Na Amiri Kilagalila
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea na jitihada za kuboresha miundombinu katika Bandari ya Dar es Salaam, ili kupunguza changamoto kubwa ya usafirishaji wa bidhaa ikiwemo matunda ya parachichi ambayo imekuwa ikisababisha wakulima kupeleka bandari zilizopo nchi jirani.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Tanzania Horticulture Association (TAHA), Dkt. Jacqueline Mkindi ameeleza hayo jana Mei 08, 2025 mkoani Njombe wakati wa uzinduzi wa vituo vya kukusanyia mazao ya horticulture mkoani humo, baada ya wawekezaji kueleza changamoto hiyo.
“Kwa sasa hivi 80% ya kontena za parachichi kwa hawa wasafirishaji bado zinapita Mombasa na unaona wawekezaji wako tayari kupita Mombasa na sio Dar es Salaam, kwanini? Ni kwa sababu ya uwezo kuondokana na mambo mengine mengi lakini tunashukuru serikali kunamaendeleo makubwa yanafanyika Dar es Salaam” amesema Dkt. Mkindi.
Dkt. Mkindi amesema changamoto hizo zinakwenda kutatuliwa kwa kipindi kifupi kijacho kwa sababu kipindi cha nyuma asilimia 100 ya wawekezaji walikuwa wakipita Mombasa, na mabadiliko makubwa yameanza ambapo kuanzia mwaka 2021 asilimia 15 mpaka 20 ya kontena zinapita Bandari ya Dar es Salaam.

Meneja wa Avodemia, Mohamed Adam Jee ambao ni wawekezaji na wasafirishaji wa parachichi, amesema uhitaji wa parachichi za Tanzania maeneo mbalimbali duniani ni mkubwa lakini wamekuwa wakipata shida na kutumia gharama kubwa kusafirisha zao hilo, huku wakilazimika kutumia bandari ya nje ya Tanzania kutokana na changamoto ya miundombinu iliyopo katika Bandari ya Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo, nchini Tanzania uzalishaji wa zao la parachichi zinazouzwa nje ya nchi (exportable varieties) umeongezeka kutoka tani 17,711.49 mwaka 2021/2022 hadi tani 26,826.3 mwaka 2022/2023.

Nae Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Dkt. Hussein Mohamed Omari amesema serikali inafanyia kazi changamoto hizo ambapo pia imeongeza bajeti kwenye sekta ya kilimo kutoka Tsh. Bilioni 294 hadi Tsh. Trilioni 1.28, ambapo ameongeza kuwa ujenzi wa vituo vya kupimia na kukusanyia parachichi vilivyojengwa na TAHA ni mkombozi kwa wakulima.

Jumla ya vituo vitano vya kukusanyia mazao ya horticulture vimezinduliwa mkoani Njombe ikiwa ni sehemu ya kuboresha miundombinu ili kupunguza upungufu wa upotevu wa mazao.
Mwandishi: Amiri Kilagalila
Mhariri: Dominic Allen


