wawili wamegundulika kuwa na maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Mpox, ambapo miongoni mwao ni dereva wa mizigo aliyetoka nje ya nchi kuelekea jijini Dar es Salaam.
Taarifa ya Wizara imeeleza kuwa mnamo Machi 07, 2025 ilipokea taarifa za wahisiwa wenye dalili za vipele usoni, mikononi, miguuni na sehemu nyingine za mwili ambapo dalili hizo ziliambatana na maumivu makali ya viungo vya mwili.
Baada ya kupokea taarifa za wahisiwa hao, sampuli zilipelekwa Maabara ya Taifa kwa uchunguzi zaidi, na majibu yaliyotolewa na maabara hapo jana yalithibitisha kuwa wahisiwa wawili wana maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugojwa wa Mpox.
Wizara ya Afya imeongeza kuwa kwa kushirikiana na TAMISEMI bado inaendelea kufuatilia kwa ukaribu zaidi kubaini wahisiwa wengine ili wapatiwe huduma stahiki.
Hata hivyo Wizara ya Afya imewahakikishia wananchi kuwa imejipanga kikamilifu kuudhibiti ugonjwa wa Mpox kutokana na uzoefu walionao katika kudhibiti magonjwa ya mlipuko, huku ikiwataka wananchi kuchukua tahadhari za kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo, ikiwemo kuwahi katika kituo chochote cha afya pindi anapoona dalili za ugonjwa huo, kuepuka kugusana kwa kupeana mikono au kukumbatiana na mtu mwenye dalili za Mpox pamoja na kuchukua tahadhari zingine.
Chanzo cha ugonjwa wa Mpox ni wanyama jamii ya nyani, ambapo binadamu anaweza kuupata kwa kugusana na wanyama, majimaji au nyama zenye maambukizi, na endapo binadamu akipata maambukizi hayo huweza kumuambikiza mwingine kwa njia ya kugusana moja kwa moja.
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


