Na Dominic Allen
Ofisi ya Kupambana na Rushwa kwa Maafisa wa ngazi za Juu (CIO) nchini Korea Kusini imependekeza kuwa Yoon Suk Yeol ambaye alikuwa Rais wa nchi hiyo kabla ya kuondolewa madarakani, ashtakiwe kwa uasi na matumizi mabaya ya ofisi baada ya kutangaza nchi hiyo kuongozwa na sheria ya kijeshi mnamo Disemba 03, 2024, sheria ambayo ilidumu kwa saa kadhaa.
CIO imetoa mapendekezo hayo leo Alhamisi ikiomba waendesha mashtaka kufungua mashtaka hayo baada ya kubaini kuwa Yoon alivuruga utaratibu wa kikatiba wa nchi hiyo.
Hata hivyo Ofisi ya Waendesha Mashtaka ya Seoul itakuwa na siku 11 kuamua kama itamshtaki Yoon kumpeleka mahakamani.
Yoon Suk Yeol aliondolewa madarakani na Bunge la Korea Kusini tangu Disemba 14, 2024 na alikmatwa na Polisi juma lililopita baada ya kukataa wito wa maafisa wanaochunguza tuhuma ya matumizi mabaya ya ofisi dhidi yake, ambapo mwanasheria wa Yoon amesema kuwa kukamatwa kwake ni kinyume na sheria.
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


