Kutoka Ziwa Victoria hadi Hong Kong: Wavuvi wazawa wanavyokosa fursa ya mabondo

Na Yohani Gwangway

Katika mialo ya Sweya, Buhongwa na Kirumba mkoani Mwanza, kuna biashara inayofanyika chini kwa chini, huku wavuvi wadogo wazawa wakiendelea kusota na umasikini. Ni rasilimali inayojulikana kama “dhahabu nyeupe” mabondo ya samaki ambayo husafirishwa kwa wingi kuelekea mataifa ya Asia, hasa Hong Kong.

Mabondo ya samaki ni viungo vya ndani vinavyofanana na puto au kibofu ambavyo humsaidia samaki kujaza hewa ili aweze kuelea na kubadili mwelekeo anapokuwa majini. Mabondo yenye thamani kubwa ya kibiashara yanatoka katika samaki aina ya Sangara (Nile Perch) anayepatikana kwa wingi katika Ziwa Victoria.

Hali halisi

Biashara ya mabondo ya Samaki hasa Sangara ni biashara ambayo imekuwa ikifanyika bila kuwa na usimamizi mzuri licha ya kuwa bei ya mabondo inawanufaisha madalali na wafanyabiashara wageni. Wavuvi wazawa ambao huvua kila siku wanauza samaki na baadaye walanguzi hutofautisha samaki na mabondo kwa kufanya upasuaji na kuyakusanya mabondo.

Zabron Chananja ambaye ni Mvuvi katika kijiji cha Mwasonge anadai kuwa katika eneo lao hakuna biashara ya mabondo. Wao wanauza tu samaki na baadaye walanguzi na mdalali ndiyo hutofautisha samaki na mabondo ili kuyauza mabondo kwa bei yao.

“Wavuvi ambao huingia ziwani kufanya uvuvi wa samaki wakubwa hasa sangara wanakaa ziwani kwa muda wa wiki moja hadi mwezi mmoja wakati mwingine. Wakitoka kule wanagawana faida na tajiri aliyewatuma. Faida hii ni ya samaki tu na siyo kitu kingine. Sasa huyo tajiri(mlanguzi) anapotoka hapo yeye ndiye anaamua samaki anauzia wapi na mabondo anauzia wapi.” Zabron Chananja akizungumzia biashara ya Mabondo.

Akizungumzia suala hili mvuvi mwingine kutoka kijiji cha Mwasonge, Frank Musa anasema wavuvi wa ndani hawafanyi biashara hii kwa sababu mwisho wa siku hawana mahali pa kuuzia. Kwa mujibu wa Frank, hakuna namna ambayo wavuvi wa ndani (wazawa) wanaweza kufanya biashara kwa sababu mwisho wa siku hawana viwanda vya kusindika na pia hawana soko la kupeleka nje na soko la wageni.

“Ni ngumu wavuvi wazawa kufanya biashara ya mabondo. Inajulikana ukifanya lazima upeleke kiwandani. Sasa hakuna viwanda vya wafanyabiashara wazawa. Mwisho wa siku wavuvi wanaona bora tu wauze samaki na siyo mabondo. Upande wa bei pia haieleweki. Wanaopanga bei haijulikani na akina nani,” Frank kuhusu biashara ya mabondo kwa wavuvi wazawa

Mitumbwi ya wavuvi ikiwa imeegeshwa katika moja ya mialo ya Ziwa Victoria, Mwanza. Picha: Yohani Gwangway

Uchunguzi wa Land Dwellers uliohusisha kuuliza kwa wavuvi wazawa, vyanzo mbalimbali vya taarifa na ripoti za kimataifa zimeonesha kuwa kuna angalau hatua 6 za biashara ya mabondo hadi kufikia soko la Asia. Katika hatua hizi faida inayotokana na kuongezeka kwa thamani inayobaki hapa nchini ni ndogo kutokana na uhalisia wa wafanyabiashara wanaotawala biashara ya mabondo.

Ulanguzi wa mabondo Ziwa Victoria

Kifungu cha 22 (1) cha Sheria ya Uvuvi ya mwaka 2003 inakataza mtu yeyote asiye na leseni kufanya shughuli za uvuvi au biashara ya samaki. Sheria hiyo inataka kila mtu asajiliwe ili aruhusiwe kufanya shughuli za uvuvi ikiwa ni pamoja na usafirishaji wa mazao ya samaki kwenda nje ya nchi. Pia Kanuni ya Uvuvi ya mwaka huo, Kanuni ya 20 inasema kuwa hairuhusiwi kusafirisha nje bidhaa za samaki ambazo hazijapitishwa kwenye kituo kilichoidhinishwa, au kusafirisha bidhaa zisizokaguliwa.

Hata hivyo, biashara ya mabondo nchini Tanzania hasa upande wa Ziwa Victoria inafanyika bila kuzingatiwa kwa sheria pamoja na kanuni hii kwa kiasi fulani jambo linalosababisha kufanyika kwa biashara ya mabondo ambayo hupelekwa nje ya nchi. Baadhi ya wavuvi ambao wamezungumza wanasema kuwa biashara ya mabondo nchini Tanzania imekuwa ikifanyika kwa ulanguzi kutoka kwa wafanyabishara kutoka nje hasa wengi wao wakiwa kutoka China. Katika maeneo ya Sweya, Mswahili, Mwasonge, na Buhongwa wavuvi wanaouza samaki wanatoa kwanza mabondo na baadaye kuuza kwa bei rahisi kwa madali ambao baadaye wao huuza tena kwa wafanyabishara wa China.

Kwa wa wavuvi wanadai kuwa, baadhi ya wafanyabishara wa China hawaingizi mabondo katika mifumo rasmi ya kodi hivyo kukwepa kulipa kodi na kuisababishia hasara taifa. Matokeo yake wafanyabishara wa ndani wanapata faida kidogo kutokana na biashara hiyo huku serikali ikikosa mapato kutokana na baadhi ya wafanyabishara wanaotumia njia zisizo rasmi kusafirisha bidhaa hiyo kwenda nje ya nchi

Ripoti ya mwaka 2018 yenye jina “Chinese markets deplete Lake Victoria’s Nile perch” iliyoandikwa na taasisi ya Institute for Security Studies (ISS Africa) mwaka 2023 inasema kwa ujumla nchi za Kenya, Uganda na Tanzania kwa pamoja zilisafirisha tani 1,747 za mabondo kwenda Hong Kong mwaka 2018 zenye thamani ya karibu dola za Marekani milioni 124.

Ripoti hiyo inaonyesha biashara hiyo iliingiza rasmi takriban dola milioni 86 pekee kwa uchumi wa Afrika Mashariki,hivyo tofauti ya karibu dola milioni 38 sawa na karibu Shilingi bilioni 100 za kitanzania ilipotea kupitia madalali na biashara zisizo rasmi.

Ripoti nyingine yenye jina Maw Trade: A rapid assessment of the trade in fish swim bladders from Africa to Hong Kong SAR inaonesha simulizi ya vijana wanaochangamkia biashara ya mabondo Ziwa Victoria ambao bado hawapati faida ya kutosha kutokana na kuingiliwa na wafanyabishara kutoka nje au hata mdalali kutoka ndani ya Tanzania.

Kwa mujibu baadhi ya wavuvi, viwanda vya kigeni ambavyo kwa kiasi kikubwa humilikiwa na mataifa ya bara la Asia, vimesambaza walanguzi wa mabondo ya samaki katika mialo na visiwa vingi katika Ziwa Victoria. John Emanuel ambaye ni mvuvi katika mwalo wa Kirumba anasema kuwa licha ya kwamba mabondo haya yanaenda kwenye viwanda vya kigeni, lakini walanguzi wengi ni wazawa ambao hata siyo wavuvi.

“Hawa wachina sijui Wakorea mwanzoni walikuwa wanakusanya mabondo wao wenyewe, lakini kwa sasa wameweka walanguzi kwenye maeneo mengi. Walanguzi wanaweza kununua mabondo moja kwa moja au wakanunua samaki ili kupata mabondo. Sisi wavuvi hatuna kitu tunachoambulia. Hili jambo lingeangaliwa na serikali. Hapa tukikataa, hatuna pa kupeleka mabondo.”

Ali Suleiman (si jina halisi) ambaye amefanya kazi miaka 10 na kuweka ofisi zake katika eneo la Ghana jijini Mwanza na kisiwa cha Goziba kisiwani Ukerewe anasema kuwa wavuvi wa kawaida hawaambulii chochote katika biashara ya mabondo kwa sababu nyingi ikiwemo za kisera na kiuelewa. Akizungumzia sababu za kiuelewa, Ali anasema kuwa wavuvi wengi hawajui bei ya mabondo jambo linalosababisha kuuza kwa hasara.

“Mfano mwaka 2019 mimi nilinunua bondo kule Ukerewe katika kisiwa Goziba lenye uzito wa kilogramu  3.5 kwa shilingi 270,000 na kuuza kwa shilingi 4,600,000 kwa Wachina. Ukitoa bei niliyonunulia hapo unaona nilipata zaidi ya 4,000,000 kama faida. Wavuvi wa kule visiwani hawajui faida hii. Hawajui mabondo yana bei kiasi gani ndiyo maana wanauza kwa bei rahisi.”

Akizungumzia upande wa Kisera, Ali anasema kuwa wavuvi hawatapata faida yoyote bila serikali kufanya uwekezaji kwenye mabondo ili kusaidia wavuvi wazawa. Kwa mujibu wa Ali, uwekezaji kutoka nje kwenye suala la mabondo unanyonya wavuvi wazawa na kufaidisha madalali na wawekezaji kutoka China ambao wanaamua soko kutokana na serikali kutowekeza.

“Hii biashara itaendelea kuwa ngumu kama serikali yetu haitaanzisha viwanda hapa Tanzania. Ukiangalia hakuna kiwanda cha serikali. Viwanda vya China vinatumia Walanguzi wa mabondo ambao wanaamua bei ya mabondo. Mwaka 2019 wakati wa Covid19 bei ya mabondo ilishuka kabisa baada ya mipaka kufungwa. Kulikuwa hakuna namna ya kusafirisha mabondo. Tungekuwa na viwanda vya ndani vingenunua mabondo ili kusaidia wavuvi na baadaye kuuza.”

Kwa Mujibu wa Ali, biashara ya mabondo ambayo licha ya kufanyika imegubikwa na usiri mwingi, inaendelea kunufaisha walanguzi na wafanyabiashara kutoka nje ambao hupanga mabondo hayo kwenye madaraja tofau tofauti kama daraja dogo, daraja la kati na daraja la mabondo makubwa.

Land Dwellers ilipotaka kufahamu kuhusiana na vibali na leseni ya kufanya biashara hii, Ali alionesha kuwa ni kweli, ili ufanye biashara hii na utambulike unahitaji vibali, lakini kwa visiwani walanguzi wengi hawana vibali kwa sababu hakuna usimamizi mzuri. Pia, wafanyabishara wanaotorosha mabondo kwenda Uganda hawana vibali ndiyo maana hawataki kupitisha upande wa Tanzania.

“Wachache wana vibali na leseni. Lakini kwa kiasi kikubwa wafanyabishara wengi hawana vibali. Ndiyo maana inakuwa rahisi kwao kufanya ulanguzi na kusafirisha mabondo kwenda nchi jirani ya Uganda.”

Ali anaeleza kuwa katika Ziwa Victoria hakuna eneo au sehemu maalumu ambayo biashara hii hufanyika. Jambo hili linafanya urahisi wa kuonekana kana kwamba biashara inayofanyika ni ya samaki tu.

Maoni wadau wa uvuvi

Juvenali Matagili ambaye ni Mkurugenzi wa Fisheries Union Organization yaani FUO amefanya kazi ya uvuvi kwa zaidi ya miaka 53. Matagili alianza kazi ya uvuvi mwaka 1964 na kuacha kazi hii mwaka 2017 ambapo kuanzia hapo alianza kupigania mabadiliko ya sera na sheria za uvuvi ili kuiunua maslahi ya wavuvi wazawa.

“Hata kodi ambayo sasa hivi Mamlaka ya Mapato inatoza kwenye mabondo ni kelele zetu kati ya mwaka 1999 na mwaka 2000 ambapo tuliwaambia kuwa samaki wana mabondo ambayo yanauzwa kwa faida kubwa lakini yalikuwa hayatozwi kodi na serikali inapoteza fedha nyingi.”

Kuhusiana na changamoto katika biashara ya mabondo kwa sasa Juvenali Matagili anasema hata viwanda ambavyo vinamilikiwa na wageni ambavyo vinatambuliwa kama viwanda havina hadhi hiyo kwa sababu hizo ni nyumba za kawaida ha hakuna uwekezaji wa hadhi ya viwanda.

“Nadhani ni jambo la ajabu kusema kuwa kuna viwanda vya mabondo. Lazima tutofautishe plant na viwanda (Industries). Hizi zilizopo ni nyumba tu za kawaida ambapo kinachofanyika ni kusafisha mabondo kwa kuondoa damu na kuanika ili yakauke”.  Anasema Matagili

Athari za biashara ya magendo ya mabondo kwa wavuvi

Akizungumzia suala la wavuvi wa ndani kutopata faida za mabondo, Juvenali anaeleza kuwa wavuvi wa ndani wanauza samaki kwa sababu hawana soko la kuuza mabondo.  Matokeo yake faida zingine zote baada ya samaki kuuzwa zinaenda kwa wamiliki wa viwanda ambao hutenganisha bidhaa za samaki.

“Wavuvi wa ndani hawana uhuru wa kuuza mabondo. Hawana pa kuuza, matokeo yake wanauza samaki akiwa na bidhaa zake zote kama ngozi, mapezi, mifupa, mafuta na mabondo. Baadaye yule mtu wa kiwandani anatenganisha hizi bidhaa na anategeneza faida kubwa wakati huyu Mvuvi ambaye ndiye anayefanya kazi kubwa anapata faida ya mauzo ya samaki tu.”

Katika mwalo wa Kirumba, baadhi ya wavuvi wanasema kuwa suala la uwekezaji katika mabondo kutoka nje linanyonya wavuvi wa ndani kwa sababu ya kukosa viwanda vya ndani. Husein Ally ambalo si jina halisi la mvuvi katika soko hili la Kirumba anasema kuwa;

“Sasa wavuvi wa ndani sisi hatuna pa kwenda. Ukilingangania bondo mwisho wa siku utalipeleka wapi? Hakuna viwanda au masoko ya ndani yanayotambulika ya kuuza mabondo. Wakati biashara hii inaanza ilionekana kama ni biashara ya madawa ya kulevya. Ni kama inaogopwa. Tangu kuanza kwake biashara ya mabondo haina uwazi wa namna inavyofanyika, bei halisi za mwisho na hata matumizi yake zinakopelekwa.”

Ukuaji wa kasi wa biashara hii tangu miaka ya 2000 umeleta fursa kubwa za kiuchumi kwa vijana mkoani Mwanza, lakini pia umeleta tishio kubwa kwa ikolojia ya Ziwa Victoria pamoja na vitendo vya uharamia, magendo, huku kukiwa na tuhuma za ukwepaji kodi katika biashara ya mabondo ya samaki.

Samwel Ngh’wani, Diwani wa Kata ya Kirumba anasema kuwa kwa kushirikiana na uongozi wa soko, wamekuwa wakipiga vita vikali tabia ya wafanyabiashara wa kigeni hususa ni kutoka nchi jirani na Asia kwenda kununua rasilimali za samaki na mabondo moja kwa moja visiwani kwa siri badala ya kutumia soko rasmi la Kirumba.

Kwa mujibu wa Samwel, biashara haramu ya giza inapofanyika ziwani au visiwani, inasababisha soko rasmi la Kirumba kukosa mizigo. “Hali hii inasababisha viwanda vya ndani kukosa malighafi, mabenki yaliyotoa mikopo kwa wavuvi kushindwa kurudisha fedha zao, na serikali za mitaa kukosa mapato ya ushuru”

Soko la Kimataifa la Samaki la Kirumba ndilo soko mama na kubwa kuliko yote kanda ya Ziwa Victoria, likihudumia kati ya wafanyabiashara 1,000 hadi 2,000 kila siku.

Ripoti ya utafiti iliyoandaliwa na International Organization for Migration (IOM) mwaka 2023 yenye kichwa cha habari Regional Assessment of Transnational Organised Crime and Integrated Border Governance on LakeVictoria iliyotolewa kwa ushirikiano na mashirika ya kimataifa inaainisha Ziwa Victoria kama eneo hatari na kutaja kuwa kati ya asilimia 40% hadi ya shughuli zote za uvuvi ziwani humo ni haramu au hazijasajiliwa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo mianya mikubwa ya usimamizi wa mipaka kati ya Tanzania, Kenya, na Uganda inatumiwa na mitandao ya magendo kusafirisha mabondo kinyume cha sheria kuelekea viwanja vya ndege vya kikanda kwa ajili ya kusafirishwa kwenda Asia.

Takwimu zilizotolewa na Institute for Security Studies (ISS), kwenye ripoti yake ya mwaka 2023 yenye kichwa cha habari “Chinese markets deplete Lake Victoria’s Nile perch” inasema kuwa uhitaji mkubwa wa mabondo huko Hong Kong unachochea uvuvi wa Sangara wachanga wenye uzito wa chini ya kilo moja.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wakati takwimu za serikali zikionyesha mauzo ya mabondo kushuka kutoka tani 838 hadi 433 zilitolewa rasmi na serikali zikilinganisha mwaka 2019 na mwaka 2023 huku soko la giza kimataifa linaonyesha uhitaji mkubwa. Inakadiriwa kuwa zaidi ya tani 400 hadi 600 za mabondo hutoroshwa kwa siri kila mwaka kwenda Asia kupitia njia za magendo.

“Kabla ya mdororo mkubwa wa soko la giza, sekta ya Sangara nchini Tanzania ilikuwa inaingiza zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 280 kwa mwaka. Thamani ya soko la ndani la kilo moja ya Sangara mzima ni kati ya TZS 8,000 hadi 12,000, lakini thamani ya mabondo yaliyokaushwa hufikia hadi USD $1,000 hadi $7,700 kwa kilo yakifika masoko ya kifahari ya Hong Kong,” inasema ripoti hiyo.

Afisa Uvuvi wa Mkoa wa Mwanza, Titus Kilo, anasema kuwa uvuvi haramu na biashara haramu ya mabondo ni miongoni mwa vyanzo vikuu vinavyosababisha kupungua kwa samaki aina ya Sangara katika Ziwa Victoria.

Kwa mujibu wa Kilo, uvuvi haramu umechochea kupungua kwa kasi kwa Sangara kutoka tani 537,479 mwaka 2020 hadi tani 335,170 katika mwaka 2021.

Kumekuwa na malalamiko makubwa katika mkoa wa Mwanza kwamba baadhi ya wavuvi haramu hukamata Sangara wakubwa, kuwapasua na kuchukua mabondo pekee (kwa sababu yana thamani kubwa na ni rahisi kuficha), kisha kutelekeza mizoga ya samaki ziwani.

Ni wakati sasa wa serikali kurekebisha mifumo ya usimamizi na kuanzisha mfumo wa kidijitali wa kufuatilia mabondo tangu yanapotolewa ziwani hadi yanaposafirishwa nje ya nchi ili kunasa mapato yanayopotea.

Mwandishi: Yohani Gwangway
Mhariri: Dominic Allen

Hot this week

Mnyonge, mnyongeni ila haki yake mpeni

By Dorlingson Edward Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), leo...

CHADEMA kutoa msimamo wake kuhusu maridhiano

By Veronica Mlyatu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa...

Popular Articles

Safari ya Mashimba katika kutetea jamii ya Wahadzabe

Nchini Tanzania  kuna jumla ya makabila zaidi ya 120...

Polisi waendelea kuwashikilia viongozi wa CHADEMA

Ni siku ya kwanza tangu kukamatwa kwa viongozi wa...

Siku ya Vijana Duniani.

Kwa sasa ni kijana wa miaka 25 ambaye amejiajiri...

BWAWA LA ARBA’AT  LASABABISHA MAAFA NCHINI SUDAN

Watu 30 mashariki mwa Sudan na na wengine 60...

Sand Mining in Tanzania: Trails of Destruction in Lake Victoria and its Environs

By Dominic Allen On November 14th, 2021 in the Geita...

 Utekaji: Fumbo linalotushinda?

Na Yohani Gwangway Taifa la Tanzania kwa miaka mingi limekuwa...

Abduction: Is it a riddle we can’t solve?

By Yohani Gwangway For many years Tanzania has been an...

Mustakabali wa Hewa Safi kwa kila kiumbe

Na Dominic Allen Msingi wa maisha ya viumbe hai yaani...
LAND DWELLERS FACT CHECK HUB VERIFY FACTS STOP MISINFORMATION Trusted Fact-Checking in Tanzania Beyond What You Know VERIFY NOW

Related Articles

Popular Categories

DWELLERS CHECK-HUB Verify Facts. Stop Misinformation Trusted Fact-Checking in Tanzania • Beyond What You Know VERIFY NOW