Na Dominic Allen
Meneja wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Mashariki Kaskazini, Glory Kombe ametoa wito kwa wanaojishughulisha na uuzaji wa chakula ‘Mama Lishe’ kuacha kutumia mifuko ya plastiki kuhifadhia vyakula hasa vya moto kutokana madhara ya kiafya yanayosababishwa na matumizi ya mifuko hiyo.
Bi. Kombe ametoa wito huo leo, ambapo ameeleza kuwa matumizi ya mifuko ya plastiki katika kuhifadhia chakula cha moto husababisha magonjwa mbalimbali ikiwemo saratani kutokana na sumu inayozalishwa na mifuko hiyo ambayo huingia kwenye chakula na kusababisha madhara kwa mlaji wa chakula hicho.
Ameongeza kuwa baadhi ya wanawake pia wamekuwa wakitumia mifuko ya plastiki kwa ajili ya kuwashia moto, ambapo amefafanua kitendo hicho pia kina madhara ya kiafya kwa kuwa mifuko hiyo huzalisha hewa ya sumu pindi inapochomwa, hivyo huleta athari za kiafya.

Wito huo wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) unafuatia baada ya uchunguzi ulifanywa na kuripotiwa na Land Dwellers mwezi Januari mwaka huu, ambao ulibaini bado kuna uzalishaji, uingizwaji, usambazaji na matumizi ya hali ya juu ya mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku hapa nchini licha ya katazo la serikali dhidi ya matumizi mifuko hiyo.
Uchunguzi wa Land Dwellers ulionesha kuwa miongoni mwa watumiaji wakubwa wa mifuko hiyo ni wauzaji wa vyakula kwenye migahawa ‘ Mama Lishe’, wakiitumia mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku kwa ajili ya kuhifadhia vyakula vya moto ili visipoe kwa haraka.

Land Dwellers ilitoa rai kwa Wizara husika na Taasisi zinazohusika na mazingira ikiwemo Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na taasisi zingine kutengeneza mtandao wa pamoja utakaoboresha zaidi ushirikiano wao katika kupambana na suala la matumizi ya mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku nchini.
Meneja wa NEMC Kanda ya Mashariki Kaskazini, Glory Kombe ametoa wito huo kwa Mama Lishe, kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Machi 08, 2025 ambapo ameeleza kuwa wanawake wana nafasi kubwa katika utunzaji wa mazingira.
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


